Majeshi ya Kiislamu yateka mji nchini Mali

Majeshi ya Kiislamu nchini Mali

MAJESHI ya Kiislam yanayohusishwa na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda yameteka mji muhimu wa Gao, Kaskazini mwa Mali, baada ya siku moja ya mapigano makali dhidi ya mahasimu wao wa kikundi cha Tuareg.

Msemaji wa Tuareg amesema kiongozi wao wa kisiasa amejeruhiwa katika mapigano hayo siku ya Jumanne, na amepelekwa nchi jirani kwa matibabu. Wakazi katika mji huo wamesema kuwa waasi wameteka majengo katika mji huo na kupeperusha bendera zenye rangi nyeusi.

Baada ya wiki kadhaa ya makubaliano ya mashaka katika mji wa Gao, na baada ya kushindwa kuungana, wapiganaji wa Tuareg wameripotiwa kuondolewa katika mji huo muhimu na waasi hao wanaotaka kuweka sheria za kiislamu, za sharia.
Mapigano makali yalizuka jana asubuhi kati ya makundi hayo hasimu na kusababisha watu kujifungia majumbani mwao siku nzima.

Daktari mmoja katika hospitali mjini Gao, amesema kupitia laini ya simu, kwamba watu wengi waliojeruhiwa walikuwa wamejihami, lakini pia raia walijeruhiwa katika mapigano hayo. Daktari huyo amesema kwamba raia wawili walifariki dunia kutokana na majeraha waliyopata.

Miili ya watu pia iliripotiwa kuonekana katika miji mingine ya nchi ya Mali.
Mji wa Gao uko kwenye ufuko wa mto na umezungukwa na eneo kubwa lililo wazi. Kwa upande wa kaskazini ni Jangwa la Sahara.

Lakini kwa miaka mingi mji huo ulikuwa eneo muhimu la biashara ya matunda, mboga na mchele. Bado mji wa Gao ni muhimu kwa sababu ndio njia muhimu ya kuelekea Mali ya kusini na pia ya kwenda nchi jirani za Niger na Nigeria.

Ndio sababu haishangazi kwamba mji huo ulitajwa kama makao makuu ya muda ya jimbo lililojitangazia uhuru wake la Azawad, wakati waasi wa Tuareg walipotwaa eneo la kaskazini mwa Mali, mapema mwaka huu.

BBC