Na Walusanga Ndaki
JANA mtandao huu (sio dev.kisakuzi.com) uliandika makala iliyokuwa na kichwa cha habari ‘MAKOSA’ ya Waziri Mulugo ni ya Bahati Mbaya au Ufahamu Mdogo? Katika makaka hiyo tulionyesha makosa yaliyokuwa ndani ya hotuba ya naibu waziri huyo wa elimu aliyoitoa katika mkutano wa wataalam wa elimu huko Afrika Kusini mwanzoni mwa mwezi huu.
Baada ya wimbi kubwa la malalamiko ya umma kuhusu hotuba yake hiyo iliyokuwa imejaa dosari nyingi, waziri huyo leo alizungumza na kituo cha Clouds FM akikiri dosari hizo japokuwa kwa kujitetea kijanja. Katika kuonyesha kwamba umakini kwa watumishi wa umma nchini ni mdogo sana, ni jinsi waziri huyo alivyokuwa akiisoma hotuba hiyo bila hata kushitukia chochote.
Kwanza kabisa, kwa ufahamisho, ni kwamba mfumo wa sasa wa hotuba duniani ni kwamba msemaji anaposoma hotuba yake wakati huohuo huonyeshwa na kompyuta katika kiwambo ambapo washiriki wengine wanaweza kuifuatilia pia kwa kuisoma. Mtandao huu umeandika yote yafuatayo kwa kufuatilia matamko ya hotuba ya Mulugo ambayo yalikwenda sambamba na hotuba yake ambayo ilionekana kwa ajili ya kusomwa.
Mfano wa kosa la kizembe la Mulugo ni pale aliposema kwamba Tanzania inapakana na nchi nane. Miongoni mwa nchi hizo nane alizozitaja ajabu ni kwamba nchi ya Burundi haikuandikwa katika hotuba yake japokuwa aliitaja toka kichwani!
Jambo jingine, ni kwamba miongoni mwa nchi hizo zinazopakana na Tanzania aliitaja nchi moja kwa jina la “Congo DRC”, hii ni kwa mujibu wa alivyotamka katika hotuba yake na jinsi ilivyokuwa imeandikwa katika hotuba hiyohiyo.
Kiuhalisia, hakuna nchi kama hiyo inayopakana na Tanzania. Nchi inayopakana na Tanzania miongoni mwa nchi nane alizozitaja ni Congo DR au Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Si “Congo DRC” aliyoitaja waziri Mulugo.
Kama Mulugo hakuliona kosa lake na alikuwa bado hajaliona hadi leo wakati anaongea na Clouds FM ni kwamba kirefu cha “Congo DRC” (kama kweli nchi hiyo ipo) ni “Congo Democratic Republic of Congo”!
Waziri Mulugo alisema kwamba neno Zanzibar alilitaja kimakosa kama Zimbabwe wakati wa hotuba yake akielezea nchi zilizounda muungano wa Tanzania, kwa vile msemaji aliyekuwa amemaliza kusema kabla yake alikuwa ametoka Zimbabwe.
Hata hivyo, katika kuisoma hotuba yake iliyokuwa imeandikwa “…islands of Pemba and Zanzibar…” aliisoma kama “…islands of Zimbabwe and Pemba…”.
Angalau kama kweli ni kwa kukosea angeisoma kama “…islands of Pemba and Zimbabwe…”, lakini kwa vile hakuwa makini, jicho na akili zake vilikimbilia neno ‘Zimbabwe’ kwanza kabla ya kuitaja Pemba ambayo ndiyo ilikuwa ianze, kama hotuba yake ilivyokuwa imeandikwa!
Hebu ona hili lifuatalo! Katika hotuba ileile, kuna aya iliyokuwa imeandikwa ifuatavyo: “The United Republic of Tanzania is located on the east cost of Africa.”
Hapa kuna makosa mawili yaliyokuwemo katika hotuba hiyo aliyoisoma. Kosa kubwa la kwanza hapa ni neno “cost” ambalo ni la Kiingereza, maana yake ni “gharama” (likiwa ni nomino) au “kugharimu” (kitenzi).
Hivyo, hilo ni kosa la waziwazi na la kuchekesha na kuchefua lililokuwa katika hotuba ya Mheshimiwa Mulugo!
Neno sahihi lilibidi liwe “coast” yaani “pwani”. Kwa mujibu wa hotuba hiyo ya Mulugo ambayo huenda aliiandika yeye mwenyewe au kuandikiwa, sentensi hiyo ya “The United Republic of Tanzania is located on the east cost of Africa” ingemaanisha nini?
Ingemaanisha kwamba “Jamhuri ya Muungano ya Tanzania iko mashariki mwa “gharama” (au “gharimu”) mwa Afrika!
Unaona kichekesho hicho?! Hiyo ni hotuba ya waziri wa Tanzania aliyoiweka kwenye mkoba, akapanda ndege, akafikia hoteli ya kisasa, akala na kulala ambapo kesho yake akaenda mbele ya wasomi wenzake na kupeleka hotuba hiyo ya kusikitisha!
Siyo hivyo tu, Mulugo aliingiza maneno mengine kutoka kichwani ambayo hayakuwemo kwenye hotuba yake hiyo. Mfano, aliingiza neno “geographically” katika sentensi hiyo kabla ya neno “located”, kitu ambacho kilionyesha wazi hakuwa anaiamini au aliipuuza hotuba yake hiyo iliyokuwa imeandikwa!
Makosa ni mengi ajabu. La pili ni kwamba sentensi hiyohiyo aliisoma hivi: “The United Republic of Tanzania is geographically located in east Africa.” Kwa aliyeisoma vizuri sentensi hii atangundua kwamba ilikuwa na kasoro mbili. Ya kwanza ni kwamba Mulugo aliongeza neno “geographically” ambalo halikuwa limeandikwa katika hotuba hiyo. Pili, ukiisoma vizuri sentensi hiyo kuna maneno ambayo aliyaacha katika hotuba hiyo ambayo yalikuwa yameandikwa.
Makosa ni mengi, na yote ni mfano mzuri wa uzembe na kazi za kulipua zinazofanywa na watumishi wa umma karibu katika kila kona. Cha kusikitisha zaidi ni kwamba uzembe huu wa kisomi umefanywa na mtu ambaye akiwa anazungumza na Clouds FM alijisifu kuwa ni msomi na mtu ambaye aliwahi kuwa mwalimu, lakini uhalisia umeonyesha mapungufu yake makubwa!
Waziri Mulugo ni mmoja tu ya mifano ya kusikitisha na kuudhi inayokwenda kwa jina la viongozi, watu ambao wengi wao wamekuwa ni kichocheo cha kuwakatisha tamaa wananchi wenzao kwa kuwaongezea majonzi ya kiuchumi, kijamii na kisiasa kutokana na kukosa umakini katika kazi zao.
Pia tukio hilo la Mulugo linachochea madai lukuki kwamba uongozi wa nchi hii ni jambo la “kupeana” kirafiki na si lenye kutokana na utaalam au utendaji bora! Kwa Mulugo, njia ya kujitoa katika aibu hii na kupunguza hasira za Watanzania ni KUACHIA NGAZI MARA MOJA!
-http://www.globalpublishers.info/