ASKOFU Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini, amesema makovu yaliyotokea katika vita vya Kagera vilivyoanzishwa na Nduli Idd Amini wa Uganda hayawezi kusahaulika kwa wakatoliki wa Kasambya na hata wana-Kagera wote.
Kilaini ametoa kauli hiyo jana alipokuwa akiwahubiri waumini wa Parokia Kasambya Kyaka na wageni anuai, kwenye Jubilee ya Miaka 75 ya kuanzishwa kwa Parokia hiyo iliyopo wilayani Misenyi.
Akifafanua zaidi, Kilaini alisema katika vita hivyo kati ya Tanzania na Uganda, Kanisa hilo lilipata athari kubwa kutokana na vita hivyo, jambo ambalo limefanya mpaka sasa uchumi wa familia nyingi haujatengemaa.
Aidha aliwapongeza baadhi ya watu ambao wamekuwa na moyo wa kusaidia maendeleo ya wana jamii eneo hilo hasa vijana waliozaliwa Kasambya-Kyaka Wilaya ya Misenyi ambao wamekuwa na moyo mzuri kwa kusaidia maendeleo ya Kanisa na Parokia hiyo.
Hata hivyo aliwashukuru wageni mbalimbali waliofika katika jubilee hiyo ya miaka 75 ya Parokia ya Kasambya, na kuongeza kuwa yote ni mapenzi ya Mungu aliyewaweka hai hadi kufikia katika sherehe hiyo ya Jubilee.
Aidha alimshukuru mgeni rasmi katika sherehe hizo, Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Dioniz Malinzi kwa kuungana na waumini wa kanisa hilo katika Jubilee hiyo.
Mwenyekiti wa BMT, ambaye pia ni Mdhamini wa Kanisa hilo, Dionis Malinzi katika Jubilee hiyo aliongoza harambee na kuchangisha zaidi za milioni 10, fedha ambazo zitatumika kujenga nyumba ya kuishi mapadre na maaskofu parokiani hapo. Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Nchimbi, aliahidi kutoa mabati ya kukamilisha nyumba nzima ikiwa ni mchango wake kwenye harambee.
Habari na picha hizi ni kwa hisani ya Blog ya Full Shangwe-Bukoba