WAZIRI Mkuu mstaafu na mwanasisa maarufu nchini mzee John Malecela amefanyiwa upasuaji wa moyo. Akizungumza mjini hapa jana, Spika wa Bunge Anne Makinda aliwaeleza wabunge Malecela yupo nje ya nchi kwa ajili ya matibabu ambapo amefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo na ndio maana hata mkewe, ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Anne Kilango hayupo bungeni.
“Kuna wenzetu hawapo bungeni kutokana na mambo mbalimbali, Naibu Spika mnaweza kuuliza mbona haonekani. Amesafiri yupo nchini Uingireza na wabunge wengine watatu na watarudi wiki ijayo. Pia Kilango yeye yupo nje ya nchi kwasababu Malecela amefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo,” alisema Makinda.
Makinda alisema kukosekana kwa Kilango kunatokana na kuwa anamuugza mzee Malecela. Makinda hakusema Malecela upasuaji huo wa moyo amekwenda kufanyiwa nchi gani lakini. Hata hivyo taarifa za uhakika zinasema kuwa yupo nchini India.
Malecela licha ya kuwa Waziri Mkuu mstaafu pia amewahi kuwa mbunge wa jimbo la Mtera kwa kipindi kirefu. Hata hivyo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana hakuweza kugombea tena ubunge baada ya kubwagwa katika mchakato wa kura za maoni ndani ya chama chake cha CCM.
Jimbo la Mtera kwa sasa linashikiliwa na Livingstone Lusinde ambaye alifanikiwa kuchukua nafasi hiyo ya ubunge katika jimbo hilo baada ya kushinda uchaguzi huo.