Mama Salma Apigania Huduma za Afya kwa Wazazi na Watoto

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akizungumza

Na Anna Nkinda – aliyekuwa Paris

KUWEPO kwa upatikanaji wa haraka wa huduma za afya na wataalamu wa kutosha wa kutoa huduma hiyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kina mama wajawazito kujifungua salama na hivyo kupunguza vifo vyao na watoto vinavyotokana na tatizo la uzazi.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati alipozitembelea ofizi za shirika la AMREF Ufaransa zilizopo mjini Paris ili kuona jinsi linavyofanya kazi mbalimbali ikiwa ni kuhakikisha kuwa vifo vya kina mama wajawazito na watoto zinapungua barani Afrika.

Mama Kikwete ambaye pia ni mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa ujenzi zaidi wa vituo vya Afya, Zahanati, Hospitali, upatikanaji wa vifaa tiba na kuwepo kwa wingi wa wataalamu wa masuala ya afya kutasaidia kina mama wajawazito kupata huduma nzuri na hivyo kujifungua salama.

“Kina mama wengi wajawazito wanakufa kutokana na kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, Maralia na upungufu wa damu hivyo basi jitihada za pamoja baina ya Serikali na wadau wa afya zinatakiwa kuchukuliwa ili kuhakikisha kuwa kina mama hawa wanajifungua salama na kutokufa na magonjwa haya”, alisema Mama Kikwete.

Mwenyekiti huyo wa WAMA aliishukuru Taasisi ya AMREF International kwa kuanzisha kampeni Barani Afrika kwa ajili ya kuchangisha fedha za kuwasomesha manesi wengi ili kina mama wajawazito waweze kupata huduma ya kutosha wakati wa kujifungua na hivyo kujifungua salama.

Akisoma taarifa ya AMREF International Mkurugenzi wa Shirika hilo nchini Ufaransa Muriel Gavila alisema kuwa mpango mkakati waliokuwa nao nchini Tanzania katika kampeni ya kuwasaidia wanawake Barani Afrika kwa mwaka 2012 – 2015 ni kuchangisha shilingi bilioni 15 kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa manesi wakunga 3800 ili kina mama wajawazito waweze kupata bora zaidi.

Gavila alisema kuwa shirika hilo limekuwa likifanya kazi mbalimbali za kuhakikisha kuwa vifo vya kina mama wajawazito na watoto vinapungua, kutoa elimu kwa wahudumu wa afya na kutoa elimu ya uzazi kwa jamii.

AMREF Ufaransa imeahidi kufanya kazi kwa pamoja na Taasisi ya WAMA katika upande wa afya ya mama na mtoto ili kuhakikisha kuwa vifo vya kina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano vinapungua nchini Tanzania. Mama Kikwete alikuwa nchini Ufaransa na Mumewe Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa ajili ya mwaliko wa ziara ya kiserikali ya siku tatu.