KOCHA wa Yanga SC, Mholanzi Hans van der Pluijm amesema kwamba hana wasiwasi kabisa na mahasimu, Simba SC kuelekea mpambano wa Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na anachokifanya kwa sasa ni kuiandaa timu yake tu.
Yanga itamenyana na Simba Jumamosi katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, baada ya mchezo wa kwanza Septemba 26, mwaka jana mabao ya Amissi Tambwe kipindi cha kwanza na Malimi Busungu kipindi cha pili kuwapa ushindi wa 2-0 dhdii ya watani wao hao wa jadi Uwanja wa Taifa.
Pluijm amesema kwamba hana wasiwasi na zaidi anawajenga wachezaji wake kisaikolojia waondokane na presha ya mechi hiyo.
“Kuna presha kubwa kwetu kutokana na ubora wa Simba kwa sasa, Simba ni timu nzuri na imekuwa na maendeleo mazuri kwa kipindi hiki na kikosi chake kimekuwa kikitoa ushindani mkubwa kwa timu nyingine kuliko nilivyokuwa nimeizoea, lakini sisi tutapigana ili tuweze kufanya vizuri,”amesema kocha huyo wa zamani wa Berekum Chelsea ya Ghana.
Pluijm amesema ni pigo kwake kumkosa beki wake tegemeo wa kati, Kevin Yondan anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu, lakini hana wasiwasi, kwani ana wachezaji wengine wa kucheza nafasi hiyo, akiwemo Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliyekuwa majeruhi kwa muda mrefu.
“Yondan hatakuwepo kwa sababu anatumia adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa dhidi ya Coastal Union. Bahati nzuri, Nahodha Cannavaro aliyekuwa nje kwa muda mrefu akisumbuliwa na maumivu amerudi na anaendelea vizuri na mazoezi kwa wiki sasa. Sijui kama atakuwa fiti kucheza, nitajua Ijumaa. Na kwa ujumla hadi kufika Ijumaa nitakuwa nimekwishajua mipango ya mechi imekaaje,” amesema.
Pluijm hakutaka kuuzungumzia sana mchezo, zaidi ya kusema wapizani wake wako vizuri safari hii na anatarajiwa mchezo mgumu Jumamosi.
Yanga SC imeweka kambi kisiwani Pemba kujiandaa na mchezo huo, wakati mahasimu wao wapo mjini Morogoro.
Naye Kocha Mkuu wa Simba Jackson Mayanja amewatoa wasiwasi wanamsimbazi akisema wasikonde kwani mfumo wa Yanga ameshaufahamu hivyo haumsumbui na wasubili kichapo
Chanzo Bin zubeiry.com