Mama Salma Aitaka Jamii Kushirikiana Kuwalea Yatima

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete.

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete.

Na Anna Nkinda – Maelezo

JAMII imetakiwa kushirikiana kwa pamoja kuwalea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi kwani wengi wao hawana wazazi na walezi wao hawana uwezo wa kuwapatia mahitaji yao ya msingi ikiwemo elimu.

Mwito huo umetolewa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akizungumza kwenye hafla fupi ya kuwapongeza walimu wa shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama iliyofanyika katika viwanja vya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) jijini Dar es Salaam.

Walimu hao wa shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama iliyopo Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani ambayo ni ya watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu walipongezwa kwa kazi wanayoifanya ya kuwafundisha na kuwalea watoto hadi kumaliza kidato cha nne na kufanya vizuri katika mitihani yao ya Taifa.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA ambayo ndiyo wamiliki wa shule hiyo alisema bila kuwa na juhudi za dhati na za pamoja watoto wengi wa kundi hilo watakosa elimu ya Sekondari hali ambayo itawanyima fursa ya kujikwamua katika mzunguko wa umaskini.

“Napata faraja kubwa moyoni mwangu kwa mafanikio haya na ninaamini mtaungana nami kuwasaidia watoto yatima na wanaotoka katika mazingira magumu popote pale walipo, nawakaribisha mlee watoto wenu na kuchangia katika uendelezaji wa huduma hii muhimu”.

Ili kuhakikisha mradi huu unakuwa endelevu tumeanzisha program ya wanafunzi wanaolipa ada ili kuweza kupata rasilimali za kuwasomesha watoto wengi zaidi wasio na uwezo”, alisema Mama Kikwete.

Kwa upande wa walimu aliwapongeza kwa kazi wanayoifanya ya kuwalea watoto hao ambao wanahitaji msaada wa malezi na juhudi za umakini mkubwa katika kufundishwa ili waweze kufuzu na kuwataka waendelee na moyo huohuo huku wakifuata maadili yao ya kazi kwani wao ni kama wazazi.

Aidha Mwenyekiti huyo wa WAMA aliwashukuru wadau mbalimbali ambao wanatoa misaada katika shule hiyo ambapo hadi sasa wanafunzi 431 hii inamaana kuwa waliopo shuleni ni 363 na 68 waliomaliza kidato cha nne mwaka jana wamesajiliwa katika shule ya WAMA-Nakayama.

Akiongea kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mecky Sadick, Mkuu wa wilaya ya Ilala Raymond Mushi aliwapongeza wadau wote wanaotumia rasilimali zao kuwasaidia watoto hao ambao wameweza kupata elimu bure ambayo ni mkombozi wa maisha yao.

Mushi alisema, “Ukiona kuna watu wanahangaika kwa ajili ya maisha ya watoto ambao ni wahitaji hapo kuna njia kwa watoto hao ya kuwa na maisha mazuri hapo baadaye kwani vijana ni rasilimali ya taifa, jambo la muhimu ni kuendelea kutoa michango kwa WAMA ili kesho iwe nzuri kwa watoto hawa,”.

Kwa upande wa wadau wa ndani wanaoisaidia shule hiyo walimpongea Mama Kikwete kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwasaidia watoto hao na kuahidi kuendelea kushirikiana nanye ili kuhakikisha kuwa watoto hao wanapata elimu sawa na watoto wengine .

Naye Kaimu Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Suma Mensah alimshukuru Mama Kikwete kwa ushirikiano na ushauri anaoutoa kwa walimu hao jambo ambalo limesababisha walimu kufanya kazi kwa bidii na kujituma nahivyo wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao.

Taasisi ya WAMA ilianzisha shule hiyo ili kutoa mchango katika juhudi za taifa za kumkomboa mwanamke. Katika hilo wamelenga kutimiza malengo waliyojiweka ya kuwapatia fursa za elimu ya Sekondari watoto wa kike wanaotoka katika mazingira magumu wakiwemo yatima.

Kwa mara ya kwanza mwaka jana wanafunzi 68 wa kidato cha nne walimaliza katika shule hiyo na katika matokeo ya mtihani wa taifa hakuna mwanafunzi aliyefeli. Wanafunzi 10 walipata daraja la kwanza, 20 walipata daraja la pili, 19 daraja la tatu na 19 daraja la nne. Hadi sasa Taasisi hiyo imeweza kusaidia watoto zaidi ya 1000 kupata fursa ya elimu ya Sekondari na watoto 14 kupata ufadhili wa vyuo wa asilimia 100 katika fani mbalimbali.