Mama Kikwete achangisha zaidi ya mil 45.4 kuwasaidia wagonjwa watoto wa saratani

Mama Salma Kikwete (kushoto) akipokea sh. 500,000 kutoka kwa Mbunge wa Viti Maalumu (CCM)anayewawakilisha walemavu bungeni, Al- Shaymaa Kwegyir wakati wa hafla ya matembezi kuchangia watoto wagonjwa wa saratani iliyofanyika Dar es Salaam, Hoteli ya Movenpick (Picha na Joachim Mushi)

Na Joachim Mushi

MKE wa Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa WAMA, Mama Salma Kikwete leo jijini Dar es Salaam amechangisha sh. milioni 45.4 kwa ajili ya kuwasaidia watoto wa chini ya miaka mitano na zaidi wanaoungua ugonjwa wa saratani nchini.

Fedha hizo zilichangishwa baada ya Mama Salma kuongoza matembezi ya mshikamano yalioanzia Viwanja vya Mnazi Mmoja na kumalizikia katika Hoteli ya Movenpick Dar es Salaam.

Akitangaza mchanganuo wa kiasi kilichochangwa Mama Salma alisema michango ya ahadi iliyotolewa na baadhi ya washiriki imefikia zaidi ya sh milioni 31.9 na fedha taslimu zilizopatikana zikiwa ni zaidi ya sh milioni 13, hivyo kupatikana zaidi ya milioni 45.4 kwa jumla.

Matembezi hayo yalioshirikisha viongozi mbalimbali wa Serikali, baadhi ya wabunge na taasisi zisizo za kiserikali – akiwemo Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Ummy Ally Mwalimu yalihudhuriwa pia na watoto kutoka shule anuai za msingi za jijini na baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.

Msanii maarufu wa filamu, Steven Kanumba (kushoto) akisaini kitabua cha michango kukubali kuchangia kiasi cha sh. milioni mbili kama mchango wake katika hafla hiyo. Kulia ni Msanii wa Muziki, Stara Thomas aliyechangia pia katika hafla hiyo.


Awali wakisoma hotuba yao kwa mgeni rasmi, Kampuni ya Edge Entertaiment ambao ni waandaaji wa matembezi hayo, kwa kushirikiana na Children in Crossfire wamesema kampuni hizo zimeguswa na matatizo ambayo wamekuwa wakiyapata watoto wagonjwa wa saratani ikiwemo mahitaji ya vyakula, nguo, maji, maziwa kwa watoto pamoja na nauli kwa wagonjwa wanaotoka mbali na hospitali.

Katika utafiti mdogo iliyofanya kampuni ya Edge imebaini Mkoa wa Dar es Salaam Wodi ya Saratani Muhimbili ina watoto 95, Mwanza watoto 70, Arusha watoto 66, Kilimanjaro watoto 82, Dodoma watoto 164, huku Zanzibar ikiwa na watoto 50 ambayo wote wako katika mazingira magumu.

Mradi huo wa kuwasaidia watoto wenye kauli mbiu ya “Saidia Watoto” uliopanga kukusanya kiasi cha sh. milioni 400, fedha zitakazochangishwa mikoa sita yaani Dar es Salaam, Dodoma, Kilimanjaro, Mwanza, Arusha pamoja na Zanzibar.