Dodoma
MWANASIASA mkongwe, Samuel John Malecela, amekitaka Chama cha Mapinduzi (CCM) kuchukua maamuzi thabiti ya kumalizana na dhana ya kujivua gamba kwa ama kutekeleza au kutangaza kuachana na mpango wa kuwatimua makada wa chama hicho wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi.
Malecela ambaye amepata kuwa Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), alitoa wito huo juzi wakati akizungumza ndani ya kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kilichokutana mjini Dodoma chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete.
Ingawa hakuwataja majina wanasiasa aliokuwa akiwalenga, kauli hiyo ya Malecela ilionekana ikielekezwa kwa Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa (CCM), na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM).
Habari ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka ndani ya kikao hicho cha CC zinaeleza kuwa pendekezo hilo la Malecela lilikataliwa na Kikwete mwenyewe ambaye katika majibu yake alisema wajibu wa utekelezaji wa dhana ya kujivua gamba ni wa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ambayo imepangwa kukutana Septemba mwaka huu.
Vyanzo kadhaa vya habari kutoka ndani ya kikao hicho, vimewaeleza waandishi wetu kwamba mbali ya majibu hayo, Rais Kikwete alisema utekelezaji wa maamuzi hayo ya NEC ulishaanza kwa hatua ya Makamu Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Pius Msekwa, kukutana na watuhumiwa hao mmoja mmoja.
Mjumbe mmoja wa Kamati Kuu aliyezungumza na Tanzania Daima alimkariri Rais Kikwete akisema taarifa iliyoandaliwa na Msekwa baada ya kukutana na watuhumiwa hao inaonyesha kwamba walikuwa wamepewa muda zaidi ya kupima wenyewe maamuzi ya NEC na kuchukua maamuzi ya kuwajibika.
Wakati Malecela akikunjua makucha yake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira, amekaririwa akieleza ndani ya kikao hicho hicho cha CC, kukerwa na kitendo cha viongozi wa juu wa chama hicho kukiuka maelekezo yanayowataka kuacha kushambuliana katika majukwaa ya kisiasa.
Pasipo kumtaja kwa jina, Wassira alieleza kusikitishwa na kitendo cha waziri mwenzake mwenye dhamana ya ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), Samuel Sitta, cha kuibeza serikali wakati akihutubia katika mkutano wa hadhara mkoani Mbeya.
Wassira aliwaambia wajumbe wa CC kuwa kuna viongozi wanatumia mikutano ya hadhara ya Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa, Nape Nnauye, kuikosoa serikali yao kwa ajili ya kujipatia umaarufu binafsi.
Sitta alikuwa miongoni mwa viongozi waliofanya mkutano wa hadhara mjini Mbeya ambapo alitumia mkutano huo kuitaka serikali iwaombe radhi Watanzania kutokana na uzembe uliosababisha kuwapo kwa matatizo makubwa ya mgao wa umeme.
Hata hivyo Rais Kikwete aliyekuwa akiongoza kikao hicho, hakujibu lolote kuhusu kauli ya Waziri Wassira dhidi ya Sitta.
Akizungumza na waandishi wa habari baadaye jana, Nape alisema wanaotuhumiwa kwa ufisadi wasipotekeleza agizo la NEC la kuwataka wajiengue wenyewe, ajenda yao itakuja kwenye kikao kijacho cha NEC kinachotarajiwa kufanyika mwezi ujao.
Nape ambaye amekuwa akizungumzia utekelezaji wa Kujivua Gamba kwenye mikutano yake ya hadhara katika mikoa mbalimbali nchini, alisema CCM iko tayari kupoteza wabunge, madiwani na wenyeviti wa vijiji na kuingia kwenye uchaguzi mdogo kuliko kuendelea kuwa na wananchama wanaotuhumiwa kwa ufisadi au wale wasiofuata maadili.
Kada huyo maarufu wa CCM, alisisitiza kuwa watuhumiwa wote wa ufisadi waliotakiwa kuwajibika, wanapaswa kufanya hivyo kabla ya NEC ijayo kwani chama hicho kiko tayari kuingia kwenye uchaguzi mdogo kuliko kuendelea kuwa na wanachama wasio na maadili ambao wamekuwa wakikiyumbisha chama.
Alisema hakuna mwanachama ambaye ni maarufu kuliko chama hicho, hivyo wanaofikiri wakiondoka CCM, chama kitayumba, wanajidanganya.
Aliongeza kuwa baadhi ya makada wanadanganywa na wenzao kuwa wakijiondoa kwenye chama hicho wataungana nao kwenda upinzani au kuanzisha vyama vingine vitakavyoiathiri CCM.
“CCM ni chama kikubwa, hakiwaogopi makada wake hasa wasiofuata maadili, tuna historia ya kuchukua maamuzi magumu na chama kimeendelea kukua siku hadi siku, walikuwapo kina Mrema, Maalim Seif na wengineo,” alisema.
Katika hatua nyingine, Nape alisema Kamati Kuu imepongeza kazi inayofanywa na sekretarieti ya chama hicho iliyochaguliwa Aprili mwaka huu.
“Kitendo cha CC, kupongeza kazi inayofanywa na sektetarieti hiyo kinajibu lawama na tuhuma zilizokuwa zikielekezwa kwake na kwa wajumbe wengine kuwa wanapotosha dhana ya Kujivua Gamba iliyoamriwa na NEC,” alisema Nape.
Alibainisha kuwa wajumbe wa sekretarieti walikuwa wakifanya kile walichoagizwa na NEC na kada yeyote ambaye hakuridhishwa na utendaji kazi, alipaswa kuwasilisha malalamiko yake kwenye vikao husika na wala si kupitia kwenye vyombo vya habari au maneno ya mitaani.
Alisema mtu yeyote makini hapaswi kukilaumu kioo kinapoonyesha uchafu wake bali anatakiwa atafute njia muafaka za kujisafisha.
Nape aliyekuwa akisoma maazimio ya Kamati Kuu alisema, kikao hicho kilipongeza uamuzi wa aliyekuwa mjumbe wa NEC Mkoa wa Tabora na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, kujiuzulu nyadhifa zake kwani uamuzi wake umezingatia maslahi mapana ya chama.
Hata hivyo, wakati Nape akisoma azimio hilo, taarifa zinaeleza kuwa hofu ya CCM kupoteza jimbo hilo la Igunga ilikuwa ni moja ya mambo yaliyoibua mvutano mkali wa hoja ndani ya Kamati Kuu kwa kiwango cha kusababisha Rais Kikwete awatahadharishe makada wa chama hicho kuachana na hatua za namna yoyote za kumpuuza au kumshambulia Rostam katika majukwaa ya siasa.
Mbali ya hilo, ili kuhakikisha jimbo hilo linaendelea kubakia mikononi mwa chama hicho, Kamati Kuu iliwazuia makada wake wawili, Nape na John Chiligati, kwenda katika kampeni za chama hicho za kusaka mrithi wa Rostam huko Igunga.