Makonda Akabidhi Majina Mengine ya Watuhumiwa Dawa za Kulevya

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ‘RC’ Paul Makonda akizungumza.

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda leo amekabidhi orodha nyingine ya watuhumiwa wa dawa za kulevya ili waweze kushughulikiwa na Mamlaka Mpya ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya. Makonda amekabidhi faili la majina hayo kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Rogers William ambaye ameahidi kuendeleza moto ule ule wa mapambano ili kuhakikisha wanatokomeza biashara hiyo haramu.

Makonda alisema kelele zinazopigwa na baadhi ya watu katika vita hiyo ndiyo kwanza zinaongeza kasi ya mapambano na awamu ya kuwataja majina wahusika inaendelea hadi awamu ya saba. Alisema kampeni hiyo ya mapambano imeanzia ngazi ya serikali na inapaswa kwenda hadi ngazi ya familia kuhakikisha kila mmoja anapambana kutokomeza biashara hiyo inaloliangamiza kundi kubwa la nguvu kazi za taifa.

Alisema kundi la majina ya awamu ya tatu ni la vigogo wanaofanya biashara hiyo tangu enzi za utawala wa Rais wa Awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi huku wakifanya biashara hiyo kwa kiwango kikubwa. Katika kundi hilo wapo baadhi ya viongozi na watoto wa viongozi ambao wamekuwa wakitumia nafasi na nyadhifa kusaidia biashara hizo kufanyika huku wenyewe wakinufaika na asilimia ya mapato ya biashara hiyo.

Alisema Tanzania imekuwa kama njia ya upitishaji biashara ya dawa za kulevya na utafiti ukionyesha kati ya kilo 10 hadi 15 za dawa ya kulevya aina ya kokeni ‘cocaine’ imekuwa ikisambaa kwa wauzaji na watumiaji kwa siku moja jijini Dar es Salaam.

Alisema wana taarifa za baadhi ya viongozi wa dini wanaojihusisha na dawa hizo na wanazifanyia kazi kisha watawataja na kuwashughulikia bila kujali wapo makanisani au misikitini, lengo likiwa ni kumaliza kabisa mtandao wa biashara hiyo haramu.

“…Leo ninakabidhi majina ya awamu ya tatu lakini tutaendelea hadi awamu ya saba tukiwashughulikia wafanyabiashara hizi. Dar es Salaam ndio kitovu cha dawa hizi na endapo tutafanikiwa tutakuwa tumesaidia na mikoa mingine…,” alisema.

Makonda alisema zipo bandari bubu, hoteli na majumba ambayo yameshamiri kufanya biashara hizo na kwa sasa vikosi maalumu vipo kazini kuwafuatilia na wote watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Alisema biashara ya dawa za kulevya jijini Dar es Salaam ilikuwa imeshamiri na kufanyika wazi wazi jambo ambalo ni hatari kwa taifa.

Alishangaa kuona baadhi ya watu wakipiga kelele kupambana naye anapotokomeza mtandao huo, na kumuomba Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kuweka utaratibu wa kuwapima wabunge kila wanapokuwa wanaingia bungeni ili kubaini wanaojihusisha na dawa hizo kama alivyo wahi kusema bungeni katika vikao vya nyuma.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Rogers William alisema kikosi kipya kimejipanga kupambana na mtandao wa dawa za kulevya nchini na nje ya nchi na kwa sasa wanaanza kuwashughulikia baadhi ya maofisa wa serikali ambao wamebainika kuruhusu kuingia kwa kemikali za dawa za kulevya.

Alisema wapo majaji na mahakimu ambao wamebainika kuvuruga kesi za watuhumiwa wa dawa za kulevya wanaandaa orodha yao watawafikisha katika mamlaka husika ili wachukuliwe hatua kwa kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria.

Alifafanua kuwa sheria imewapa nguvu ya kuwakamata watumiaji wa dawa za kulevya ili wasaidie kuwataja wanaowauzia na imeruhusu kuitaifisha hata mali iliyopatikana kwa biashara hiyo haramu kwa muhusika. Aliwataka wananchi na viongozi wote kuunga mkono juhudi za RC Makonda katika vita hiyo ili kuokoa familia zetu na nguvu kazi ya taifa ambao ni vijana wanaoteketea kwa matumizi ya dawa hizo.