Mama Tunu Pinda ahimiza elimu kwa watoto wa kike

Na Mwandishi Wetu

MKE wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda ametoa wito kwa jamii kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuinua viwango vya elimu nchini na hasa kwa watoto wa kike.

Ametoa wito huo Jumamosi ya Agosti 4, 2012 wakati akizungumza na mamia wa wakazi wa mji wa Shirati, wilayani Rorya mkoani Mara walioshiriki harambee ya kuchangia ukarabati wa bweni la wasichana linalosimamiwa na Kanisa la Mennonite Tanzania (KMT), Dayosisi ya Mara Kaskazini. Ukarabati huo utagharimu sh. milioni 55.

“Nawaomba tuendelee kuisaidia Serikali kwani bado watoto hawa wanakabiliwa na matatizo mengi na wale wachache ambao wanapata msaada bado wanahitaji kupata msaada zaidi ili waweze kuhitimu masomo yao na waweze pia kusonga mbele,” alisema.

Mama Pinda ambaye pia alifungua kongamano la akinamama wa KMT, aliendesha harambee ya kufanikisha ukarabati wa jengo lililokuwa likitumiwa na wazee wenye ugonjwa wa ukoma ambalo sasa litageuzwa kuwa hosteli kwa ajili ya wasichana kati ya 80 na 100. Jumla ya sh. milioni 56 zilipatikana kwenya harambee hiyo ambapo sh. milioni 29.5 zilikuwa ni fedha taslimu na sh. milioni 26.6 zilikuwa ahadi.

“Kukamilika kwa hosteli hii ni ukombozi siyo kwa watoto hawa pekee bali kwa wazazi na kwa Taifa ujumla kwani tutakuwa tumewalinda dhidi ya mimba za utotoni, ndoa za lazima na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI,” alisema Mama Pinda.

Mapema, akimkaribisha Mama Pinda kuzungumza na wakazi wa Shirati, Askofu John Nyagwegwe wa Kanisa la Mennonite Dayosisi ya Mara Kaskazini alisema katika dunia ya sasa kuna mabinti wengi ambao wanakua lakini hawajui waende wapi ama wafanye nini na akasisitiza kuwa wote hawa wanahitaji malezi ili wakue katika maadili mema.

Alisema katika kipindi cha miaka minne, Kanisa hilo limewafikia watoto 1,613 wanaoishi kwenye mazingira magumu ambapo kati yao 580 ni wasichana na 1,033 ni wavulana.

“Katika wilaya nzima ya Rorya, kupitia watendaji wa vijiji na kata, tulipata watoto 4,840 ambao wanaishi kwenye mazingira magumu na wanahitaji msaada wa elimu, mavazi na huduma za afya. Tulioweza kuwahudumia ni 1,613 tu kwa hiyo kuna wengine 3,233 bado wanahitaji msaada wa jamii,” alisema.

Alisema anatamani kuona viongozi wanaguswa na shida za Watanzania ili wasaidie kutatua shida hizo. “Natamani sana kama viongozi wetu wangeona maisha yao siyo bora kuliko maisha ya Watanzania, basi maisha ya Watanzania yangekuwa bora kuliko ilivyo sasa.”

Askofu Nyagwegwe alitumia fursa hiyo kukemea tabia ya baadhi ya viongozi ambao wanataka kuvuruga amani kwa kudhani kuwa wao watabakia salama wakati nchi ikiingia kwenye machafuko.

“Kuna baadhi ya viongozi wanachezea kitu cha thamani ambacho tumedumu nacho kwa zaidi ya miaka 50. Kuna wachahche wanataka kuangamiza nchi wakidhani wao watapona. Amani ikipotea hakuna kiongozi wa Serikali wala Maaskofu wala Wachungaji watakaopona,” alisisitiza.

Akisoma risala yao, Katibu wa Idara ya Akinamama ya kanisa hilo, Bi. Leah Makoyo alisema kukamilika kwa ukarabati huo kutawasaidia wasichana kutoka shule sita za sekondari za Katuru, Tai, Masonga, Prof. Sarungi, Bukama na Mukoma ambazo ziko umbali wa kati ya kilometa tano hadi 28 kutoka Shirati mjini.

Alisema licha ya umbali mrefu wa kwenda shule, watoto wa kike katika wilaya hiyo wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za makazi yasiyo salama, mimba za utotoni, ukeketaji, maambukizi ya VVU, dawa za kulevya na tatizo la maji ambalo huchukua sehemu kubwa ya muda wao wa masomo.