Mama Pinda Aiasa Jamii Kusaidia Wasiojiweza

MKE wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda


 
MKE wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda amewataka Watanzania kujitoa kwa hali na mali kuwasaidia watu wenye uhitaji ili nao waweze kujiamini na kujiona wako sawa mbele ya jamii. Ametoa kauli hiyo leo, Aprili 23, 2013 wakati alipopewa fursa na Taasisi ya Catherine Foundation Development Limited ya jijini Arusha kuwa mgeni rasmi kwenye hafla fupi ya kutoa zawadi kwa watoto zaidi ya 160 wanaoishi kwenye kijiji cha Matumaini ambacho kinalea watoto yatima eneo la Kisasa, nje kidogo ya mji wa Dodoma.
 
Akizungumza na watoto wa kituo hicho, Mama Pinda alisema kazi iliyofanywa na Taasisi ya Catherine Foundation inasaidia kuwafanya watoto hao wajiamini kwa kuona kwamba kuna watu nje ya mkoa huo ambao pia wanawathamini na kuwakumbuka.
 
“Catherine Magige ni mbunge, kwa hiyo leo hii amewatia hawasa hawa watoto. Ni kama amewekeza kitu kwa watoto hawa ili nao wapate moyo wa kusonga mbele na kujiona kuwa wanaweza kuwa viongozi wa baadaye,” alisema.
 
Aliwataka watoto hao wasome kwa bidii ili waweze kuongoza kwenye masomo yao kuanzia shule ya msingi hadi watakapofika sekondari. Akipokea msaada huo kwa niaba ya mkurugenzi wa kituo hicho, mlezi wa watoto hao, Sista Suzana Maingu wa Shirika la Masista waabuduo Damu ya Yesu alimshukuru Mama Pinda, Bi. Catherine Magige na viongozi wengine alioambatana nao kwa upendo wao na kwa kutoa muda wao kuamua kuwatembelea na kuwafariji watoto hao.
 
Kijiji hicho ambacho pia kinalea watoto wanaoishi na Virusi vya UKIMWI, kilianzishwa mwaka 2002 kikiwa na watoto watatu na sasa hivi kina watoto 161 wanaolelewa kituoni hapo kwa mtindo wa familia kwenye nyumba 14 ambazo zina baba na mama wa kujitolea.
 
Zawadi zilizotolewa leo zenye thamani ya sh. milioni 3.2 ni mchele (kg. 150), unga wa mahindi (kg. 100), sukari (kg. 100), mafuta ya kupikia (lita 40), katoni moja ya sabuni za miche, sabuni ya unga (kg.60), madaftari 400, kalamu za wino 200 na penseli 100. Nyingine ni biskuti (katoni sita), pipi (pakiti nne), juisi (katoni 30) khanga doti 20 (kwa ajili ya walezi), nguo za watoto beli moja, miswaki (dazeni 10) na dawa za meno (dazeni 17).
 
Mama Pinda naye alitoa mbuzi wawili, lita 10 za asali, khanga doti tano na vitenge doti tano kwa ajili ya walezi wa watoto hao.
 
Mapema akimkaribisha Mama Pinda kuzungumza na watoto hao, muasisi wa taasisi hiyo, Bi. Catherine Magige ambaye pia ni mbunge wa viti maalum kwa tiketi ya vijana kutoka mkoa wa Arusha, alisema taasisi yake ni ya kijamii isiyofungamana na imani yoyote ambayo imedhamiria kuwafariji na kuwaonyesha upendo Watanzania wenye mahitaji hasa akinamama, watoto na watu wenye ulemavu.