Mama Samia Suluhu; Mgombea Mwenza Aliyepanga Kuwapigania Wanawake

Mgombea mwenza wa nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan akihutubia wananchi katika moja ya mikutano yake ya kampeni inayoendelea nchini akiinadi ilani ya CCM.

Mgombea mwenza wa nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan akihutubia wananchi katika moja ya mikutano yake ya kampeni inayoendelea nchini akiinadi ilani ya CCM.


Na Joachim Mushi, dev.kisakuzi.com

MCHUANO wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Tanzania unaotarajia kufanyika Oktoba 25, 2015 unaendelea maeneo mbalimbali ya nchini, huku vyama anuai vilivyofanikiwa kuingia katika ushindani huo wa kisiasa vikinadi ilani na sera zao kwa Watanzania ili kuwashawishi wachaguliwe.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa mara ya kwanza kimemsimamisha mwanamke katika ngazi ya juu ya uongozi. Kimemteuwa mwanamama, Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza wa mgombea wa nafasi ya urais kupitia chama hicho, John Pombe Magufuli. Kwa mantiki hiyo endapo kitafanikiwa kushinda urais Tanzania kwa mara ya kwanza mwanamke atashika nafasi ya juu ya madaraka ndani ya Serikali.

Bi. Suluhu ambaye amewahi kufanya kazi kama kiongozi katika Serikali zote mbili yaani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar (Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar-SMZ) anauzoevu wa kutosha na elimu nzuri inayomuongeze sifa ya kuimudu nafasi aliyopewa kwa sasa.

Ki historia, Bi. Suluhu alizaliwa Januari 27, mwaka 1960 nchini na kupata elimu yake ya msingi na sekondari Zanzibar, kabla ya kuendelea na elimu ya juu kwa kozi mbalimbali katika vyuo vikuu vya Mzumbe nchini Tanzania, Chuo Kikuu cha Manchester nchini Uingereza kwa ushirikiano na Chuo Kikuu Huri cha Tanzania (OUT).

Mgombea mwenza wa nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan (kulia) akimjulia hali mmoja wa akinamama katika moja ya wodi za wazazi nchini. Kiongozi huyo anaahidi endapo atashinda uchaguzi kupitia chama chake ataziangalia zaidi huduma za afya ya uzazi ili kuboresha zaidi.

Mgombea mwenza wa nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan (kulia) akimjulia hali mmoja wa akinamama katika moja ya wodi za wazazi nchini. Kiongozi huyo anaahidi endapo atashinda uchaguzi kupitia chama chake ataziangalia zaidi huduma za afya ya uzazi ili kuboresha zaidi.


Mwanamama huyu pia amefanikiwa kuchukua kozi ndogo ndogo anuai katika vyuo vya ndani na nje ya Tanzania, vikiwemo vya; ‘Institute of Management for Leaders, Hyderabad, India’, Zanzibar Institute of Financial Administration, ZIFA, pamoja na National Institute of Public Administration, Lahore Pakistan.

Mgombea huyo mwanamama amekuwa waziri na mbunge kwa zaidi ya miaka mitano mfululizo na pia kufanikiwa kushika nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, nafasi ambazo kwa kiasi kikubwa zinamuongezea sifa ya kuweza kuimudu nafasi aliyopewa kwa sasa anasema hii ni nafasi pekee kwa akinamama wote bila kujali itikadi zao kumuunga mkono ili aweze kushinda na kuweka historia nchini ya mwanamke kushika nafasi ya juu kuliko zote nchini. Kwa sasa kiongozi huyu anazunguka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani kuinadi ilani ya CCM.

Bi. Suluhu anasema ilani ya CCM imepanga kufanya mengi mazuri kwa Watanzania, lakini pamoja na hayo amejitolea kuhakikisha anawapigania akinamama endapo atafanikiwa kushinda nafasi hiyo ili kuweza kukabiliana na changamoto anuai ambazo zimekuwa kero na kikwazo kwao.

Anazitaja changamoto hizo ni pamoja na huduma za afya ya uzazi ambapo akinamama wengi na watoto wachanga wamekuwa wakipoteza maisha katika eneo hilo. Anasema licha ya ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM kufafanua zaidi itakavyo boresha huduma za afya kiujumla, lakini atalisimamia na kuongeza nguvu za ziada kuhakikisha akinamama wanapata huduma za kuridhisha maeneo wanapopata huduma za afya ya uzazi.

Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika Jimbo la Mbulu Mjini anasema endapo CCM itashinda uchaguzi huu imepanga kuajiri watumishi 15,000 wa sekta ya afya wakiwemo madaktari 2020 ndani ya kipindi kifupi ili kuhakikisha inaboresha zaidi huduma za afya maeneo mbalimbali nchini hasa huduma za akinamama na watoto. Bi. Suluhu anasema hatua hiyo ni mpango maalumu wa kuboresha huduma za afya kiujumla na hasa huduma za akinamama wajawazito na watoto ambapo wamekuwa na changamoto katika huduma hizo.

Mgombea mwenza wa nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan akiinadi ilani mpya ya Uchaguzi Mkuu ya CCM kwa wananchi (hawapo pichani) katika moja ya mikutano yake.

Mgombea mwenza wa nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan akiinadi ilani mpya ya Uchaguzi Mkuu ya CCM kwa wananchi (hawapo pichani) katika moja ya mikutano yake.


Aidha anaongeza kuwa mpango mwingine ni kuwawezesha akinamama na vijana kiuchumi kupitia vikundi vyao. Anabainisha kuwa eneo hili Serikali ya CCM kupitia ilani yake imetenga shilimi milioni 50 kwa kila kijiji fedha ambazo zitakuwa zikikopeshwa makundi hayo kwa masharti nafuu ili waweze kujikwamua kiuchumi. Anasema eneo hilo pia halmashauri zitasimamiwa kutoa asilimia tano ya mapato kuwaunga mkono akinamama na vijana ili kuchochea maendeleo yao. Ili kukuza biashara zao Bi. Suluhu anasema Serikali itasimamia kuhakikisha asilimia 30 ya tenda ndogondogo za halmashauri mbalimbali zipewe vikundi vya akinamama na vijana.

Anaeleza kuwa ili kuongeza thamani kwa mazao yatakaokuwa yakizalishwa na vikundi hivyo kupitia miradi ya kilimo imepanga kujenga viwanda vingi maeneo mbalimbali ya nchi ambavyo vitayaongezea thamani mazao na pia kuzalisha ajira kwa asilimia 40, jambo ambalo pia litakuza uchumia wa akinamama na vijana.

Mwanamama huyo shupavu anabainisha kuwa kutokana na suala la kero ya maji pia kuwaumiza zaidi akinamama ilani ya chama chake imedhamiria kumalizia miradi ya maji na kuanzisha mingine anuai ili kukabiliana na changamoto ya kero ya maji safi na salama iliyopo maeneo mbalimbali ya nchini vijijini ama mjini.

Bi. Suluhu anasema Serikali watakayoiunda itaendelea kushughulikia kero ya maji katika vijiji vyenye ukame na kuhakikisha kila kijiji kinapata maji safi na salama kwa matumizi. Lakini ili kumaliza kabisa kero hiyo anasema Serikali itaunda mfuko wa maji ambao utashughulikia kero za huduma za maji safi na salama.

Anasema migogoro yoyote inayosababisha mapigano idadi kuwa inayoathirika ni wanawake na watoto, hivyo Serikali itakayoundwa na CCM itahakikisha inapima ardhi yote ya vijiji pamoja na Wilaya na kuainisha mipaka ili kukomesha migogoro ya ardhi inayochangia mapigano ya wakulima na wafugaji baadhi ya maeneo ya Tanzania mara kwa mara.

Mgombea mwenza wa nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan (mwenye miwani) akisalimiana na baadhi ya akinamama na wananchi katika moja ya mikutano yake ya kampeni.

Mgombea mwenza wa nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan (mwenye miwani) akisalimiana na baadhi ya akinamama na wananchi katika moja ya mikutano yake ya kampeni.

Mgombea mwenza wa nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan (hayupo pichani) akihutubia wananchi katika moja ya mikutano yake ya kampeni inayoendelea nchini akiinadi ilani ya CCM.

Mgombea mwenza wa nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan (hayupo pichani) akihutubia wananchi katika moja ya mikutano yake ya kampeni inayoendelea nchini akiinadi ilani ya CCM.


Anasema mara baada ya kupima ardhi na kuweka mipaka kati ya maeneo ya wakulima na wafugaji watahakikisha mipaka hiyo inatambulika na kuheshimiwa na jamii zote mbili ili kuzuia migogoro na mapigano ambayo yamekuwa na uhasama mkubwa na kupoteza uhai na mali za raia wasio kuwa na hatia katika maeneo yenye mgogoro.

Hata hivyo katika kampeni zake mara zote amemalizia kwa kuwaomba wananchi kutunza amani iliyoasisiwa na viongozi wetu wa taifa kwa kutokubali kuyumbishwa na kushawishia kuvuruga amani ya nchi. “…Tusikubali kuchokozwa na kuchokoseka na kuvuruga amani…bila amani hakuna maendeleo,” alisema Bi. Suluhu.

Anawataka viongozi wa siasa kuacha kutoa vitisho kwa wapiga kura kwani hali hiyo ni kuibaka demokrasia hivyo CCM na vijana wake hawatakuwa tayari kuona demokrasia inabakwa nchini na wapuuzi wachahe. “…Vijana wa CCM naomba mkikamata kibaka wa demokrasia shughulikeni naye kidogo kabla ya kumpeleka polisi…CCM itashinda kwa kishindo,” alisema Nape Nnauye.

Miongoni mwa vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo kulingana na taarifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ni pamoja na CCM, CUF, CHADEMA, UMD, NCCR- Mageuzi, NLD, UPDP, NRA, TADEA, TLP, UDP, DEMOKRASIA MAKINI, CHAUSTA, DP, APPT-Maendeleo, Jahazi Asilia, SAU, AFP, CCK, ADC, CHAUMMA na ACT-Wazalendo.