MAJAJI 12 ambao ni wakuu wa Kanda za Mahakama Kuu ya Tanzania, jana waliingia katika orodha ya vigogo kufika Samunge, Loliondo kupata tiba ya magonjwa sugu kwa Mchungaji Ambilikile Mwasapila. Habari zilizopatikana jana zimeeleza kwamba majaji hao walifika Samunge wakitokea Arusha ambako walikuwa na semina ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Idara ya Mahakama katika kushughulikia kesi za ukiukwaji wa haki za binadamu.
Majaji hao, walifika kijiji hapo majira ya saa saba mchana wakiwa wanaongozwa na maofisa wa Serikali wilayani Ngorongoro. Walifika kwa magari ya kukodi aina ya Land Cruiser ambayo ni maalumu kwa ajili ya kubeba watalii.
Tofauti na viongozi wengine, majaji hao, walikwenda kwa njia ya barabara wakitokea Arusha mjini na mara baada ya kufika nyumbani kwa mchungaji Mwasapila, waliandaliwa eneo maalumu na kila mmoja kupata kikombe cha dawa.
Raia 500 wa kigeni wapata tiba Mamia ya raia wa kigeni kutoka nchi mbalimbali duniani pia wamekuwa wakimiminika katika Kijiji cha Samunge kupata tiba ya magonjwa ambayo ni shinikizo la damu, Ukimwi, kisukari, kifafa na ugonjwa wa pumu.
Uchunguzi uliofanywa na timu ya waandishi wa Mwananchi iliyoweka kambi Samunge kwa takriban wiki mbili sasa, umebaini kuwa hadi juzi jioni, raia zaidi ya 500 wa kigeni walikuwa wamefika kwa Babu kupata kikombe cha dawa.
Takwimu zinazokusanywa katika eneo la utoaji wa dawa zinaonyesha kuwa wageni kutoka nchi jirani ya Kenya ndiyo wanaoongoza kwa kunywa dawa hiyo. Hadi sasa, zaidi ya Wakenya 300 wameripotiwa kupata kikombe cha babu.
Nchi nyingine ambazo raia wake wameishafika kijijini Samunge na kunywa dawa hiyo ni Marekani, Finland, Uholanzi, Sir Lanka, Jumuiya ya Falme za Kiarabu (UAE), Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Uganda, Rwanda, Burundi na Comoro.
Kutokana na wingi wa wageni hao, tayari Idara ya Uhamiaji, imepeleka ofisa wake ambaye ameweka kambi Samunge kupitia nyaraka mbalimbali za wageni hao.
Jana, gazeti hili lilishuhudia raia wawili wa Uholanzi na wawili kutoka Falme ya Kiarabu huko Dubai, ambao ni wageni wa kampuni ya Ortelo Business Corporation (OBC), inayoendesha shughuli za uwindaji katika pori tengefu la Loliondo wakipata dawa.
Kauli za wageni Wakizungumza na Mwananchi raia wa Uholanzi, Marise Koch na mumewe, George Koch, walisema wamefika Samunge kunywa dawa hiyo baada ya kusikia sifa yake.“Ni dawa nzuri, tumekunywa safi sana tunajisikia vizuri,” alisema Marise baada ya kupata kikombe.
Raia hao wa Uholanzi ambao ni wamiliki wa hoteli ya kitalii ya Rhotia Valley Tented Lodge iliyopo Karatu, pia waliwapeleka kunywa dawa wafanyakazi wao zaidi ya 20.
“Tumekuja na wafanyakazi wetu, wamekunywa dawa, ninaamini kila mmoja amefurahi sana maana walikuwa na shauku kubwa . Tutawaleta wengine” alisema George Koch.
Raia wa Oman ambao hawakuwa tayari kutaja majina yao walisema walifika Tanzania kutembelea jamaa zao ndipo walipopata taarifa za kuwepo kwa dawa hiyo na kuamua kwenda kupata kikombe.
“Mimi naumwa, nina presha (shinikizo la damu) na kisukari na magonjwa haya yananisumbua sana, hivyo nimekunywa dawa ili nipone,”alisema mmoja wa wageni hao alipozungumza na Mwananchi.
Raia mwingine wa Kenya aliyejitambulisha kwa jina la Lucy Njuguna aliliambia Mwananchi kuwa alipata taarifa za kuwepo kwa dawa hiyo kupitia vyombo vya habari vya Kenya.
Alipoulizwa kuwepo kwa taarifa kwamba Serikali ya Kenya imewazuia raia wake kunywa dawa hiyo, Njuguna alisema: “Hayo ni maneno tu, haiwezekani eti watu wote hawa ni wajinga kupanga foleni kwa siku sita wakisubiri kunywa dawa isiyoponya.”Alisema anaamini kwamba dawa hiyo itamponya ugonjwa wa kisukari uliokuwa ukimsubua.
Kauli ya Polisi Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ngorongoro (OCD), Listone Mponjoli aliliambia Mwananchi kuwa polisi wamekuwa wakihakikisha kuwa wageni wote wanaoingia nchini kwa ajili ya kunywa dawa wanazingatia sheria na taratibu za uhamiaji.
Katika kusimamia suala hilo, suala la wageni wanaoingia Samunge, Mponjoli alisema wamekuwa wakifanya doria kwenye msururu wa magari na kukagua nyaraka mbalimbali kabla ya wageni husika kufika kwa Mchungaji Mwasapile kunywa dawa ambapo pia hukaguliwa na ofisa uhamiaji aliyepo katika eneo hilo.
Katika moja ya doria hizo, Mwananchi lilishuhudia baadhi ya magari kutoka nchi jirani ya Kenya yakiondolewa kwenye foleni na kuwekwa pembeni kutokana na kutokuwa na nyaraka zinazokidhi matakwa ya taratibu za uvukaji mipaka.
Eneo la Loliondo linapakana na Kenya, ambapo kumekuwa na mwingiliano wa raia wa nchi hiyo na Tanzania.
Serikali yajipatia mradi
Wakati huo huo, mgogoro mkubwa umeibuka jana mjini Arusha kutoka na serikali kuzuia magari ya utalii ya kwenda Samunge hadi hapo wamiliki wake watakapokuwa wameyakatia vibali kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi kavu (Sumatra).
Wakizungumza na Mwananchi kwa simu kutoka Arusha, baadhi madereva wa magari ya utalii na binafsi walisema wanapinga kulipia tena Sumatra kwa safari za Loliondo pekee kwani tayari wamekwishalipia ada za kazi nyingine wanazofanya.
“Serikali sasa inataka kujinufaisha kupita kiasi na Babu wa Loliondo, wanalazimisha kulipia Sumatra eti kupata leseni ya muda na wakati huo wanatoza kodi ya kuingia Samunge, huu ni unyanyasaji,” alisema dereva, John Mallya.
Mallya alisema wanalazimishwa kulipia Sumatra kiasi cha Sh9,000 kwa mwezi au Sh7,000 kwa wiki na gharama ya kukaguliwa gari Sh1,000.
Magari zaidi ya 100 yaliyokuwa yasafiri kwenda Samunge jana kupeleka wagonjwa yalikuwa yamezuiwa katika eneo la Kilombero mjini Arusha yakitakiwa kwanza kulipa ada hizo Sumatra kabla ya kuendelea na safari.
Ndesamburo apeleka helikopta nyingine Loliondo
Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo amesema ameagiza helikopta nyingine kwa ajili ya kutoa huduma ya dharura kwa wagonjwa wanaokwenda Samunge.
Hata hivyo, anasema wakati anafikiria suala hilo, bado anaumizwa na uamuzi wa Serikali wa kuizuia helikopta yake ya kwanza iliyokuwa ikitoa huduma kwa wagonjwa hao. Helikopta hiyo inayomilikiwa na kampuni yake ya Keys Aviation, ilizuiliwa kuruka kwenda Loliondo kwa mwezi mmoja kuanzia Machi 25 hadi Aprili 26 na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).
Ndesamburo aliliambia Mwananchi jana mjini Moshi kuwa ameamua kuagiza helikopta ya pili kutokana na wingi wa maombi ya kuchukua wagonjwa wanaohitaji usafiri maalumu na wa haraka kwenda Loliondo kupata tiba.
“Nina order (maombi) nyingi na booking za kupeleka wagonjwa kule zimejaa hadi mwezi wa sita lakini Serikali imenizuia na hainiambii sababu ni nini hasa… “Wapo watu waliozidiwa sana ambao wanahitaji kuchukuliwa haraka na kurejeshwa hospitali, isipofanyika hivyo watakufa kabla hata ya kufika kwa babu kunywa kikombe na kuna maiti ziko kule za kurejesha.”
Ombi la wagonjwa
Wagonjwa wanaokwenda katika Kijiji cha Samunge, Loliondo wameiomba Serikali kuongeza idadi ya watu wanaotakiwa kwenda huko kwa siku kutoka kutoka 200 hadi hadi 1,000.
Wakizungumza na gazeti hili jana walisema idadi ya wagonjwa 200 wanaoruhusiwa kupita kwenye vizuizi zilivyowekwa kwa siku, ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya watu wanaotaka kwenda huko.
Baada ya magari kukwama njiani yakielekea Loliondo, Serikali iliamua kuweka vizuizi kikiwamo cha Bunda ambako magari husimamishwa na kukaguliwa kisha kuruhusiwa kulingana na ratiba.
Mmoja wa madereva wanaosafirisha wagonjwa kwenda huko kutokea mkoani Kagera, Haji Mnyonge aliitaka Serikali inapaswa kuangalia upya maazimio yake ya kupitisha watu 200 pekee idadi aliyosema ni sawa na magari 16 tu kwa siku.