WATU wanaodhaniwa kuwa majambazi wamekivamia kituo cha Polisi Stakishari kilichopo eneo la Ukonga jijini Dar es Salaam majira ya saa tatu usiku na kuuwa askari pamoja na kupora silaha. Kwa mujibu wa taarifa za awali ambazo hazijathibitishwa na Jeshi la Polisi inasemekana watu hao wamevunja chumba cha kuhifadhia silaha na kuiba silaha kadhaa nyingi aina ya SMG zilizokuwa zimehifadhiwa kituoni hapo.
Inasemekana askari 4 wameuwawa na raia wawili pamoja na jambazi mmoja aliyepigwa na risasi ya jambazi mwenzie wakiwa katika uvamizi huo. Inasemakana majambazi hayo yamekimbia na kuacha pikipiki tatu (3) eneo la tukio. Inasemekana waliingia kituoni hapo kwa staili kana kwamba walikuwa wamembeba mtu aliyepata ajali na waliitaji msaada wa polisi kabla ya kugeuka gafla na kuanza kuwashambulia askari kituoni hapo. Askari wawili wamenusurika kituoni hapo, ambapo mmoja alijificha chini ya kaunta baada ya kuvamiwa. Majirani na eneo hilo walisema walisikia milio ya risasi ikisikika kabla ya kelele za ving’ora vya magari ya Polisi kusikika baadaye eneo hilo la stakishari.
Taarifa zinaendelea kueleza kuwa jambazi aliyeuwawa inadaiwa ni dereva wa bodaboda wa kituo cha Njia Panda anayefahamika kwa jina la Madevu. Mtandao huu bado unafatilia taarifa zaidi juu ya tukio hilo na tutawajuza kadri zitakavyo tufikia.