Na Anna Nkinda, Cape Town
JAMII imetakiwa kushirikiana kwa pamoja na kuchukua hatua za karibu kwa kuwalea watoto wa kike kama watoto wao wa kuwazaa huku wakiwapa nafasi kama watoto wa kiume, kuwapatia elimu, kuwaheshimu na kuwalinda jambo ambalo litawafanya wafanikiwe katika maisha yao.
Wito huo umetolewa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akizungumza kwenye mkutano wa kamati maalum ya viongozi wanaoshughulikia huduma na elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kutoka nchi za Jumuia ya Afrika ya Mashariki (EAC) na Jumuia ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kikanda kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika katika Hoteli ya The Westin iliyopo mjini Cape Town nchini Afrika ya Kusini.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema tafiti zinaonyesha Duniani kote zaidi ya wasichana milioni 58 wameolewa wakiwa na umri wa chini ya miaka 18 kati ya hao milioni 15 wanaumri wa kati ya miaka 10 hadi 14 huku wengi wao wakiwa wameolewa kinyume na matakwa yao na kushuhudia unyanyasaji wa kijinsia, uelewa mdogo wa haki zao na kutopata elimu ya afya ya uzazi.
“Idadi ya watoto wa kike wanaomaliza elimu ya msingi imeongezeka na kuwazidi watoto wa kiume ingawa idadi ya wasichana wanaomaliza elimu ya Sekondari ni ndogo ukilinganisha na watoto wa kiume katika nchi nyingi za Afrika”, alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wa maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi Mama Kikwete alisema asilimia 42 ya watu wanaopata maambukizi ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 24, katika nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara vijana ni asilimia 80.
Mama Kikwete alisema, “Nchini Tanzania tafiti zilizofanyika zimeonyesha kuwa watoto wa kike wengi wanajihusisha na mahusiano ya kimapenzi mapema kwa asilimi 13 ambao wanafanya mapenzi kabla ya umri wa miaka 15 na kwa upande wa watoto wa kiume ni asilimia saba matokeo yake ni upatikanaji wa mimba za utotoni.
Msichana mmoja kati ya wasichana wanne wenye umri wa miaka 15 hadi 19 ni mjamzito au ameshazaa. Idadi hii ni kubwa katika nchi nyingi za Afrika inasikitisha kwani kubeba mimba katika umri mdogo kunaweza kusababisha kifo cha mama mjamzito pamoja na mtoto wakati wa kujifungua”.
Akifungua mkutano huo wa siku mbili Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupamba na Ukimwi (UNAIDS) Prof. Sheila Tlou alisema wajumbe wa kamati hiyo wanatakiwa kuhakikisha maazimio waliyokubaliana yanapitishwa na kufanyiwa kazi katika nchi husika ili vijana waweze kupata elimu ya afya ya uzazi.
Prof. Tlou alisema, “Tutahakikisha kuwa rasilimali za kutosha zinapatikana ikiwa ni pamoja na kutafuta fedha kutoka kwa wafadhili mbalimbali hii ni kuhakikisha kuwa maadhimio haya yanafanikiwa kwani vijana ni viongozi wa leo wanaohitaji kupata huduma ikiwa ni pamoja na elimu ili waweze kujiepusha na mazingira ambayo yatawapelekea kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi”.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa EAC Jesca Eriyo alisema mwaka mmoja uliopita wakuu wa nchi za Afrika ya Mashariki walikubaliana kuhakikisha wanaimarisha utolewaji wa elimu ya afya ya uzazi katika nchi zao na hivyo kuwa rahisi kwa nchi hizo kufanyika kazi maazimio hayo.
“Vijana wanamaswali mengi kuhusu afya ya uzazi na inafika wakati hawajui wa kumuuliza hivyo basi elimu ya uzazi ifundishwe kwao kwani kutokana na mila za kiafrika ni vigumu kwa mzazi kuongea na mtoto wake kuhusu afya ya uzazi”, alisema Eriyo.
Alimalizia kwa kusema kuwa vijana wanatakiwa kujua hali ya afya zao ikiwa ni pamoja na kupima kama wamepata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na kujiepusha na wababa na wamama (mafataki) ambao wanaweza kuwarubuni na kuwaharibia maisha yao jambo ambalo litasababisha kupatikana kwa kizazi kizuri hapo baadaye.
Kamati hiyo imekutana kwa mara ya pili kwa ajili ya kupitia rasimu ya maazimio ya kuhakikisha kuwa vijana wote katika nchi zilizopo ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kusini wanapata elimu kuhusiana na afya ya uzazi na ujinsia jambo ambalo litawasaidia kufahamu zaidi ugonjwa Ukimwi kwamara ya kwanza ilikutana mwezi wa nane nchini Botswana.
Makubaliano hayo yanatarajiwa kusainiwa na mawaziri wa Afya na Elimu kutoka nchi 21 za Afrika Mashariki na Kusini ambayo inatakuwa ni sehemu ya utekelezaji kwa nchi kabla ya kufanyika kwa mkutano wa kimataifa wa vita dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi na magonjwa ya zinaa unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni mjini humo.