‘Majambazi’ watatu wauwawa, wakutwa na bunduki, risasi 25

Na Janeth Mushi, Arusha

WATU watatu wanaodhaniwa kuwa majambazi wameuwawa na Polisi mkoani Arusha walipokuwa wakirushiana risasi na askari hao na tayari mtu mmoja anashikiliwa na Jeshi la Polisi kuhusishwa na tukio hilo.

Akizungumza na wanahabari jana Septemba 18, 2011 mjini hapa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Leonard Paul alisema tukio hilo lilitokea Septemba 17 mwaka huu usiku eneo la Losiningori wilayani Monduli.

Alisema kuwa walipokea taarifa kuwa kuna majambazi ambao walikuwa wamepanga mawe barabarani kwa lengo la kuteka magariyaliyokuwa yakisafirisha abiria.

Aidha alibainisha mara baada ya taarifa hizo askari walifuatilia tukio, walipofika eneo hilo majambazi walishtuka na kuanza kurusha risasi kwa majibizano hivyo askari kufanikiwa kuwapiga risasi watatu kati yao ambapo walifariki dunia papo hapo.

Kaimu huyo alisema majina ya majambazi wawili hayajaweza kufahamika mara moja na mmoja kati ya waliofariki dunia ametambulika kwa jina Joseph Marwa. Hata hivyo amesema majambazi wengine wawili walikimbia baada ya kuzidiwa.

Ameongeza kuwa katika tukio hilo wamefanikiwa kukamata silaha moja aina ya SMG, ambayo majambazi walikuwa wanaitumia huku ikiwa na risasi 25 ndani yake, ambapo upelelezi wa tukio hilo unaendelea ili watuhumiwa waliokimbia waweze kukamatwa na kufikishwa mahakamani.