Na Anna Nkinda – Maelezo, Rufiji
WANACHAMA wa vikundi vya kukopa na kuweka akiba wametakiwa kuwa na uthubutu na kujiwekea malengo ya maendeleo kutokana na fedha wanazokopa kwa kufanya hivyo wataweza kujikwamua kutoka maisha ya umaskini na kuongeza kipato cha familia.
Rai hiyo imetolewa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati wa sherehe za kuadhimisha mwaka mmoja wa kuanzishwa kwa vikundi vya mradi wa Mwanamke Mwezeshe unaoongozwa na Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) zilizofanyika katika viwanja vya shule ya Sekondari ya Zimbwini iliyopo Kibiti wilayani Rufiji mkoa wa Pwani.
Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi hiyo alisema kupitia vikundi hivyo vya hisa wanawake wameweza kukopa na kuweka akiba na kufanya mambo ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kulipa ada za watoto, kununua mashamba, viwanja, kujenga nyumba na hivyo kuongeza thamani yao katika jamii kwani mwanamke akiwa na fedha mkononi hadhi yake inaongezeka lakini akiwa ombaomba hadhi yake inapungua na kudharaulika na mme wake.
“Pamoja na jina la mradi huu kuitwa mwanamke mwezeshe nawasihi wanaume msiogope kujiunga kwani lengo la mradi ni kumkomboa mtanzania kutoka maisha ya umaskini pia vikundi vilivyopo katika mfumo huu vimeweza kupata huduma ya bima ya afya kupitia mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) hali kadhalika kupitia vikundi wanachama ameweza kupewa mafunzo ya kuwaongezea ujuzi kupitia semina na maonesho”.
Muwe makini na waaminifu kwani vikundi hivi ni nyenzo muhimu ya kuwakomboa. Msikubli kuondolewa katika lengo lenu la msingi la kuinua hali zenu za maisha na kutumiwa na watu wabaya kufanya mambo yaliyo kinyume, mkumbuke amani ya nchi ikipotea waathirika wakubwa ni kina mama na watoto,” alisema Mama Kikwete.
Aidha Mwenyekiti huyo wa Taasisi ya WAMA alisema huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu na kupiga kura ya maoni na kuwataka wanavikundi hao kuhakikisha wanajitokeza kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kushiriki katika zoezi la kura za maoni na kuchagua katiba inayopendekezwa na mwishoni mwa mwaka huu kuchagua rais, mbunge na diwani.
Mama Kikwete alisisitiza, “Nawasihi ndugu zangu msiwasikilize watu atakao washawishi msijitokeze kujiandikisha au msiende kupiga kura ya maoni kuhusu katiba inayopendekezwa. Na baya zaidi msikubali kufanya mambo yanayoweza kuvuruga amani ya nchi, Historia inatufundisha kuwa kila palipoharibika amani walioteseka zaidi ni wanawake na watoto”.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Evarist Ndekilo aliishukuru Taasisi ya WAMA kwa kuwawezesha wanawake katika mkoa huo kwani hivi sasa wanaweza kutoa michango mbalimbali ya kifedha katika jamii zao bila ya kumtegemea mwanaume tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma. Alisema kupitia wataalam waliopo katika ofisi za Halmashauri za mkoa huo wakiwemo maafisa maendeleo ya jamii watahakikisha wanavisaidia vikundi hivyo ili viwe endelevu.
“Wanachama wa vikundi hivi nawaomba mshikamane na kushirikiana bila ya kufanya hivyo mradi huu hautakuwa endelevu WAMA wamewapa nyavu nendeni mkavue samaki, ipandeni hii mbegu mliyopewa iweze kustawi zaidi na hivi vikundi viwe vya mfano ili waliopo nje nao wajiunge,” alisema Ndekilo.
Akisoma risara ya vikundi hivyo Arafa Ngwaya ambaye ni mwalimu wa vikundi vya hisa na Katibu wa Umoja Ikwiriri alisema umoja huo umeanzishwa na vikundi vya hisa vipatavyo 51 venye wanachama 1643 kati ya hao wanaume 268 na wanawake 1375 ambavyo vimemaliza mzunguko wa mwaka wa kwanza na kugawana hisa ya shilingi 492,422,947/=.
Alisema madhumuni ya umoja huo ni kuviunganisha vikundi vya hisa wilaya ya Rufiji ili umoja uweze kusimama na kuleta ufanisi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya ujasiriamali na ya utunzaji wa kumbukumbu za fedha kwa wanachama wake na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika biashara zao. Kutafuta vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwemo michango ya wanavikundi na wanahisa na mikopo kutoka taasisi mbalimbali za kifedha ili kuweza kuvikopesha vikundi vya wanachama.
“Changamoto zinazotukabili ni hakuna vifa vya kutosha vya kuendesha ofisi vifaa hivyo ni samani za ofisi na Computer, tunahitaji msaada wa kitaalam ili tuweze kufungua benki yetu kwani tunahakika malengo yetu yakitimia na changamoto hizi kutatuliwa tutakuwa tumepunguza suala la umaskini kwa kiasi kikubwa kama si kuondoa kabisa katika wilaya yetu”, alisema Arafa.
Akiongea jinsi alivyoweza kunufaika na mradi huo Fatuma Mbuzi ambaye ni mkazi wa Ikwiriri anasema aliweka akiba na kukopa fedha za mkopo wa kwanza ambazo alizitumia katika mradi wa kutengeneza batiki, mkopo wa pili alinunua kiwanja na baada ya kumaliza mzunguko wa mwaka waligawana hisa na kununua shamba.
Mradi wa Mwanamke Mwezeshe ulianza kufanya shughuli za kijamii mwanzoni mwa mwaka jana katika wilaya za Rufiji, Kilwa, Liwale, Lindi vijijini, Nachingwea kwa ufadhili wa Financial Sector Deeping Trust (FSDT) unalenga kuanzisha vikundi 3000 vyenye jumla ya wanavikundi 60,000 kwa kipindi cha miaka mitatu.
Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana mradi ulikwishaunda vikundi 1,047 na kuwafikia wanavikundi 26,710 kati ya hivyo vikundi 450 viko wilaya ya Rufiji na vina wanavikundi 10,499. Mradi huo pia umetoa mafunzo ya kuweka akiba ambayo yatawawezesha wanavikundi kuweka akiba za jumla ya shilingi bilioni moja na nusu, kufikia mwishoni mwa mwaka jana mradi ulikusanya shilingi 1,518,643,430/= na hivyo kuvuka lengo la mwaka la kukusanya akiba ya shilingi milioni 500.