Na Joachim Mushi
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu amemfukuza kazi Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Profesa Alexander Songorwa kwa kile kutoridhishwa na utendaji wake wa kazi. Hatua hiyo ni mwendelezo wa kuwawajibisha vigogo ndani ya taasisi hiyo kwa kushindwa kutimiza wajibu wao.
Kwa mujibu wa taarifa ya Nyalandu kwa vyombo vya habari, wengine ambao wamewajibishwa ndani ya idara hiyo ni pamoja na Mkurugenzi Msaidizi wa Matumizi Endelevu ya Wanyamapori, Profesa Jafari Kidegesho, ambapo nafasi yake inachukuliwa na Dk. Charles Mulokozi. Waziri Nyalandu pia amemteuwa, Paul Sarakilya kukaimu nafasi hiyo ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori ya Wizara ya Maliasili na Utalii hadi hapo yatakapotokea mabadiliko mengine.
“…Natangaza kuubadili uongozi wa Idara ya Wanyamapori ya Wizara ya maliasili na Utalii kama ifuatavyo; Ninamuondoa Profesa Alexander Songorwa katika nafasi ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Nachukua hatua hii kutokana na kutokuridhishwa kwangu na utendaji wa kazi wa idara hiyo katika mapambano dhidi ya ujangili yanayoendelea nchini,” alisema Waziri Nyalandu.
Alisema kuwa pia hatua hiyo ni utekelezaji wa Azimio la Bunge lililotolewa Disemba 22, 2013, lililotaka Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori kuwajibishwa kutokana na tuhuma za uzembe na ukiukwaji wa haki za binadamu katika Operesheni Tokomeza.
Aidha alisema utekelezaji wa agizo hilo unaanza mara moja, huku akimteuwa Julius Kibebe kuwa Mkurugenzi Msaidizi Uzuiaji – Ujangili na anachukua nafasi ya anayeenda kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Alisema katika mabadiliko hayo Bi. Nebbo Mwina anaendelea kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo, Utafiti na Takwimu, na Herman Keiraryo anaendelea kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Uendelezaji wa Wanyamapori. Pamoja na Kitengo cha Uzuiaji – Ujangili nilichokitaja awali, hivi ni vitengo vya Idara ya Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utafiti.
“…Nawaagiza kwamba Wakurugenzi na Wakuu wote wa kila Idara, kila Shirika, na Taasisi zote ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii kutengeneza viashiria muhimu vya utendaji kazi (Key Performance Indicators) nakukabidhi kwangu ndani ya siku 30 zijazo. Viashiria hivi ni hatua ya kufanikisha yafuatavyo, 1) Malengo ya wizara, 2) Uwajibikaji, 3) Uwazina 4) Ufanisi katika utendaji wa kazi za kila siku. Ni sharti tutekeleze mikakati ya wizara katika mifumo inayopimika, tuweze kujipima natuweze kupimwa, natutumikie Taifa kwa uadilifu.”
“Kwa mtumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii ikiwemo mimi mwenyewe, Lazaro Nyalandu, atapaswa kuzingatia na kutekeleza majukumu ya kazi kwa kuzingatia Kanuni za Mwenendo (Code of Conduct) ambazo zitapendekezwa na kupitishwa na Baraza la Wafanyakazi wa Wizara. Baraza hili liwe limeitishwa na Katibu Mkuu wa Wizara kabla ya mwisho ya mwezi ujao. Azma ya kanuni hizi ni kuwa na misingi bora ya utumishi, uwajibikaji, utu, usawa na haki katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku.” Alisema na kumalizia kwa kauli ya ‘Mungu ibariki Tanzania’.