Makocha Poulsen, Angels kunguruma leo Dar

Kocha Jan Poulsen wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars)

Na Mwandishi Wetu

MAKOCHA Jan Poulsen wa Tanzania (Taifa Stars) na Gert Josef Angels wa Msumbiji (Mambas) leo, Februari 28 mwaka huu watakuwa na mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia maandalizi ya timu zao.

Taifa Stars na Mambas zinatarajia kukiputa Februari 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni katika mechi ya kwanza ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.

Mkutano huo na waandishi wa habari ambapo makocha hao pia watajibu maswali ya waandishi wa habari utafanyika saa 6 kamili mchana kwenye ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Mambas iliwasili nchini Februari 26 mwaka huu ikiwa na wachezaji 19 na viongozi kumi. Wachezaji walioko kwenye kikosi hicho ni Francisco Muchanga, Clesio Bauque, Almiro Lobo, Manuel Fernandes na Francisco Massinga.

Wengine ni Joao Rafael, Nelson Longomate, Joao Mazive, Zainadine Chavango, Osvaldo Sunde, Luis Vaz, Carlos Chimomole, Joao Aguiar, Edson Sitoe, Jeremias Sitoe, Stelio Ernesto, Elias Pelembe, Eduardo Jumisse na Simao Mate.