Na mwandishi wetu
Musoma
WATU wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamewavamia wachimbaji wadogo wa dhahabu katika machimbo ya Magunga Buhemba Wilaya ya Musoma Vijijini na kuua watu watano na kujeruhi wengine watano na kuchukua pesa,dhahabu pamoja na mali mbalimbali ambazo thamani zake bado hazijafahamika.
Wakiongea na MTANZANIA katika Hospitali ya Mkoa wa Mara majeruhi wa tukio hilo lililotokea siku ya jana majira ya saa tisa alasiri walisema kuwa wakiwa katika maeneo ya manunuzi ya dhahabu watu sita baadhi yao wakiwa wamejifunika vitambaa usoni waliwavamia na kuwataka kutoa kila kitu walichokuwa nacho huku wakiwa wanapiga risasi hewani.
Walisema watu hao waliokuwa na bunduki mbili pamoja na mapanga mara baada ya kuwavamia walianza kupiga risasi ovyo na kuwakata mapanga baadhi ya wanunuzi na kuanza kukusanya fedha,simu pamoja na dhahabu na kutoa kauli za vitisho kwa yule atakayeleta ubishi atapoteza maisha.
Mmoja wa majeruhi hao aliyejitambulisha kwa jina la Mboyi Keya mkazi wa kijiji cha Masumbwe Mkoani Geita alisema kuwa yeye akiwa katika moja ya vibanda vya manunuzi alishukia anakatwa panga la bega na kunyang’anywa kiasi cha shilingi milioni moja na laki nane alizokuwa na zo pamoja na dhahabu zenye thamani ya shilingi laki tano pamoja na simu ya nokia huku wakiendelea kufanya matukio kama hayo kwa watu wengine.
Majeruhi mwingine aliyelazwa katika hospitali hiyo ya Mkoa wa Mara aliyejitambulisha kwa jina la Mashine Muli alionyesha kusitikitishwa na askari wa eneo hilo baada ya kushindwa kutoa msaada wowote licha ya tukio hilo kudumu kwa takribani saa moja huku wananchi wakipigwa risasi na kukatwa mapanga na majambazi hao.
“Askari wale wa Buhemba ni bora wahamishwe haiwezekani risasi zinapigwa kwa muda mrefu na wao wanashindwa kufika eneo la tukio kutoa msaada saa wanalinda vipi wananchi na mali zao,wapo maaskari majasiri ndio wanaotakiwa kupangwa maeneo kama haya ambayo huwa kutokea matukio ya kuvamiwa na kupoteza maisha ya Wananchi”,alisema Mashine.
Alipo watembelea majeruhi hao pamoja na ndugu wa marehemu waliokuwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mara John Tuppa amabaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama alisema Serikali pamoja na jeshi la Polisi litahakikisha linaendesha msako mkali kwa wale wote waliohusika na tukio hilo na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
“Serikali ya Mkoa imesikitishwa sana na tukio hili na tuko pamoja na ndugu pamoja na jamaa wa watu wote waliokutana na hadha ya tukio na kwa upande wa majeruhi kwa kushirikiana na Mganga mkuu mkuu pamoja na madaktari wote inatolewa huduma yenye kukidhi kqwa majeruhi hili warudi katika hali ya uzima na mkoa unatoa pole kwa wale wote waliopoteza ndugu pamoja jamaa zao,”alisema Tuppa.
Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo docta Joseph Nyamagwira alisema hali za majeruhi zinaendelea vizuri na wanaendelea kupata matibabu kutoka kwa waganga na wauguzi kwa ukaribu zaidi baada ya kufanikiwa kuwashona kwa ufanisi wale majeruhi waliokuwa wamepigwa risasi na kukatwa mapanga.
Watu waliofariki katika tukio hilo ni Charles Jaoko wa Buhemba,China Magige wa Tarime,Joseph Chacha Nchago wa Tarime,Juma Marwa wa na Gungwa Gungwa wa wakazi wa Mirwa Wilaya ya Musoma Vijijini.
Majeruhi waliojeruhiwa katika tukio hilo ambao wamelazwa katika hospitali ya Mkoa wa Mara ni Mashine Muli wa Buhemba,Nganyira Nyanda wa Magunga,Japhet Henry wa Buhemba,Mboyi Keya wa Masumbwe Geita na Zakaria Zakayo wa Geita.