Makubaliano ya Kongamano la Uwekezaji Ukanda wa Ziwa Tanganyika

Rais Jakaya Kikwete akizindua Tovuti (Website) ya Ukanda wa Ziwa Tanganyika, wanaoshuhudia ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Viwanda na Biashara Marry Nagu (kulia) Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Col. Mst. Issa Machibya (kushoto) na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng. Stella Manyanya. Tovuti hiyo ni www.laketanganyikazone.go.tz

HIVI karibuni wilayani Mpanda lilifanyika Kongamano la Uwekezaji Ukanda wa Ziwa Tanganyika (Oktoba 17, 2011) na kuhudhuriwa na wajumbe zaidi ya 300.
Mgeni rasmi katika Kongamano hilo alikuwa ni Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda (MB) alikuwa ni Mwenyekiti wa Kongamano hilo.

Kongamano lilihudhuriwa na mawaziri mbalimbali, mabalozi, wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi pamoja na wadau mbalimbali wa uwekezaji wakiwemo wajasiriamali na viongozi wa chama na Serikali.

Yalikuwepo maonyesho kwa njia ya mabanda ambayo wajasiriamali tofauti na baadhi ya wawekezaji walinadi bidhaa na fursa mbalimbali za uwekezaji. Maonesho hayo yalikuwa ya siku nne (4) kuanzi Oktoba 15-18, 2011.

Mada mbalimbali ziliwasilishwa katika kuonyesha fursa zilizopo kwenye Ukanda wa Uwekezaji wa Ziwa Tanganyika, Aidha Halmashauri zote za Mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi zilipata fursa ya kunadi miradi yake ambayo inahitaji uwekezaji.

Ili kufanikisha adhma ya kufungua Ukanda wa Uwekezaji wa Ziwa Tanganyika, Kongamano hilo lilifikia makubaliano kadhaa ambayo yakifanyiwa kazi ipasavyo itarahisisha na kufanikisha uwekeza kwa njia rahisi, Makubaliano hayo ni kama ifuatavyo:

*Halmashauri zote kutenga maeneo maalum kwa ajili ya uwekezaji.
*Hakuna maendeleo ya kiuchumi bila uwekezaji.
*Kuinua rasilimali zilizopo kwa kuongeza uzalishaji.
*Uwekezaji katika sekta ya nishati upewe kipaumbele cha kwanza.
*Ianzishwe ofisi ya Uwekezaji (TIC) katika Ukanda wa Uwekezaji wa Ziwa Tanganyika.
*Awepo mtu maalum (One Stop Centre) ambaye atakuwa kiunganishi kwa Mikoa yote mitatu (Rukwa, Kigoma na Katavi)
*Kujenga mfumo mmoja unaokubalika na wote kwa ajili ya uwekezaji tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo kuna baadhi ya watu wanaukubali uwekezaji na wengine wanaukataa.
*Jamii ishirikishwe ipasavyo katika kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji kwa mujibu wa sheria (Act No: 48.5) ili kuepusha migogoro isiyokuwa ya msingi.
*Kuvutia uwekezaji katika sekta ya ufugaji wa nyuki.
*Mikoa yote kushawishi wawekezaji wa ndani.
*Kutambua na kuainisha maeneo kwa ajili ya huduma za mawasiliano
*Kuwaongezea uwezo watendaji katika Serikali za Mitaa na Halmashauri ili waweze kufanya mambo kwa ufanisi zaidi.
*TIB (Benki ya Uwekezaji Tanzania) ipitie sera zake za mikopo upya kuwawezesha watanzania wa hali ya chini kupata mikopo na kuwekeza.
*Kuandaa mpango mkakati wa matumizi bora ya ardhi kwa mkoa mpya wa Katavi.
*Kuandaa mipaka sahihi katika Ziwa Tanganyika kuweza kuruhusu uchimbaji wa mafuta kirahisi.
*Makubaliano hayo yalifikiwa na wajumbe wote wa mkutano huo ili kufanikisha uwekezaji wenye tija na wa kudumu katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika.
Aidha makubaliano hayo yalipata Baraka zote kutoka kwa wajumbe wakiongozwa na mwenyekiti wa Konagamano hilo Waziri Mkuu wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda.

Makubaliano hayo yakifanyiwakazi ipasavyo ni wazi kuwa Ukanda wa Uwekezaji wa Ziwa Tanganyika utapata taswira tofauti na mafanikio makubwa.