Majengo ya Polisi, Usalama Yashambuliwa Cairo

Mmoja wa askari waliojeruhiwa (kulia) katika mlipuko akisaidiwa baada ya kupata huduma ya kwanza.

Mmoja wa askari waliojeruhiwa (kulia) katika mlipuko akisaidiwa baada ya kupata huduma ya kwanza.


ZAIDI ya watu wanne wameuwawa na wengi kujeruhiwa kufuatia mashambulio matatu ya mabomu karibu na vituo vya polisi katika Mji Mkuu wa Misri Cairo. Shambulio la kwanza lilitokea eneo la uwanja yanakoegeshwa magari ambalo ni Makao Makuu ya Polisi mjini Cairo, katika mlipuko huo mtu mmoja anadaiwa kujilipua akiwa ndani ya gari eneo hilo.

Kwa mujibu wa duru za idara za usalama watu wasiopungua wanne wameuwawa na wengine 70 kujeruhiwa katika mlipuko huo. Mlipuko huo pia umebomoa ukuta wa jengo la usalama la kituo cha polisi na idara ya usalama wa taifa. Jengo la makumbusho ya sanaa ya kiislam nalo pia limebomoka kwa mlipuko huo.

Hata hivyo askari polisi watatu ni miongoni mwa wahanga wa mashambulio hayo. Taarifa zaidi zinasema umeadhiri baadhi ya majengo jirani na eneo hilo kama maduka ambayo yamepasuka vioo, vigae kuanguka na kutapakaa kwa vyuma na mbao mia kadhaa kutoka eneo la shambulio hilo.

Shambulio la pili limetokea katika kituo cha polisi cha Talbeya, katika eneo la Ihram huko Gizah karibu na Cairo, muda mfupi baada ya shambulio la bomu dhidi ya makao makuu ya polisi. Hata hivyo taarifa za madhara ya mlipuko huo bado hazijawekwa hadharani. Mlipuko wa tatu umetokea mbele ya ofisi ya polisi magharibi mwa Mji Mkuu Cairo njia panda inayoelekea katika eneo la Ihram la Gizah.

Taarifa za awali zinasema mtu mmoja ameuwawa katika mlipuko huo japokuwa haijathibitishwa na vyombo vya ulinzi na usalama. Kikosi cha Polisi wa kuzuia fujo kimewatawanya mamia ya wafuasi wa utawala mpya waliokuwa wakiwakaripia wafuasi wa rais aliyepinduliwa Mohammed Mursi kuwa nyuma ya mashambulio hayo.

Wakati huo huo kundi la itikadi kali Ansar-Beit al-Maqdes, lenye vituo vyake katika eneo la Sinai limedai kuhusika na mashambulio hayo. Mashambulio haya yanatokea ndani ya mkesha wa kuadhimisha miaka mitatu tangu mapinduzi yaliyomng’oa madarakani kiongozi Hosni Mubarak.

Maandalizi ya sherehe hizo yanafanyika huku hali ikionekana kuwa tete na polisi na wanajeshi kutawanywa katika kila pembe ya Misri na hasa katika eneo la kati ya Mji Mkuu Cairo, unakokutikana uwanja mashuhuri wa Tahrir.
-DW