Mama Salma: Walimu anzisheni vikundi vya kujisomea

Na Anna Nkinda – Maelezo

WALIMU nchini wametakiwa kuanzisha vikundi vya kujisomea kwa wanafunzi ili watoto hao wawe na tabia ya kupenda kusoma ambayo itawasaidia kutotumia muda wao vibaya na kujiingiza katika tabia hatarishi zilizopo ndani ya jamii.

Wito huo umetolewa leo na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akifungua mradi wa asante maktaba ndogo ya kujisomea iliyopo katika shule ya msingi Milenia Ya Tatu Kimara jijini Dar es Salaam.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) aliwataka wakazi wa eneo hilo kutumia huduma ya maktaba hiyo kikamilifu ili waweze kupata taarifa mbalimbali za maendeleo kwani maktaba licha ya kuwasaidia wanafunzi huwa ni chanzo muhimu cha taarifa na ufahamu wa kina kuhusu mambo mbalimbali.

“Maktaba nyingi zilizopo mjini na vijijini zina manufaa makubwa sana kwa wanawake kwani zinawasaidia kupata taarifa mbalimbali na kuwapunguzia adha ya kutukufahamu mambo yanayoendelea ulimwenguni.

Hakuna asiyejua kuwa mwanamke akielimishwa anakuwa katika nafasi nzuri ya kuielimisha jamii yake nawasihi wanawake wenzangu muitumie maktaba hii kudumisha tabia ya kujisomea kwani unapojisomea unapata taarifa na ujuzi mbalimbali hivyo kuwa na uwezo zaidi wa kupambana na changamoto zinazotuzunguka kwani ujuzi ni ngao”, alisema Mama Kikwete.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Theresia Mbepela alisema kuwa maktaba hiyo ni nzuri na kuahidi kuwasaidia wanafunzi kwa hali na mali ili waweze kuitumia na kuitunza pia aliwataka wazazi wa watoto hao kuwahimiza kusoma kwani elimu ni nguzo na ukombozi kwa kila mwanadamu.

Ukarabati wa Maktaba hiyo ulifanywa na Halmashauri ya manispaa ya Kinondoni huku gharama za ukarabati huo ikiwa ni shilingi milioni tano za kitanzania kwa upande wake Serikali ya Korea imegharamia kompyuta, vitabu, thamani na projector. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu mradi huo wa asante maktaba ndogo unaofadhiliwa na Serikali ya Korea utakuwa umezifikia maktaba 19 za shule za msingi hapa nchini.