MAKAMUwa Rais wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal leo ameongoza viongozi mbalimbali wa majeshi na serikali katika mapokezi ya askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) waliouwawa hivi karibuni nchini Sudan mjini Darfur.
Miili ya mashujaa hao iliwasili kwenye uwanja wa ndege wa JWTZ jijini Dar es Salaam (Airwing) majira ya saa kumi na moja kasoro kwa ndege kubwa nyeupe maalumu iliyokodishwa na Umoja wa Mataifa (UN) kwa ajili ya kusafirisha miili hiyo. Baada ya kuwasili ilishushwa kwa vyombo maalumu kabla ya majeneza hayo yaliyokuwa na bendera za UN kuvishwa bendera ya Taifa la Tanzania.
Baadaye miili hiyo ya askari saba, yaani Sajenti Shaibu Othuman, Koplo Osward Chaula, koplo Mohamed Juma, koplo Mohamed Chikilizo, Private Rodney Ndunguru, Private Peter Werema pamoja na Private Photunatus Msofe wote wakiwa askari wa JWTZ ilishushwa kwenye ndege na heshima za kijeshi na kupakiwa kwenye magari maalum.
Kila jeneza lilipakizwa kwenye gari moja la kijeshi na kusafirishwa kwa msafara maalumu kwenda katika hospitali ya Jeshi, Lugalo kuifadhiwa huku ikisubiri taratibu za kuagwa rasmi kijeshi na kusafirishwa maeneo mbalimbali ya mikoa tayari kwa mazishi.
Akizungumza mmoja wa maofisa wa Jeshi la JWTZ kutoka kitengo cha habari na mawasiliano alisema miili hiyo itaifadhiwa katika hospitali ya Jeshi ya Lugalo hadi siku ya Jumatatu ambapo itaagwa rasmi kijeshi majira ya saa mbili asubuhi katika viwanja vya Jeshi la ulinzi jijini Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa mikoani kwao kwa mazishi.
Miongoni mwa viongozi walioshiriki katika mapokezi ya mashujaa hao ni pamoja na Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Makamo Rais wa Pili wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Generali Devis Mwamunyange, Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Inspekta Generali Said Mwema, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulahaman Kinana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Sadic, baadhi ya maofisa na wanajeshi wa JWTZ, pamoja na familia ndugu jamaa na marafiki wa mashujaa hao.
Wanajeshi hao wa Jeshi la Wananchi Tanzania waliuwawa hivi karibuni mjini Darfur, nchini Sudan walipokuwa katika kazi maalumu ya kulinda amani chini ya majeshi ya UN.