Mama Salma Kikwete Awataka Watanzania Kuthamini Bidhaa Zao

Baadhi ya akina mama wajasiriamali wakionesha bidhaa zao ambazo zimetengenezwa ndani ya nchi

Na Anna Nkinda – Maelezo

WATANZANIA wametakiwa kujenga utaratibu wa kupenda kuthamini bidhaa za ndani na kuziona ni bora zaidi, kwani hatua hiyo itawafanya na wageni kutoka nje kuzipenda bidhaa hizo ambazo zinazalishwa ndani ya nchi. Alisema tendo la kuzipenda litasababisha kuongezeka kwa thamani ya bidhaa hizo.

Mwito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza kutembelea maonesho ya 37 ya Biashara ya Kimataifa yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa wilayani Temeke Dar es Salaam.

Mama Kikwete katika ziara hiyo aliambatana na Mke wa Mfalme Mswati wa Swaziland Inkhosikati Lambikiza, Mke wa Makamu wa Rais wa Zambia Mama Charlotte Scott na Mwakilishi wa Mke wa Rais Joseph Kabila wa Jamuhuri ya watu wa Congo ambaye ni Waziri wa Jinsia, Watoto na Familia Inagosi Bulo.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa walitembelea maonyesho hayo ili kuona shughuli mbalimbali zinazofanywa ndani na nje ya nchi kuanzia ngazi ya juu hadi chini.

“Tumeona bidhaa za aina mbalimbali zinazozalishwa ndani na nje ya nchi na jinsi watu wanavyoweza kubadilishana uzoefu wa biashara hakika kadri siku zinavyozidi  kwenda kuna maboresho makubwa juu ya utengenezaji wa bidhaa zinazozalishwa nchini”, alisema Mama Kikwete.

Aliwashukuru wageni alioambatana nao kwa kuzipenda bidhaa zilizopo kwenye mabada ya watanzania na kuwaomba wananchi kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya mkoa wa Dar es Salaam kutembelea maonyesho hayo kwani kuona ni kujifunza.

Pia aliwapongeza na kuwashukuru wanawake kwa kazi kubwa wanazozifanya za kuzalisha bidhaa na kufanya biashara mbalimbali ambazo zimewasaidia kujiletea maendeleo yao na jamii inayowazunguka.