Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete amewataka wanachama wa chama hicho pamoja na wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajia kufanyika mwishoni mwa wiki hii.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete alitoa rai hiyo jana wakati akiongea na wanachama pamoja na wagombea wa nafasi za Uenyeviti na Wajumbe wa Serikali za mitaa katika kata za Ndoro na Mikumbi zilizopo wilaya ya Lindi mjini.
Alisema kuna baadhi ya watu hawajiandikishi na wengine siku ya uchaguzi ikifika hawaendi kupiga kura, wanabaki kulalamika viongozi hawafai. Lakini kama wangeshiriki katika uchaguzi kusingekuwa na malalamiko kwa kuwa wangekuwa wamechagua viongozi wanaowataka.
“Siku ya uchaguzi ikifika amkeni mapema mkapige kura na msipoteze kura zenu kwa kuchagua watu wengine, chagueni viongozi wa CCM ambao chama chetu kimefanya mambo mengi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za afya, ujenzi wa shule na kuendelea kuimarisha amani ya nchi yetu,” alisema Mama Kikwete.
Aidha MNEC huyo pia aliwasisitiza wanachama hao wakati wa kujiandikisha majina katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali Kuu ukifika wawahamasishe wananchi wakajiandikishe ili waweze kuwachagua viongozi wao.
Akiwa katika mkutano wa kampeni uliofanyika mtaa wa Mto Mkavu Mama Kikwete aliwanadi kwa wananchi wagombea wa chama hicho wanaowania nafasi za Wenyeviti na Wajumbe wa Serikali za mitaa kutoka Kata ya Mbanja.
Aliwasihi vijana kubadilika na kujifunza historia ya nchi yao hapo ndipo watajua wapi nchi imetoka na wapi inakwenda kwani hivi sasa kuna watu wanapita na kuwadanganya hakuna maendeleo yoyote yaliyopatikana ukilingamisha na miaka ya nyuma.
Mama Kikwete alisisitiza, “Lazima mtambue kuwa Serikali ya CCM imeleta maendeleo kwa wananchi wake kwa kujenga barabara na hivi sasa kutoka Lindi hadi Dar es Salaam kwa gari dogo unatumia masaa matano na unaweza kwenda na kurudi, kwa basi siyo zaidi ya masaa saba. Leo watu wanapita na kuwadanganya hakuna maendeleo yaliyofanyika jambo ambalo siyo kweli”.
Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Lindi Mjini Muksini Rafii alisema kuna propaganda zinazosambazwa na wapinzani kuwa Serikali imesogeza mbele siku ya uchaguzi hadi tarehe 17 kitu ambacho siyo sahihi kwani uchaguzi utafanyika tarehe 14 mwezi huu kama ilivyopangwa.
Muksini alimalizia kwa kuwaomba wananchi kuwa makini katika uchaguzi wa viongozi kwani kuna watu wanapita na kuwadanganya wasiwachague wagombea wenye dini na makabila tofauti na yao wasiwasikilize, Tanzania haina dini wala kabila watu wote ni sawa na kuwasisitiza kuwachagua viongozi wa CCM ambao watawaletea maendeleo.
Katika mkutano huo wa kampeni wanachama wanne kutoka chama cha Wananchi (CUF) walimkabidhi Mama Kikwete kadi za chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi.