TAKRIBANI familia 125 za wapangaji ambao walikuwa wanaishi kwenye hifadhi ya muda ya Shule ya Sekodari Benjamin Dar es Salaam sasa wanaishi chini ya miti nje ya lango la kuingilia shule hiyo, eneo la barabara ya Uhuru.
Hali hii imekuja baada ya Serikali kuwaondoa katika kambi hiyo pale shule zilipofunguliwa na kusema haina namna ya kuwasaidia wapangaji hao hivyo watafute sehemu ya kukaa na kuanza maisha yao.
Wapangaji hao walikuwa wamepanga maeneo ya mabondeni hasa Bonde la Msimbazi ambapo mwishoni mwa mwaka 2011, yalikubwa na mafuriko hivyo kuathiri maisha ya wapangaji hao.
Wakizungumza na dev.kisakuzi.com jana Dar es Salaam kupitia kwa kiongozi wao, Mussa Magambo wamesema wao hawana uwezo wa kupanga nyumba nyingine kwa sasa kutokana na wengi kupoteza, fedha na shughuli walizokuwa wakizifanya.
“Sisi ni baadhi ya wapangaji ambao tumeshindwa kupata fedha za haraka na kuweza kupanga na kuendelea na maisha yetu kama kawaida kwa sasa…tumejihifadhi hapa wakati tunaangalia namna ya kujikwamua,” alisema Magambo.
Wapangaji hao ambao baadhi wana watoto wadogo na wazee wanalala nje ya eneo hilo na kuishi kwa kuomba omba wakati wakijipanga kuondoka katika hali hiyo iliyochangiwa na mafuriko ya mvua kubwa zilizonyesha mwaka jana.
Hata hivyo wameiomba Serikali kuwa badala ya kuendelea kuwasaidia msaada ya dawa, vyakula, mavazi na vitu vingine ingejipanga angalau kuwasaidia fedha za kupanga kwa miezi mitatu ama kulingana na uwezo wake ili wajipange na kuendelea na shughuli zao.