MATUKIO ya kusikitisha kwamba wanamgambo wa kiislamu wameyaharibu maeneo ya makumbusho ya utamaduni katika mji wa Timbuktu nchini Mali. Inatia wasiwawasi kwa kuwa hatua ya wananamgambo hao haihusiani tu na utamaduni, bali pia inalenga kuliyumbisha kabisa bara zima la Afrika – sababu ya kutosha kuilazimu jumuiya ya kimataifa kukabiliana na hofu mpya ya mashambulizi ya kigaidi.
Ni ishara ya onyo lililo wazi. Kwa kutumia majembe na silaha wapiganaji wa kundi la waasi wa kiislamu la Ansar Dine waliyaharibu makaburi ya kihistoria mjini Timbuktu. Onyo hilo ni la dharura na linaelekezwa mataifa ya magharibi. Linaulenga pia utamaduni mpana wa eneo ambalo mji wake wa Timbuktu umetumika kama njia ya kibiashara tangu karne iliyopita. Ujumbe kutoka kwa msemaji wa waasi wa kundi hilo, Sanda Ould Boumana baada ya mashambulizi hayo ya kigaidi dhidi ya utamaduni ulikuwa wazi na mfupi: Hakuna kama Mungu. Sisi sote ni Waislamu. UNESCO ni kitu gani? Msemaji huyo alitangaza Jumamosi iliyopita kwamba makaburi yote 16 matakatifu ya udongo pamoja na misikiti yote mitatu mikubwa mjini humo yenye thamani muhimu kitamaduni, itaharibiwa. Na leo kauli yake imetimia.
Tangu mwaka 1988 mji wa Timbuktu umeorodheshwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO, kama mji wenye utamaduni wa kulindwa. Wiki iliyopita shirika hilo liliizindua jumuiya ya kimataifa kuhusu kitisho kinachoukabili mji wa Timbuktu. Kwa kuyaharibu makumbusho ya utamaduni ya mji huo, waasi wa Tuareg wa kundi la Ansar Dine wanafanya kama walivyofanywa wanamgambo wa kundi la Taliban nchini Afghanistan mnamo mwaka 2001 wakati walipoziharibu kwa mabomu sanamu za Budha katika mkoa wa Bamijan. Maandishi ni hayo hayo na itikadi ni hiyo hiyo moja iliyotumiwa na Taliban na inayotumiwa hivi sasa waasi wa Tuareg.
Wakati wanajeshi wa Marekani walipoingia Afghanistan mwaka 2001, wapiganaji wa al Qaeda walitafuta maficho mengine. Na waliyapata katika eneo la Afrika Kaskazini na eneo la Sahel ambayo hayadhibitiwi sana. Matukio ya ugaidi dhidi ya utamaduni yanaashiria kuenea kwa ugaidi wa kiislamu, au kwa maneno mengine utandawazi.
Nchini Yemen na katika mataifa ya eneo la Sahel, wanamgambo wa al Qaeda wanaweza kujificha na kuwapa mafunzo wengine. Kutoka hapa wanawatuma wapiganaji waliohitimu katika maeneo ya mbali kama vile barani Afrika. Kurejea na kuhamia Afrika ulikuwa uamuzi wa kimkakati, ili kuliyumbisha bara zima. Ni mchanganyiko hatari wa uhalifu wa kupanga, kukosekana uzalendo, taasisi dhaifu na itikadi kali ya kiislamu, inayohakikisha ugaidi wa kundi la al Qaeda unaenezwa kote barani Afrika kwa kasi kubwa.
Kuna kitisho cha kukua mtandao wa kigaidi kutoka kusini mwa Algeria na Libya kupitia mataifa ya eneo la Sahel kufikia hadi kaskazini mwa Nigeria. Kwa mantiki hiyo kuna kitisho cha bara la Ulaya kukabiliwa na ugaidi kutoka Afrika katika siku za usoni ikizingatiwa mabara hayo yanapakana.
Mhariri Mkuu wa Deutsche Welle, Bi Ute Schaeffer, anasema wakati umewadia kuyatambua maingilio haya na kuyapa majina. Wakati umekwisha sasa kutotilia maanani hatari iliyopo. Kundi l awanaitikadi kali la Boko Haram nchini Nigeria linaloyashambulia kwa mabomu makanisa si kundi dogo tu la wahalifu wa kiislamu au wapinzani wa rais mkristo wa nchi hiyo, Goodluck Jonathan. Hawataki chochote mbali na kuanzisha vita vya kidini vya Jihad nchini humo. Na wanafanya hivyo kupitia msaada kutoka nje kutoka kwa mitandao ya kimataifa ya ugaidi, ambayo sasa inawadhamini wanamgambo wa kiislamu nchini Mali. Wapiganaji wa Boko Haram watapokea mafunzo kutoka Mali au Yemen, silaha na fedha zinatiririka kuelekea kaskazini mwa Nigeria.
Wafadhili wa wapiganaji wa kiislamu nchini Mali na Nigeria ni kundi la al Qaeda katika eneo la Maghreb. Kundi hilo hupata fedha zake kutoka kwa utekaji nyara, biashara ya dawa za kulevya na silaha na kisha kuyasaidia makundi madogo ya kigaidi kusini mwa Afrika ambayo hayana fedha za kuendesha harakati zake.
Ulaya na Marekani lazima zifahamu wazi kuwa jeshi la Mali peke yake haliwezi kuwashinda waasi wa Tuareg wanaolidhibiti eneo la kaskazini mwa nchi. Na hata nchi jirani za Afrika hazijafanya chochote kukabiliana na ugaidi mpya nchini Mali. Mauritania kama jirani wa upande wa magharibi na Niger upande wa mashariki zenyewe zimekabiliwa na mfululizo wa mapinduzi na serikali zao si thabiti na hazidhibiti maeneo yao. Kiongozi wa Niger alikuwa na maneno mafupi na ya haraka haraka. “Taasisi zetu ni dhaifu mno kiasi cha kutoweza kufanya chochote kukabiliana na hali halisi ya mambo nchini Mali.”
Lazima kupatikane hatua za kuchukuliwa kwa haraka kabla maji hayajazidi unga. Makubaliano imara kati ya Marekani na Ufaransa na vile vile washirika wengine wa Ulaya, kuhusu kinachotakiwa kufanywa. Msaada wa dharura wa kifedha kwa jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika Magharibi, ECOWAS. Hatua hii tayari katika tume za amani za siku zilizopita imekuwa na ufanisi na inafaa
-DW