Na Sixmund Begashe, Wa Makumbusho ya Taifa
MAKUMBUSHO na Nyumba ya Utamaduni imekutana na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) na kufanya mazungumzo ya namna vyombo hivi vya Serikali vitakavyo weza kudumisha mashirikiano katika shughuli za kila siku ili kuhifadhi na kuendeleza Sanaa na Utamaduni wa Mtanzania.
Akizungumza kwenye kikao hicho Katibu Mtendaji wa BASATA, Godfrey L. Mngereza ameipongeza Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni kwa kuanzisha Program ya kila mwisho wa mwezi “Museum Art Explosion” ili kutoa nafasi kwa wasanii wa Tanzania kuosesha kazi zao za sanaa za Ufundi na za jukwaani kitu ambacho kinasaidia kukuza pato la msanii na pia kuutangaza Utamaduni wetu.
“Mashirikiano yetu BASATA na Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es Salaam yatasaidia vyombo hivi hasa Makumbusho kufanya kazi za Sanaa na Utabaduni kwa usalama mkubwa kwa kuwa BASATA itasaidia kuwamulika wasanii wasio tambuliwa na Baraza ambao watataka kufanya maonesho kwenye Makumbusho yetu na hasa kwenye hii program ya Museum Art Explosion” Aliongeza Bw. Mngereza.
Naye Mkurugenzi wa Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, Bw. Achiles Bufure, ameeleza kuwa mahusiano ya BASATA na Makumbusho hiyo ni ya kihistoria kwani BASATA ilihusika kwa kiasi kikubwa kwenye kutoa ushauri juu ujenzi wa mradi wa Nyumba ya Utamaduni na namna itakavyo tekeleza kazi zake za Maendeleo ya Sanaa na Utamaduni Nchini.
“Japokuwa tunatekeleza kazi zetu za msingi kama Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni kwa kupitia program mbali mbali za sanaa na Utamaduni lakini tumeona ni vyema tukakutana na wenzetu wa BASATA ili watuongezee maarifa zaidi ya namna ya kuziboresha hizi program zetu hususani hii ya MUSEUM ART EXPLOSION maana wao ni wabobezi wa Sanaa na Utamaduni”. Alisema Bw Bufure
Kikao hicho kilicho udhuriwa na wajumbe wa tano kutoka Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni na wanne kutoka BASATA kiliangazia mashirikiano katika nyaja ya Utoaji elimu kwa Wasanii, Mawasiliano, Utafiti na Maonesho ya kazi za Sanaa hivyo kamati ndogo ziliundwa ili zitoke na mapendekezo zaidi yatakayo wezesha vikao vya juu kupitia na kupitisha maamudhi sahii.