Makandarasi daraja la Kigamboni wakagua eneo la ujenzi

Mtaalam Mshauri (katikati mwenye miwani nyeusi) kutoka Kampuni ya Arab Consulting Engineers (ACE) Mhandisi Mohamed Shaeb, akitoa ufafanuzi wa kitaalamu kwa Makandarasi ambao wamepita katika mchakato wa awali wa zabuni ya ujenzi wa Daraja la Kigamboni. Makandarasi hao walikwenda (tarehe 16 Novemba 2011) kukagua eneo litakapojengwa daraja la hilo huko Vijibweni – Kurasini, Jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu

JUMLA ya makandarasi saba waliopita katika mchakato wa awali wa kumpata mkandarasi atakayeshinda zabuni ya ujenzi wa Daraja la Kigamboni wamefanya ziara ya ukaguzi wa eneo la ujenzi.

Mtaalam Mshauri kutoka Kampuni ya Arab Consulting Engineers (ACE), Mhandisi Mohamed Shaeb aliongoza ziara hiyo iliyokuwa na lengo la kuwapa maeleza ya kitaalamu wakandarasi hao juu ya maudhui ya mradi husika na changamoto zake kabla ya ya uwasilishaji makisio kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo.

Awali kabla ya mchakato huu walikwisha jitokeza makandarasi 16 ambapo baada ya mchujo wakashinda hao saba. Shirika la Hifadhi ya Jamii nchini (NSSF) kwa kushirikia na Wizara ya Ujenzi wanaendelea na mchakato wa kuanza ujenzi wa Daraja la Kigamboni ambalo ujenzi wake unatarajiwa kuanza mapema 2012.

Daraja hilo ambalo ni la kisasa zaidi kujengwa hapa nchini ambapo litakuwa na barabara tatu kila upande yaani kuwa na uwezo wa kuruhusu magari sita kupita kwa wakati mmoja. Daraja la Kigamboni linatarajiwa kuwa na urefu wa mita 600 na hapo litakapokamilika litakuwa ni kiungo muhimu kati ya Jiji la Dar es Salaam na Kigamboni na pia litachangia katika jitihada za kupunguza msongamano wa magari hapa jijini.

Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli mnamo mwezi Machi mwaka huu wa 2011 ililiagiza Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuanza ujenzi wa Daraja la Kigamboni mapema iwezekanavyo ili kuhakikisha kuwa usafiri kwa wakazi wa maeneo ya Kigamboni unaimarishwa na hivyo kuondoa kero na adha nyingi wanazozipata kwa sasa.

Agizo hilo lilitolewa wakati wa ziara aliyoifanya Waziri Magufuli alipotembelea eneo la Kurasini Vijibweni, ambako daraja hilo litajengwa. Waziri Magufuli alichukua hatua hiyo kutokana na mazungumzo kuhusu ujenzi wa daraja hili kuwa yamechukua muda mrefu bila ya hatua madhubuti kuonekana.

Ujenzi wa daraja hili utachangiwa kwa asilimia 60 na NSSF wakati ambapo Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi itachangia asilimia 40 zilizobakia. NSSF tayari imekwishatenga kiasi cha Shilingi bilioni 100 hadi sasa kwa ajili ya mradi huu.