Na Ronald Munga
DESEMBA 27, 2012, mkoani Mtwara, lilijiri tukio ombalo, kwa watawala wetu,halikufikirika, halikutegemewa na katu halikutazamiwa. Wananchi wa eneo hilo waliingia barabarani kudai manufaa ya gesi asilia iliyoko Msimbati, Mtwara vijijini. kwa mujibu wa wana Mtwara gesi hiyo ilikuwa inasafirishwa Dar es Salaam bila wao kubainishiwa watakavyonufaika .
Tukio hili lilileta mshtuko wa volteji kubwa (high voltage shock) serikalini. Mkuu wa Mkoa huo Kanali Joseph Simbakalile, alikuwa wa mwanzo kutoa kauli. Waandamaji na waratibu (vyama vya upizani) walipewa lebo ya “wahaini na wapuuzi”. Kwa mujibu wa Kiswahili sanifu, “uhaini ni tendo la kusaliti nchi yako au / kufanya mipango ya kupindua serikali halali iliyopo madarakani”. Na upuuzi ni jambo au tendo lisilo la maana au la kijinga. Naye Waziri wa Nishati na Madini Profesa Dr. Sospeter Muhongo akajitokeza : naye akasema madai ya waandamanaji yanataka kuigawa nchi ( Tanzania ) vipande vipande.
Rasilimali ya nchi ni kwa manufaa ya nchi; hilo linaeleweka kwa kila mtu.Mifano aliyotoa ya katani (mkonge)iliyolimwa Morogoro na Tanga kuwa iliwanufaisha watu wa Mtwara ina upogo. Profesa angejua kuwa mkonge umelimwa Ubena zomozi (Pwani ) na huko kusini kulikuwa na mashanba Mikindani, Kitunda, Mkwaya, Ngurumahamba na Kikwetu. Uwanja wa ndege wa Lindi umezungukwa na shamba hilo la Kikwetu. Kwa nini watu wa Mtwara hawajasema maduhuli ya korosho yatumiwe huko kusini tu? Kauli za viongozi wa serikali hazijagusa kiini au msingi wa madai ya watu wa Mtwara. Watawala wametumia shoka mahali ambapo ukucha ungestahiki.
“Uhaini na upuuzi” wa wana Mtwara umesimama katika miguu ya historia. Kimantiki walichosema ni kuambia serikali yao “mpaka hapa si zaidi” (this farther and no further). Kuwaelewa watu hao hatuna budi kutalii mazingira yaliyowasukuma kufanya walivyofanya. Wanakinyongo kilichorundikana kwa muda mrefu. Hawakuwa bado wamepata mahali pakuegemea na kuyatoa yaliyokuwa yanawakera na kuwasibu.
Walatini wamesema “Veritatis vos liberabit “ ( ukweli utatuweka huru); hivyo kuibua usuli na mazingira ya ukweli kutaepusha kuwaelewa watu hao kwa mtazamo hasi.
Kusini na buti la Wadachi (Wajerumani)
Vita vya MajiMaji (1905 – 1907 ) vya kupinga utawala wa Wajerumani vilianzia Nandete, wilayani Kilwa, mkoani Lindi Mashamba ya pamba yalihujumiwa , na harakati za wazalendo hao zilienea maeneo yote ya kusini ya mto Rufiji na kati ya Bahari ya Hindi na Ziwa Nyasa. Kipindi kifupi tu baada ya upinzani dhahiri kuanza askofu Cassian Spiss ( Mswisi – wananchi walimweka katika kundi la Wajerumani) aliuawa akiwa njiani kuelekea Liwale . Huko Nyangao ( Lindi) misheni ya Wajerumani ilishambuliwa na wapiganaji. Masista wawili wa Kijerumani waliuawa baada ya kudhalilishwa na kuteswa na Waafrika.
Mwaka 1902 huko Kitangali (Newala) Mkulungwa (kiongozi ) Mkoto aliwahamasisha wananchi wasilipe kodi kwa Wadachi. Wale ambao wangelipa wangepata maradhi ya ndui. Ujumbe ulieleweka na wananchi wakaacha kulipa kodi. Wajerumani wakatuma kikosi maalumu cha askari kutoka Lindi kumshughulikia kiongozi huyo. Alikamatwa na kunyongwa hadharani .
Kama tulivyosema upinzani wa Wadachi ulikuwa umeenea sana kusini. Kwenye uwanda wa Makonde wananchi waliwaunga mkono wazalendo wenzao. Mwaka 1907 kikosi cha mamluki kilitumwa toka Lindi ( makao makuu ya watawala katika sehemu hizo ) kwenda kuuzima uasi.
Walipokuwa wanaelekea kwenye lengo wananchi wakapata habari za ujio huo. Walipokuwa katika kijiji cha Mtopwa (Newala) walivamiwa na wananchi. Askari wote waliuliwa wakazikwa pamoja .Mahali hapo pako katikati ya kijiji cha Mtopwa.
Tukio hilo lilikoleza hasira, ghadhabu na ukatili wa Wajerumani.
Askari wengine walipelekwa kumsaka kiongozi wa Mtopwa aliyeitwa Mtumba bin Omari. Alikamatwa na kupelekwa Lindi ambako aliteswa na hatimaye kunyongwa. Kaburi lake liko Lindi mjini sehemu iitwayo Mikumbi.
Hii ni sehemu ya katalogi ya matukio ambayo yalichefua utawala wa Wajerumani kwa eneo la kusini. Hivyo wakati sehemu nyingine za nchi zikisonga mbele kidogo huko kusini waliwekwa kwenye kifukofuko (cocoon0.
Kusini chini ya Waingereza
Baada ya Wajerumani kuangushwa duniani pote katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia (1914 – 1918), Tanganyika, iliyokuwa sehemu ya Dutch East Africa (nchi nyingine katika eneo hili zikiwa Rwanda na Burundi) iliwekwa chini ya utawala wa Waingereza kama wadhamini. Nchi haikuwa koloni kama ilivyokuwa Kenya, Nyasaland( Malawi) na Northern Rhodesia (Zambia). Kwa maeneo ya kusini hali ilikuwa kama Wadachi waliwaambia cha kuwafanyia wenyeji wa kusini. Hakuna kumbukumbu zinazoonyesha kwamba watawala wapya walikuwa na mipango au azma ya kuendeleza eneo hilo katika fani mbali mbali. Yaliyotokea yalilenga kunufaisha watawala.
Baada ya vita Waingereza walikuwa wachovu kiuchumi hali ya huduma za kijamii ziliathirika na vita. Kampuni iliyoitwa Overseas Food Corporation ilianzisha mradi mkubwa wa kulima karanga Urambo (Tabora) Kongwa (Dodoma) na Nachingwea (Lindi). Ili kuhudumia mashamba kwa ufanisi bandari ya Mtwara iliboreshwa. Wakati huo huo wakajenga reli na bomba la mafuta toka bandarini Mtwara hadi Nachingwea. Reli ilikuwa ienddelee hadi Mbamba bay pwani ya ziwa Nyasa.
Mnamo mwezi Oktoba 1961 lilifunguliwa tawi la reli la kilomita takribani 40, toka Chilungula hadi Masasi. Miundombinu na shughuli za kilimo zilitoa ajira na maeneo yaliyopitiwa na miundo msingi hiyo yalifunguka kwa maendeleo
Kwa sababu mbali mbali mradi wa karanga Nachingwea ulifungwa. Mwaka mmoja baada ya Tanganyika kupata Uhuru, sarikali ya Tanganyika huru ikaamini kuwa reli na bomba la mafuta vilikuwa ni miradi isiyo na tija. (white elephant). Reli na bomba vikang’olewa. Athari za hatua hiyo ni bayana .Kusini kulizidi kuzama kimaendeleo, taswira iliyodumu kwa kipindi kirefu. Lakini kwa muda mfupi watawala (Waingereza) walimaizi kwamba eneo la kusini lilikuwa na utajiri mwingi hivyo wakaita “Cinderella Province” Cinderella ikiwa na maana ya ‘mtu au kitu ambacho uzuri au uwezo wake haujatambulikana”.
Jingine walilolifanya Waingereza ni kuangusha magogo na kupasua mbao huko Rondo Mnara (Lindi vijijini). Kampuni iliyoitwa Steel Brothers ilifanya kazi hiyo miaka ya 1950. Wakavuna , wakachuma na kuondoka . Wananchi wakaachiwa visiki vya mipingo , mbambakofi,mivule nk. wakati huo huo walikumbatia umasikini.
Kusini baada ya uhuru.
Miaka michache ya kuelekea uhuru kulianzishwa mradi mkubwa wa maji toka mto Ruvuma ,uliendeshwa na kampuni ya Makonde Water Corporation. Ilipangwa maji yaenezwe sehemu mbalimbali huko kusini. Miaka michache baada ya kuasisiwa kwa vishindo mradi ulikufa. Wananchi hawakuelezwa sababu za mabadiliko hayo.
Madhila,taabu na kero za kukosa maji hazikumilithika .
Katihati ya miaka 1960 kulizuka mgogoro wa kiwanja katika mji mdogo wa Mahuta (wakati huo Newala , sazsa uko katika wilaya ya Tandahimba ). Mfanyabiashara wa Kiasia alipora eneo hilo ili ajenge kituo cha mafuta ya nishati. Wananchi wakachachamaa. Uongozi wa mkoa na wilaya ukaingilia kati. Kwenye mkutano wa hadhara hapo Mahuta , kiongozi wa wananchi alipigwa viboko kwa sababu za “kupinga hatua za maendeleo “ kama walivyoita watawala. Kupinga uonevu kunyanyaswa na kudharauliwa, wananchi waliandika barua ngazi za juu za taifa na kudai , moja , mkuu wa mkoa na yule wa wilaya wahamishwe ,mbili, wapendekeze majina ambayo yatatoa mkuu wa mkoa na yule wa wilaya ; na tatu kama maombi hayo hayatakubalika watajitenga na kujiunga na Msumbiji ili wawe pamoja na FRELIMO kutafuta ukombozi. Yaliyofuata ni historia.
Miaka mitatu baada ya uhuru wa Tanganyika , wana Msumbiji kupitia FRELIMO walianzisha vita vya ukombozi. Kutokana na mazingira ya kijiografia ( kati ya nchi mbili ) eneo lote la kusini likawa “no go area” – hapakuwa na shughuli zozote za maana za kimaendeleo zilizokuwa zikifanyika . FRELIMO wakafanikiwa kukunja jamvi ukoloni mwaka 1975. Ni dhahiri kwa miaka kumi wengine walikuwa wamesonga mbele hapa nchini . Mategemeo na matumaini ya wengi huko kusini ni kuwa serikali ingekuwa na programu maalum “kufidia muda uliopotea”. Wakati wa Vita kuu ya Pili vya dunia Yugoslavia ilipambana na majeshi ya Adolf Hitler .
Marshal Josef Tito akawaambia wapiganaji wale “ The wounded should not be left behind “ ( majeruhi wasiachwe nyuma). Kimaendeleo kusini ilijeruhiwa na kuachwa nyuma.
Barabara ya Dar es salaam – Lindi ni “mkunga” wa matatizo ya kusini. Ahadi za serikali kuijenga zimechukua kipindi kirefu kutekelezwa. Miaka ya 1970 – 80 kampuni moja ya Kitanzania na taasisi moja ya serikali waliteuliwa kujenga barabara hiyo. Wakajenga makambi Nangurukuru (Kilwa).Hakuna ushahidi wa kazi iliyofanywa – tatizo la barabara likawa “ kichwa cha mwenda wazimu”. Mwaka 1977 wananchi wa kusini, wakiungwa mkono na wa maeneo mengine, waliasisi mchango maalum kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo. Mwitikio wa wito huo ulikuwa chanya. Ofisini ya Waziri Mkuu ikasitisha zoezi hilo kwa ahadi kuwa serikali igejenga mradi huo. Imechukua miongo kadhaa kukamilika kazi hiyo.
Miaka ya 1960 – 70 wananchi wa kusini walihamasishwa kulima korosho kwa ajili ya biashara. Matokeo yalikuwa ya kutia moyo. Mapori yalipisha mashamba ya mikorosho. Zao likachangia umasikini. – Pembejeo bei juu na soko likawa halina uhakika .
Kuna viwanda vya kubangua korosho Masasi , Newala Lindi na Mtwara lakini hakuna msimamo maalum wa Bodi ya Korosho na wanasiasa wa kuuza nje zao lililoongezewa thamani. Bado wanakumbatia fikra hafidhina zilizopitwa na wakati wa kuuza nje ya nchi korosho ambazo hazijabanguliwa.
Alama za nyakati na Baba Kundambanda.
Walioandamana huko Mtwara walikuwa wanadai haki waliyoikosa kwa miaka mingi. Kilichoonekana kama uhaini na upuuzi ni mbegu ya tunda ya mti wa ahadi zisizotekelezwa. Kwa wachunguzi wa mambo dalili zilianza kujitokeza mapema mwaka 2012. Msanii mmoja wa huko kusini alitoa nyimbo zinazochambua uadilifu wa polisi, EPA, sera nzuri za Mwalimu Nyerere na wanasiasa wa maeneo ya kusini wanavyo waona wananchi kuwa ni mazuzu . Nyimba za msanii huyo, Baba kundambanda, anaimba kwa lafudhi ya Kimakonde, moja ya lugha za kusini na pia huingiza maneno ya lugha hiyo kwa mfano anasema viongozi / wanasiasa huwaambia wananchi kuwa koromeo lilkipanda na kushuka maelezo yake ni kuwa shetani anatwanga mtama ( Nandenga atwangi ntama pang’ulo ) . lakini wananchi kwa kuwa si “ mavelu “ (mazuzu, wajinga ) hujibu “ kulambila” ( huo ni uongo ). Wimbo huu una umarufu mkubwa na jijini Dar es salaam huchezwa na baadhi ya vituo vya redio.
Nani hamwelewi nani ?
Maelezo ya Waziri Muhongo kupitia vyombo vya habari hayajibu hoja ya msingi ya madai anayoyapuuza. Yakichambuliwa kwa uyakinifu na mantiki ni kama kuhamisha magoli ili mabao yasiingie kimiani. Takwimu anazotoa zipo kando ya madai ya wananchi – tutanufaikaje? Kama ni zile ahadi za “yatakayofanywa baadaye” ndiyo yanayewapa watu hao nguvu ya kutamka “ mpaka hapa si zaidi” kwa sababu wamepitia mengi ya ahadi zisizotelekezwa. Msamiati wa vitisho hautapunguza ari ya wananchi kutoa maoni na madai.
Makala inahitimishwa kwa aina mbili za semi ambazo ni maarufu sana katika eneo hilo la nchi. Watu wakipeana mikono kisha mkono mmoja ukaacha viganja na kuelekeza kwapani mtu huyo ana lake jambo. Anayedai kuendelezwa hawi haini au mpuuzi – mkono unaelekea kwapani. Mahusiano ya ukwe ni ya heshima kubwa sana katika jamii za Watanzania: – usemi wa pili -kijana wa kiume alikuwa anavuka kijito kwa miguu na mama mkwe: mama mkwe alikuda ili nguo zake zisirowe na kwa kufanya hivyo mapaja yake yakaonekana. Katika usemi huu badala ya kijana weka neno wana Mtwara na mama mkwe weka “viongozi wa serikali/ wanasiasa”. Nani kaonesha kisichostahiki?
Chanzo: Zitto Kabwe Blog