Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
WAKAZI mkoani Lindi wametakiwa kusimamia elimu ya watoto wao kwa kufuatilia mahudhuria yao shuleni jambo ambalo litawasaidia katika maisha yao ya baadaye kwa kuweza kujiajiri au kuajiriwa pindi watakapomaliza masomo na hivyo kujikwamua na hali ngumu ya maisha.
Wito huo umetolewa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa (NEC) wakati akiongea kwa nyakati tofauti na viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi ya Chama hicho katika matawi ya Jangwani, Tandangongoro na Mkupama yaliyopo katika wilaya ya Lindi mjini.
Akiwa katika tawi la Jangwani lililopo katika kata ya Chikonji Mama Kikwete aliongea na watoto ambao aliwaita ili awasalimie na baada ya kuwauliza maswali kuhusu elimu walisema baadhi yao waliacha shule kwa ajili ya utoro. Jambo alilolifanya ni kuwasisitiza watoto hao kusoma kwa bidii na kuepukana na tabia ya utoro kwani elimu ni ukombozi wa maisha yao.
Baada ya kuongea na watoto hao ambao wengi wao walikuwa ni wanafunzi wa shule ya Msingi Mjumbe huyo wa NEC taifa aliongea na viongozi wa CCM na kuwataka wao kama wazazi kutatua tatizo la utoro kwa watoto wa kijiji hicho kwa kusimamia na kuhakikisha wanakwenda shule kwa wakati.
“Hali ya elimu katika mkoa wa Lindi ni ngumu vijana hawasomi wengi wao wanakatiza masomo kwa ajili ya utoro na kuolewa sisi kama viongozi ni lazima tupige kelele ili kuhakikisha watoto wanakwenda shule na kuhudhuria masomo darasani,” alisema Mama Kikwete.
Aidha Mama Kikwete pia aliwaasa viongozi hao wa Halmashauri kuu ya tawi kutunza amani iliyopo na kuitumia katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwa ni pamoja na kulima mazao hasa yanayohimili ukame ikiwa ni pamoja na mtama ili kuepukana na tatizo la njaa linaloikabii wilaya hiyo mara kwa mara.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Lindi Mzee Ali Mtopa alisema katika mikoa ya Kusini ambayo ni Lindi na Mtwara hivi sasa kuna maeneo matatu yanayotoa gesi ambayo inaleta utajiri lakini uchimbaji wake unahitaji vijana waliosoma.
“Uchimbaji wa gesi unahitaji kupata wataalam ambao wamesoma kama watoto wetu hawatakuwa na elimu watakuja watu kutoka mbali na kufanya kazi ya uchimbaji wakwetu wataishia kufanya kazi ya vibarua tu. Nawaomba muwaache watoto wasome msiwaoze au kuwaacha wanakatiza masomo kwa ajili ya utoro”, alisema Mzee Mtope.
Mama Kikwete ambaye ni mjumbe wa NEC Taifa kupitia wilaya ya Lindi mjini alikutana na viongozi hao wa Halmashauri kuu ya tawi ya CCM kwa ajili ya kuimarisha kazi za chama hicho ikiwa ni pamoja na kufanya vikao na viongozi.