MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amezitaka taasisi na mashirika ya umma yaliopo chini ya mkoa wake kuiunga mkono Kampuni ya Simu ya kizalendo Tanzania (TTCL) kwa kuanza kuzitumia bidhaa za kampuni hiyo hasa kwenye shughuli za mawasiliano ili kuonesha uzalendo kwa vitendo.
Makonda ametoa kauli hiyo leo Makao Makuu ya TTCL jijini Dar es Salaam alipokuwa akizinduwa Wiki ya Huduma kwa Wateja wa kampuni ya TTCL, huku akiahidi kuzishawishi taasisi na mashirika ya umma yanayofanya kazi chini ya utawala wake kuhakikisha wanatumia huduma za TTCL ili kuiunga mkono kampuni hiyo ya kizalendo ya mawasiliano.
Alisema Serikali imeonesha nia njema ya kuirejesha TTCL katika hali nzuri baada ya kuirejesha kwa asilimia 100 chini ya umiliki wake, hivyo kuyataka mashirika na taasisi za umma kuunga mkono juhudi za Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli kuirejesha kampuni hiyo chini ya umiliki wa serikali kwa asilimia 100. Alisema yete kama kiongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam atahakikisha ofisi zote za umma zilizopo chini ya mkoa wake zitatumia huduma za TTCL na endapo watendaji wa TTCL sinazosita kutumia watoe taarifa ili yeye ahoji ni kwanini wanapinga agizo hilo.
Aidha Mkuu wa Mkoa huyo alisitaka baadhi ya taasisi za umma wadaiwa sugu wa TTCL walipe madeni yao mara moja na zile zinazokaidi zifikizwe kwenye mkono wa sheria (mahakamani) kwa ajiri ya taratibu za kisheria. Alisema kampuni itafanya vizuri kihuduma endapo wateja wanaopewa huduma wanalipa kwa wakati ili iweze kuboresha huduma zake kwa wateja wote.
Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri Waziri Kindamba akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa Makonda alisema Kampuni ya Simu Tanzani iliianza mchakato wa kuleta mabadiliko ndani ya kampuni hiyo tangu mwaka 2014, mpango uliopewa jina la ‘TTCL Business Transformation Project’ ambao ulilenga kuongeza tija na ufanisi katika uzalishaji na uwajibikaji ili kutoa huduma bora kwa Wananchi na Wateja wetu wote wa ndani na nje ya Tanzania.
Aliyataja miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi chote cha mabadiliko ya kibiashara ni pamoja na kuirejesha Kampuni ya TTCL kumilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 baada ya kuondoka kwa aliekuwa mbia mwenza, kupatikana kwa Masafa yanayowezesha kutolewa kwa huduma za 3G/4G na utekelezaji wa miradi mbali mbali ya kuboresha huduma.
Kindamba aliongeza mafanikio mengine ni kupatikana kwa fedha kutoka kwenye vyanzo mbalimbali ikiwemo Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB), Kupatikana fedha kutoka Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ambazo zinatumika kwa ajili ya kupeleka mawasiliano vijijini na Ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya mtandao wa Mawasiliano, mitambo chakavu, kusimika mitambo ya GSM-2G, UMTS- 3G na LTE- 4G.
“…pia katika eneo la Biashara; Tumeendelea na juhudi za kutangaza na kuitambulisha huduma ya 3G/4G katika jiji la Dar es salaam, bidhaa nzuri ambazo zinakidhi mahitaji ya wateja zimekuwa chachu ya wananchi kuanza kuvutiwa na bidhaa za TTCL. TTCL tunatoa huduma ya T-TV ambayo wateja wanapata fursa ya kutazama matangazo ya vituo mbalimbali vya Luninga kupitia simu zao za Smartphone na tablet. Pia, TTCL imefanikiwa kuunganisha Hospitali Kuu za Mkoa wa Dar es salaam katika Mkongo wa TTCL, hivyo kutengeneza mazingira mazuri kwa taasisi hizo kuendesha huduma za afya kwa kutumia teknolojia yaani Afya-Mtandao (E-Health),” alisema Kindamba.
Aidha alisema wiki ya Huduma kwa Wateja, TTCL inalenga kutambua na kuthamini mchango wa wateja, ambao wamekuwa chachu ya ukuaji wa Kampuni, huku kampuni ikijipanga kuwatembelea wateja wake, kuzungumza nao na kuomba ushauri wao ili tuweze kutoa huduma bora na endelevu ambazo zitaongeza tija katika kazi zao.
“…Tumejipanga vyema kufanya kazi kwa ufanisi, tunatekeleza kwa vitendo falsafa ya Serikali yetu ya awamu ya tano ya Hapa Kazi Tu. Tutatumia rasilimali zetu vizuri ili Kampuni itoe mchango stahiki mageuzi yanayoendelea ya kuifanya nchi yetu kupiga hatua kuelekea kuwa nchi ya Uchumi wa Kati, Nchi ya Uchumi wa Viwanda. Katika kufikia lengo hili, huduma za Mawasiliano ni muhimu sana, na napenda kukuhakikishia kwamba, kwa kutumia huduma za TTCL, lengo hili litafikiwa,” Alisema.