Mama Salma Awataka Wasichana Kutoogopa Sayansi

Mama Salma Kikwete

Mama Salma Kikwete

Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi

WANAFUNZI wa kike nchini wameaswa kutoogopa masomo ya sayansi kwani masomo hayo siyo magumu ukilinganisha na mengine, bali wanachotakiwa kufanya ni kuzishika na kuzijua kanuni za somo husika.

Rai hiyo imetolewa jana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Angaza iliyopo wilayani humo.

Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete alisema mwanafunzi anayesoma masomo ya sayansi akizishika kanuni anafanya vizuri katika masomo yake tofauti na mwanafunzi wa masomo ya sanaa na kutoa mfano kama mwanafunzi anataka kujua hesabu ni lazima kila siku kabla hajalala afanye mazoezi kwa maswali yasiyopungua 10.

Kwa upande wa uongozi aliwataka wasichana kutoogopa kuomba nafasi mbalimbali za uongozi kwani wakianza uongozi katika umri mdogo watakuwa viongozi wzuri hapo baadaye. MNEC huyo aliendelea kuwaasa wanafunzi hao na kuwaambia kuwa wao ni ndugu na wakiona mwenzao mvulana au msichana amesimama na mtu wa jinsia tofauti katika mazingira tatanishi wamkanye aache tabia hiyo kwani kilichowapeleka shule ni kusoma na siyo kufanya mapenzi.

“Elimu ni nguzo ya maisha ni lazima mjitambue nyie ni kina nani, mnafanya nini na mnataka kuwa nani hapo baadaye. Someni kwa bidii, waheshimuni na kuwasikiliza walimu wenu kwa kufanya hivyo mtafaulu na kufika chuo kikuu.

“Mkiwa wasomi wazuri mtawezaa kuzitumia fursa zilizopo katika mkoa wetu ikiwa ni pamoja na kuajiriwa katika sekta mbalimbali ikiwemo ya gesi,” alisisitiza Mama Kikwete.

Naye Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Lindi Mzee Alli Mtopa alisema Dunia ya leo ni ya wasomi hivyo basi ni lazima wanafunzi hao wasome ili wafanye kazi katika sekta ya gesi inayopatikana mkoani humo kwani wasiposoma kazi za kitaalamu zitafanywa na watu wengine na wao watabaki kufanya kazi za vibarua na mwisho wake wataandamana kuzuia gesi isitoke.

Akisoma taarifa ya shule hiyo mchanganyiko Mkuu wa shule mwalimu Upendo Muro alisema shule hiyo ambayo ni ya kata ilianza mwaka 2008 ina wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne 359 na walimu 25. Mwalimu Muro alisema kwa upande wa wanafunzi wa kidato cha kwanza waliochaguliwa kujiunga katika shule shule hiyo kwa mwaka huu ni 102 walioripoti ni 87 kati yao wanawake ni 45 na wanaume ni 42.

“Changamoto zinazoikabili shule yetu ni upungufu wa majengo, nyumba za walimu, vifaa vya maabara na walimu wa masomo ya sayansi ambayo ni kemia, fizikia na hesabu, ukosefu wa umeme, maji, kutokuwa na jengo la maabara, na ukosefu wa vyoo vya walimu”, alisema Mwalimu Muro.

Aliyataja mafanikio waliyoyapata kuwa ni pamoja na kuwarudisha shuleni wanafunzi watoro, matokeo ya kidato cha pili na cha nne yanazidi kuwa mazuri kadri miaka inavyokwenda, wanafunzi wanakunywa uji na mchakato unaendelea ili wale chakula cha mchana.

Wanafunzi wa kidato cha nne waliohitimu mwaka jana wote walifanya mitihani ya masomo ya sayansi kwa vitendo na matokeo ya kidato cha nne ya mwaka jana shule imeweza kutoa wanafunzi waliojiunga na kidato cha tano katika masomo ya PCB wawili, PCM mmoja na HGL wawili.

Akiwa shuleni hapo alikagua ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara za fizikia, kemia na bailojia na kuahidi kuchangia mabati 100 pia aliahidi kuwaletea wanafunzi vifaa vya bendi ya shule.

Aidha Mama Kikwete alifanya vikao na viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi ya Chama hicho katika matawi ya Angola, Majani Mapana na Angaza yaliyopo kata ya Wailesi na kuwahimiza wazazi wawasisitize watoto waone umuhimu wa kuwa na elimu.

“Kina mama zungumzeni na watoto wenu wa kike ili wasijihusishe na mapenzi wawapo shuleni kwani mimba ni sumu, mtoto akipata ujauzito atakatisha masomo yake na kutotimiza ndoto zake. Nanyi kinababa msipokee mahari za watoto wenu ambao ni wanafunzi subirini hadi watakapomaliza masomo yao,” alisisitiza.

Kuhusu ufanyaji wa kazi za nyumbani aliwaambia viongozi hao ni muhimu watoto wote wa kike na wa kiume wakafundishwa kazi hizo na siyo kazi hizo zikafanywa na mtoto wa kike peke yake jambo litakalomfanya kukosa muda wa kujisomea pindi arudipo shuleni.

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Wailesi Mama Kikwete aliwaambia wananchi kwamba Serikali ya CCM imeboresha elimu kwa kujenga shule za Sekondari za Kata ambazo hivi sasa hata watoto kutoka familia maskini wanapata elimu ya Sekondari tofati na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Mama Kikwete alisema, “Hivi sasa hakuna mtoto anayefaulu na kukosa shule, zamani katika mkoa huu kulikuwa na Sekondari mbili tu ya Lindi Sekondari kwa wanafunzi waliofaulu darasa la saba na Mkonge kwa wanafunzi waliofeli, na kujiunga na shule hii ilikuwa ni lazima mzazi awe na fedha ya kulipa.

“Mtoto akifeli usihangaike kumtafutia shule ya kulipia bali mpeleke elimu ya ufundi kwani siyo wote watakaosoma elimu ya sekondari wengine watasoma masomo ya ufundi ambayo yatawasaidia kuweza kuajiriwa au kujiajiri wenyewe”.

Mama Kikwete yupo wilayani humo kwa ajili ya kuimarisha kazi za chama hicho ikiwa ni pamoja na kufanya vikao na viongozi na kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010.