Mwenyekiti wa Tume ya Katiba Jaji Warioba kabla ya kumruhusu Mheshimiwa Makamu Wa Rais kutoa maoni yake, alimuelezea namna tume hiyo inavyofanya kazi na namna zoezi zima la kukusanya maoni ya mtu mmoja mmoja lilivyofanyika na kisha akaeleza kuwa, tume hiyo inaendelea na zoezi hilo kwa kukutana na makundi maalum sambamba na mtu mmoja mmoja kufuatia umuhimu wa hoja ambazo tume inakutana nazo na hivyo kuhitaji ufafanuzi.
Katika muktadha huo, Jaji Warioba sambamba na kumpa fursa ya kuchangia maoni yake mengine anayopenda alimtaka Mheshimiwa Makamu wa Rais kujikita zaidi katika suala la Muungano kufuatia yeye kuwa na uzoefu wa kiuongozi katika serikali zote mbili yaani ya Muungano sambamba na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Akizungumzia suala la Muungano Makamu wa Rais Dkt. Bilal ameieleza Tume kuwa yeye ni muumini wa Muungano wa serikali mbili na kwamba haoni sababu ya kubadili mfumo uliopo kwa kuwa umeipatia tija nchi yetu na kuipambanua kama nchi yenye muungano wa mfano katika dunia.
Pia alifafanua kuwa mfumo wa serikali mbili umesaidia kujenga na kudumisha udugu, amani na utulivu baina ya wananchi wa Tanzania Bara na Visiwani kwa kipindi cha miaka 49 sasa.
Tanzania imechangia kitu kikubwa katika historia, kudumisha Muungano wa mfumo wa serikali mbili kati ya nchi mbili, kubwa na ndogo, jambo ambalo kwa nchi nyingine za Afrika wameshindwa. Kumekuwepo na nchi nyingi ambazo ziliungana na kushindwa kudumu kama tulivyo sisi. Hatuna haja ya kujifunza mfumo mpya wakati tulionao umeweza kudumu, « alisema.
Katika ujumbe wa tume uliofika kuchukua maoni ya Mheshimiwa Makamu wa Rais ni pamoja na Waziri Mkuu Mstaafu Salim Ahmed Salim, Profesa wa Sheria Palamagamba Kabudi, Ndugu Simai Said, Ndugu Assa Rashid, Ndugu Sasmir Kyuki, Ndugu Salum Athuman, Ndugu Juma Mzalau na Mratibu wa Tume hiyo Ndugu Ramadhan Kailima.