MKE wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda amesema wanawake wa Tanzania bila kujali itikadi, rangi wala dini zao, hawana budi kuungana na kuwaombea viongozi wote ili wawe na ujasiri wa kutetea maslahi ya Watanzania.
“Tunapaswa tuwaombee viongozi wetu wa ngazi mbalimbali ili wapate maono na ujasiri. Tuwaombee ili watambue kwamba uongozi walionao ni dhamana waliyopewa na Mungu na kwamba wanapaswa kujiuliza wataisaidiaje Tanzania kusonga mbele na siyo kuuliza Tanzania itawafanyia nini,” alisema.
Mama Pinda ametoa kauli hiyo leo wakati akizindua Kongamano la Kitaifa la Wanawake Waombolezao litakalofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Sinza Christian Centre jijini Dar es Salaam. Kongamano hilo lilijumuisha wanawake kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania.
Alitumia fursa hiyo pia kuwaomba akinamama hao na viongozi wa kanisa la Tanzania Fellowship of Churches wakiongozwa na Askofu Godfrey Malassy wajumuike kuwaombea Waheshimiwa Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi ili waguswe na matatizo ya Watanzania.
“Sote tunaona jinsi mjadala unavyokwenda. Tumuombe Mungu awaguse waheshimiwa Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi zaidi ya milioni 45 ili wabaini kwamba wana jukumu la kuhakikisha wanawasaidia Watanzania kujikwamua kutoka kwenye umaskini ili waweze kupata maisha bora,” alisema.
Akizungumzia jukumu la wanawake kulea familia, Mama Tupu Pinda alisema akinamama wa Tanzania wana jukumu la kuwaombea vijana wa nchi hii na watoto ili wakue kwa kufuata maadili mema na kuishi maisha ya uadilifu.
“Wanawake ni walezi wa familia, tunalo jukumu la kuwaombea watoto wetu ili kuwakinga na kadhia za dunia hii. Tuwaombee ili wakulie katika imani, waweze kumcha Mungu. Hatuna budi kuwaombea kwa bidii ili kuwakinga na wimbi la utandawazi ambalo limeikumba nchi yetu ambapo maadili yanamomonyoka kwa kasi ya kutisha,” aliongeza.
Akisisitiza umuhimu wa maombi, Mama Pinda alisema: “Ni dhahiri kwamba mwanamke ndiye mwangalizi na mshauri wa familia ambayo ndio chimbuko la Taifa. Tutakaposimama imara kwenye nafasi zetu, kwa kupeleka mbele za Mungu yale yanayotukabili na kututatiza Kitaifa, kwa njia ya dua na maombezi, Mungu wetu atasikia naye atanusuru Taifa letu na majanga mbalimbali. Kwa yale ambayo sisi wanadamu tumeshindwa, Mwenyezi Mungu hashindwi kamwe!”
“Napenda kuwasihi wanawake tuendelee na moyo huu, kwani ni imani yangu kwamba wanawake wakiamua jambo litafanyika tena kwa ufanisi mkubwa kama ilivyonenwa katika Zab. 68:11 kwamba: “…. Wanawake…ni jeshi kubwa”. Tutumie nafasi yetu kama wanawake, kuunda jeshi kubwa la maombezi kwa ajili ya nchi yetu,” alisisitiza.
Mapema akimkaribisha Mama Pinda, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkesha Mkubwa Kitaifa ambayo imeandaa kongamano hilo, Askofu Godfrey Mallassy alisema akinamama wa Tanzania wano mzigo mkubwa wa kulia na kuomboleza kwa ajili ya Taifa la Tanzania.
“Taifa la Tanzania linakabiliwa na vita, vita vyake si vya kisiasa wala bunduki, si vya nyama na damu bali ni vita katika ulimwengu wa roho. Taifa letu linahitaji uponyaji wa kiroho na hakuna njia nyingine isipokuwa kwa sala na maombi,” alisema.
Alisema kama watu watasimama katika maombi, Tanzania itabadilika na kuwa na hali nzuri. “Tanzania itarudi mahali pake, itarudi kuwa tunu na wala bara la Afrika halipaswi kuwa bara la gizo kama wengi wanavyodai,” aliongeza na kuwahimiza wanawake kuiombea nchi kwa bidii.
Katika sherehe hiyo ya uzinduzi, Askofu Mallassy aliogoza maombi kwa ajili ya Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na viongozi wa wengine wa kitaifa ambapo aliwaita wake wa viongozi wasimame madhabahuni kwa niaba ya waume zao na kuwaombea.