Na Mwandishi Wetu, Arusha
JAJI wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Aloyce Mujulizi anayesikiliza
kesi ya kupinga matokeo inayomkabili Mbunge wa Arusha Mjini Godbless
Lema (CHADEMA) ameonya vikali vyama vya siasa, watendaji wa vyama
hivyo, vyombo vya habari pamoja na waandishi wa habari nchini kuingilia masuala yanayoendelea mahakamani.
“Vyama vya siasa, watendaji wa vyama vya siasa, waandishi wa habari
pamona na vyombo vya habari mara moja wanatakiwa kuacha kufanya utani na masuala yanayoendelea mahakamani kwani siyo ya maigizo, mambo ya mahakamani yaheshimiwe kwa umakini kwani ni wakati muafaka kwa vyombo vya habari kuchukua tahadhari kwa kuandika ukweli bila mbwembwe wala matambo habari za mahakamani,” alisema Mujulizi.
Jaji huyo alitoa taadhari hiyo jana mahakamani wakati kesi
hiyo ilipotajwa, ambapo Oktoba 28 mwaka huu, Mahakama hiyo ilitoa amri ya kufika mahakamani Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye na mhariri wa Gazeti la Nipashe kuthibitisha kauli zilizotolewa na Katibu huyo katika gazeti hilo.
Jaji huyo alimtaka Katibu huyo na mhariri baada ya Wakili anayemtetea Lema, Method Kimomogolo, kudai kuwa walikiuka taratibu na sheria za mahakama kwa kuingilia uhuru wa mahakama, pele Nape alipozungumzia suala ambalo lipo mahakamani.
Mbele ya hakimu huyo, Mhariri wa Nipashe, Flora Wingia ambaye
alikuwa pamoja na wakili anayemtetea, Michael Ngalo ambapo Katibu huyo hakuweza kufika mahakamani kwa mujibu wa wakili aliyemuwakilisha Jerome Msemwa.
Wakili anayewakilisha upande wa wadai ukiongozwa na Alute Mughwai na Modest Akida, waliieleza mahakama hiyo kuwa mara ya mwisho shauri hilo kutajwa mahakamani hapo, Nape na Flora walitakiwa kufika mahakamani hapo kwa ajili ya kutoa ufafanuzi kutokana na habari iliyoandikwa katika gazeti hilo toleo Namba 57162 la Oktoba 9 mwaka huu. Msemwa aliieleza mahakama hiyo Nape amepokea wito wa kuitwa
mahakamani ila alishindwa kufika baada ya kuugua ghafla.
“Mheshimiwa Jaji wakati tunapanga safari ya kuja Arusha kuitikia wito
wa mahakama tayari, Nape alishakata tiketi ya ndege kuja huku ila
alipata maradhi ghafla yaliyomsababishia kulazwa katika hospitali ya
Mission Mikocheni ya Jijini Dar es Salaam,” alisema.
Wakili huyo litoa tiketi iliyokuwa na namba 432 ya shirika la ndege
la Precision iliyokuwa iondoke Dar es Salaam juzi saa 12 jioni na
kufika Arusha saa 1;30 jioni pamoja na hati iliyotoka hospitali hiyo aliyolazwa kama vielelezo na kukabidhi nakala zake kwa mahakama, ili zibaki kwenye jalada la Mahakama.
Jaji Mujulizi alimtaka Mhariri huyo kusoma nakala hiyo iliyokuwa
inazungumziwa mahakamani hapo. Akijitetea mahakamani hapo Wingia alidai kuwa baada ya kupata taarifa za kutakiwa kufika mahakamani jana amegundua upungufu katika uandishi wa lugha ambapo kuna maneno mwandishi aliyeandika habari hiyo aliyaweka ambayo Nape hakuyasema.
Baada ya mhariri huyo kujitetetea hivyo Jaji alimweleza wakili
anayemtetea Wingia kuwa kutokana na yeye mwenyewe kugundua kuwa kuna mabo ndivyo sivyo, hatua anayoingia ni hatua ambayo mahakama inamtaka kula kiapo ili atoe ushahidi.
Wingia aliieleza mahakama hiyo kuwa habari hiyo hakuihariri yeye bali
ilihaririwa na Msanifu gazeti aliyemtaja kwa jina la Owde
Kyambile, ambapo Nape alinukuliwa akisema kuwa “Tunatoka Igunga kupiga kambi Arusha ila kesi ya uchaguzi tunashinda na tunakwenda kulichukua jimbo letu” ila hakusema wana Uhakika wa kushinda kesi hiyo kama ilivyokuwa imeandikwa katika gazeti hilo.
Alisema kuwa baada ya kupata taarifa za kuitwa mahakamani alizungumza na Katibu Huyo wa Itikadi na Uenezi, ambaye alimweleza kuwa maneno anayodaiwa kusema kuwa CCM wana uhakika wa kushinda kesi iliyopo mahakamani hakuyasema.
“Nipo tayari kurekebisha kwa sababu hayo ni mapungufu kwa kuwa
hatukumtendea haki Nape, tuko tayari kuchapisha toleo na kuomba radhi Mahakama kwa kuingilia uhuru wake, Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema na Nape kwa pamoja tutawaomba radhi,” alisema Flora.
Kwa upande wake wakili anayemuwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali Anjela Chacha, alimhoji Mhariri huyo iwapo tangu toleo hilo kuchapisha habari hiyo, Nape amewahi kufika ofisini na kulalamika ambapo alijibu kuwa hakuwahi kufika katika ofisi zao na kulalamika.
“Nimejiridhisha kutokana na ushahidi uliotolewa na Mhariri huyo wa
Nipashe la Jumapili kwamba maneno yaliyochapishwa yanayodaiwa
kuzungumzwa na Nape ni maneno yaliyotumika kwa uzembe na mwandishi aliyeandika habari hiyo au kwa tamaa ya kutaka kutia pilipili kwenye habari. “Mahakama inakubaliana na kuomba radhi na kuamrisha Mhariri achukue hatua ya habari hiyo na kuomba radhi kwa kuchapisha ukurasa wa kwanza,” alisema na kuongeza Jaji huyo
Awali Kimomogolo aliieleza mahakama hiyo kuwa kutokana na kauli ya katibu huyo Lema,viongozi wa Chadema na wafuasi wake wameingiwa wasiwasi juu ya uendeshwaji wa kesi hiyo na kumtaka Jaji huyo kujiengua katika shauri hilo.
Kimomogolo alisema kuwa kufuatia uamuzi uliotolewa na Jaji huyo
anaiomba mahakama hiyo kumpa muda wanasiliane na mteja wake (Lema) kuhusiana na suala la Jaji kutakiwa kujiengua katika kesi hiyo.
Jaji Mujulzii alisema kuwa kutokana na mapumziko ya shughuli za
mahakama mwisho wa mwaka ambapo alisema kuwa suala la kesi hiyo
kuongezewa muda kama ilivyoombwa awali mchakato unaendelea
Kwa upande wake Alute alimwomba Jaji huyo kutupilia mbali maombi ya
Kimomogolo ya kutaka ajitoe kwa madai kuwa anahitaji muda ili
akazungume na mteja wake, kutokana na suala la ushahidi uliotolewa juu ya kuingilia uhuru wa mahakama kuisha kwani haijaweza kuthibitika kuwa yaliyonukuliwa kwenye gazeti ni sahihi.
“Ambaye hamtaki Jaji Mujulizi atakata rufaa kwa hiyo baada ya hapa
kazi inaanza”alisema Jaji huyo ambaye aliahirisha kesi hiyo hadi
Fabruari 6 mwakani.