Mke wa Rais Mama Salma Kikwete, amewaonya wananchi kuepuka majungu, fitna na migongano kwani ni sumu ambayo kamwe haiwezi kuleta maendeleo.
Mama Salma aliyasema hayo juzi jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa umoja wa vikundi vilivyopo chini ya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Wama).
“Vikundi vilianzishwa ili kuleta maendeleo nchini lakini vikundi vingi huvunjika kutokana na mfumo mbaya wa uongozi, fitna, majungu na migongano sasa tukiiendekeza hiyo hatuwezi kujiletea maendeleo hata kidogo,” alisisitiza.
Aidha, alieleza kuwa Wama inatambua kuwa kuna vikundi vingi ambavyo vimetawanyika hivyo imeona ni vyema kuvikusanya na kuviweka pamoja chini ya kata ili kuviunganisha na wadau wa maendeleo.
Awali katika risala ya shukurani ya kikundi hicho iliyosomwa na Juliana Remmy, alimshukuru Mama Salma kwa kuwakumbuka wanawake ambao hawakupata nafasi kama hiyo na asasi ya Care International ambayo imewaunganisha na wadau mbalimbali wa maendeleo kama vile Benki ya Maendeleo na Shirika la Viwanda Vidogo (Sido) ambalo limewapa elimu ya usindikaji.
Vikundi hivyo ambavyo sasa vimefikia 40 vikiwa na wanachama zaidi ya 700, vimefikisha Sh. milioni 15 kwa mwaka 2010.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa, aliahidi kukichangia kikundi hicho Shilingi milioni mbili na akasema kwamba kuna sheria ianyozitaka manispaa zote kupeleka asilimia 10 ya pato lake kwa vikundi kama hivyo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiq, alisema kwa kutambua mchango wa Mama Salma katika kuleta maendeleo, atahakikisha kikundi hicho kinapata kiwanja cha kujenga ofisi.