Na Anna Nkinda – Brussels, Ubelgiji
MKE wa Rais Mama Salma Kikwete amepewa cheti na Umoja wa wake wa Mabalozi wa Afrika waishio katika nchi za Jumuia ya Ulaya kwa kutambua na kuthamini mchango wake na kazi anazozifanya za kuwasaidia wanawake, wasichana na watoto wa Tanzania.
Cheti hicho amekabidhiwa jana katika hafla fupi ya chakula cha mchana kilichoandaliwa na wake hao wa mabalozi katika ukumbi wa mikutano uliopo Hoteli ya Sheraton mjini Brussels. Mama Kikwete ni mmoja kati ya wake wa Marais wa tano wa Afrika waliokabidhiwa vyeti hivyo vya heshima kutokana na kazi zao wanazozifanya za kuisaidia jamii na kuhakikisha kuwa inapata mahitaji ya muhimu kama huduma ya afya na elimu.
Akiongea kabla ya kuwakabidhi wake hao wa marais vyeti hivyo Mke wa Balozi wa Equatorial Guinea ambaye pia ni rais wa umoja huo Mama Mangue de Nvono Nca alisema nia ya kuanzishwa kwa umoja wao ni kulitambulisha bara la Afrika ambalo linajulikana kuwa na changamoto za njaa, magonjwa, kutokuwa na haki na usalama wa kutosha katika nchi za Ulaya.
“Siyo kama Bara letu la Afrika linakabiliwa na changamoto peke yake bali pia limejaliwa kuwa na umoja, mshikamano na ukarimu na haya yote yamejidhihirisha kwetu leo hii kutokana na kitendo cha wake wa marais wetu kushiriki pamoja nasi katika hafla hii na kubadilishana mawazo,” alisema Mangue de Nvono Nca.
Alisema umoja huo unatambua kazi kubwa inayofanywa na wake wa Marais wa Afrika kwa jinsi wanavyowaunga mkono wenza wao kwa kufanya kazi ambazo malengo yake makubwa ni kuwasaidia wanawake, wasichana, watoto na watu ambao wako katika makundi hatarishi ndani ya jamii.
Akiongea kwa niaba ya wenzake mara baada ya kutunukiwa vyeti hivyo Mke wa Rais wa Congo Brazzavile Mama Antoinette N’Guesso aliwashukuru wake hao wa mabalozi kwa kazi wanayoifanya ya kulitangaza bara la Afrika kuwa ni nchi ya umoja, mshikamano na ukarimu jambo ambalo litaondoa dhana iliyopo miongoni mwa watu kuwa kitu pekee kilichopo barani Afrika ni matatizo.
Wengine waliokabidhiwa vyeti hivyo ni pamoja na Malkia wa Swaziland Inkhosikati Zena Seraya Mahlangu, Mke wa Rais wa Madagascar Mama Lalao Rajaonarimampianina, Congo Brazzaville Mama Antoinette N’Guesso na Cameroon Mama Chantal Biy.
Wake hao wa Marais wameambatana na wenza wao ambao ni Marais wa Afrika wanaohudhuria mkutano wa nne wa wakuu wa nchi za Afrika na Jumuia ya Ulaya unaofanyika nchini humo.