Mama Salma Asaidia Madawati 100 Shule ya Msingi Mnacho

Mama Salma Kikwete.

Mama Salma Kikwete.

Na Anna Nkinda – Maelezo, Ruangwa

MKE wa Rais Mama Salma Kikwete ametoa msaada wa madawati 100 kwa shule ya msingi Mnacho iliyopo kijiji cha Ng’au wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi ambayo alifanya mazoezi ya kufundisha kwa vitendo (BTP) wakati akiwa mwanachuo wa Chuo cha Ualimu Nachingwea.

Mwishoni mwa mwaka jana Mama Kikwete ambaye kitaaluma ni mwalimu na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alitembelea shuleni hapo na kukuta kuna upungufu mkubwa wa madawati na kuamua kutoa msaada huo ili uweze kukabiliana na tatizo hilo.

Akizungumza na wananchi waliohudhuria hafla ya makabidhiano ya madawati hayo Mama Kikwete aliwasihi wazazi kuhakikisha watoto wao wanakwenda shule, wanasoma na kufaulu katika mitihani yao kwani elimu ni mkombozi wa maisha. Alisema elimu ni haki ya mtoto hivyo basi wazazi wafuatilie na kuhakikisha watoto wao wanasoma hadi ngazi ya elimu ya juu.

“Naamini kupatikana kwa madawati haya kutaondoa tatizo la watoto kubanana katika madawati yaliyokuwepo. Nawasihi waleteni watoto shule wasome kwani hivi sasa kuna madawati ya kutosha,” alisema Mama Kikwete.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ruangwa ambaye ni Naibu waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Kassim Majaliwa alimshukuru mama Kikwete kwa msaada wa madawati aina ya plastiki ngumu aliyoyatoa kwa shule hiyo.

Waziri Majaliwa alisema kutokana na changamoto ya upungufu wa madawati uliokuwepo  katika shule hiyo Mama Kikwete alimpatia shilingi milioni tano kwa ajili ya kununua madawati 100 ili yaweze kutatua tatizo hilo.

Akisoma taarifa ya shule ya Msingi Mnacho Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa Stephano Ngondo alisema shule hiyo ilianzishwa mwaka 1932 na wamisionari ikiwa inatoa elimu ya msingi na baadaye kurudishwa chini ya usimamizi wa Serikali mwaka 1963 na kuendelea kutoa elimu hiyo mpaka sasa. Shule hiyo inawanafunzi 371 kati ya hao 177 ni wavulana na 194 wasichana na walimu 10 kati yao wanawake sita na wanaume wanne, vyumba vya madarasa 10 na nyumba za walimu mbili.

Ngondo alisema, “Idadi ya uandikishaji wa wanafunzi shuleni hapo imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka na ufaulu umeongezeka. Kwa mwaka 2014 jumla ya wanafunzi 27 walifanya mtihani wa kumalia elimu ya msingi kati ya hao 22 sawa na asilimia 81.84 walifaulu na kujiunga na kidato cha kwanza.

Alizitaja changamoto zinazoikabili shule hiyo ni uhaba wa nyumba za walimu, uchakavu wa vyumba vya madarasa, uhaba wa vyoo vya kudumu hasa vilivyokuwepo kutitia, umiliki wa eneo la shule kwani eneo ambalo shule ipo linamilikiwa na kanisa Katoliki Parokia ya Mnacho na uhaba wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Wakati huo huo Mama Kikwete akiwa wilayani Ruangwa alifanya mkutano na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuongea nao mambo mbalimbali yahusuyo chama hicho.

Mama Kikwete ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) wilaya ya Lindi mjini aliwahimiza wajumbe waliohudhuria mkutano huo kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftati la kudumu la wapiga kura na kuipigia kura ya ndiyo katiba inayopendekezwa.

“Wakati ukifika mkajiandikishe katika daftari la kudumu la wapiga kura na mvitunze vitambulisho vyenu msivitupe kwani ndivyo vitakavyotumika kuipigia kura ya maoni katiba inayopendekezwa na kuchagua viongozi wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu,” alisisitiza Mama Kikwete.