MTOTO wa Rais wa kwanza wa taifa la Tanzania anagombea nafasi ya ubunge katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) kutimiza adhma ya Baba yake ya kuwa na Afrika Mashariki iliyoungana. Charles Makongoro Nyerere, mwanasiasa machachari na mtoto wa kiume wa Rais mwanzilishi wa taifa la Tanzania, ni miongoni mwa wanachama wa chama tawala, Chama cha Mapinduzi wanaowania nafasi nane za chama hicho katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA).
Mwandishi Nicodemus Ikonko wa Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) alimhoji mgombea huyo wa nafasi hiyo ya ubunge wa kanda na kutaka kujua matarajio yake iwapo atachaguliwa kwenye nafasi hiyo…endelea.
Swali.
Nini kimekusukuma kugombea nafasi hiyo ya ubunge katika Bunge la
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA)?
Jibu.
Napenda ieleweke kwamba Bunge la Afrika Mashariki lina nafasi ya pekee katika kanda hii kutokana na nafasi yake kama chombo muhimu katika muundo mzima wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na majukumu yake katika kuimarisha na kupanua mwenendo mzima wa mtangamano ndani ya kanda.
Kutokana na sababu hiyo, nimeamua kuingia katika kinyang’anyiro hiki
ili niweze kuiwakilisha nchi yangu, watu wake na matakwa yao vilivyo
katika bunge hilo la kanda iwapo nikichaguliwa na Bunge letu la
Kitaifa kushika nafasi hiyo.
Swali.
Iwapo utachaguliwa kuwa mwakilishi katika Bunge la Afrika Mashariki, ungependa nini kifanyike katika muda utakaokuwa mwakilishi
kwenye bunge hilo?
Jibu.
Mungu akipenda nikakachaguliwa kuwa mbunge wa EALA, ningetaka kuona kwamba malengo mawili yaliyosalia ya EAC, ambayo ni Umoja wa Sarafu na Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki ambalo ndilo kwa muda mrefu limekuwa likisubiriwa, yote yanatimizwa mapema iwezekanavyo.
Malengo mengine mawaili ya awali ya EAC, yaani, Umoja wa Forodha na
Soko la Pamoja, tayari yameshaanza utekelezaji wake kwa mujibu wa
sheria na taratibu zilizorejesha upya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Swali
Kwa mtazamo wako, EALA ina changamoto gani?
Jibu
Naamini kwamba changamoto kumbwa kwa EALA, nionavyo mimi ni kutekeleza malengo mawili yaliyosalia ya Jumuiya ya Afrika mashariki ambayo ni pamoja na Umoja wa Sarafu na Shirikisho la Kisiasa la Afrika
Mashariki.
Ninaamini pia na kufikiri kuwa utekelezaji wa malengo hayo yaliyosalia
ufanywe kwa kufuata na kuzingatia misingi inayotawala Jumuiya na nchi
wananchama za Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi. Pia naamini
kwamba EALA haina budi kuchukua nafasi yake muhimu katika kutunga
sheria zitakazoleta manufaa kwa nchi wananchama.
Swali
Unadhani unaweza kuwasha upya adhma nzito ya marehemu Baba yako,
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya kutaka kuona Afrika Mashariki
iliyoungana iwapo utachaguliwa kuwa mbunge wa EALA?
Jibu
Kwanza ningependa kuchukua nafasi hii kukiri kwamba Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere, Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alikuwa kweli mwuumini mkubwa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kama historia ingempatia nafasi wakati wa uhai wake wa kulitumikia
taifa kutimiza adhma yake , naamini kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki
iliyokuwa ndoto yake, labda sasa ingeshakua na kufikia hatua ya kuwa
Shirikisho imara la Kisiasa la Afrika Mashariki.
Lakini ninadhani kwamba kwa muda tuliokuwa nao hivi sasa, kufanikiwa
kwa ndoto ya Mwalimu kunategemea kwa kiasi kikubwa nia njema ya
viongozi pamoja na wananchi katika nchi wananchama wa jumuiya hiyo.
Njia moja bora zaidi ya kuwasha upya ndoto hiyo ni kupitia EALA kwa
kuhakikisha kwamba watu/raia katika jumuiya wanashirikishwa vilivyo
katika mchakato mzima wa kufikia mtangamano wa wana Afrika Mashariki.
Nikichaguliwa nitawasha upya ndoto ya Mwalimu kwa kushirikiana kwa
karibu na wabunge wenzangu wa EALA kutimiza malengo ya EAC.