MAHAKAMA nchini Uingereza imetoa maamuzi kuwa wazee watatu wa Kenya ambao waliteswa na majeshi ya utawala wa kikoloni wa Uingereza wanaweza kufungua mashtaka dhidi ya Serikali ya Uingereza, na hivyo kuendelea mbele madai yao mengine ya ukatili. Maamuzi hayo yametolewa Oktoba 05, 2012 katika mahakama hiyo mjini London.
Serikali ya Uingereza ambayo kwa miaka mitatu imekuwa ikiajribu kuzuia hatua zozote za kisheria kuchukuliwa, imesema leo kuwa imesikitishwa na uamuzi huo na kwamba inapanga kukata rufaa. Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza imesema kuwa haipingi kuwa kila mdai wa kesi hiyo alinyanyaswa na kuteswa wakati wa utawala wa kikoloni, lakini hata hivyo itakata rufaa kutokana na kwamba maamuzi hayo yanaweza kuwa na madhara makubwa ya kisheria.
Wazee hao Paulo Nzili mwenye umri wa miaka 85, Wambugu Wa Nyingi mwenye umri wa miaka 84 na Jane Muthoni Mara mwenye umri wa miaka 73, walifanyiwa ukatili wa aina mbalimbali ikiwemo kuhasiwa, kubakwa na kupigwa wakiwa kizuizini katika miaka ya 1959, wakati wa ukandamizaji wa majeshi ya utawala wa Uingereza na washirika wao wa Kenya wakati wa harakati za Mau Mau kupigania uhuru pamoja na ardhi.
Wazee hao watatu wanaitaka Uingereza kuwaomba radhi na kuwalipa fidia kwa manufaa ya waathirika wote walioteswa na majeshi ya ukoloni. Wakati maamuzi hayo yanatolewa, wazee hao watatu hawakuwepo mahakamani mjini London. Wafuasi wa wazee hao waliokuwa wapiganaji wa Mau Mau walikumbatiana na kufuta machozi ya furaha katika mahakama hiyo, baada ya Jaji Richard McCombe kutoa maamuzi hayo.
Mwaka 2011, Jaji McCombe alitupilia mbali hoja ya serikali ya Uingereza ambayo ilisema kuwa matukio yaliyotokea wakati wa vita vya Mau Mau yalitokea wakati Kenya ikipigania uhuru wake 1963. Kwa mujibu wa Uingereza, madai hayo yametolewa muda mrefu baada ya muda halisi wa kisheria kupita.
Wakili anayewatetea wazee hao, Martyn Day, ameitaka serikali kuacha kutumia sababu za kisheria kupambana na kesi hiyo na badala yake ikubaliane namna ya kuimaliza kesi hiyo mapema iwezekanavyo kutokana na wapiganaji hao wa zamani wa Mau Mau kuwa dhaifu na wazee.
Nzili aliyelazimishwa kujiunga na Mau Mau mwaka 1957 na ambaye alijiondoa kwenye harakati hizo miezi sita baadae, alikamatwa akiwa nyumbani kwake. Alihasiwa wakati yuko kizuizini kwenye kambi ya Embakasi. Nyingi, ambaye hakuwa kabisa mwanaharakati wa Mau Mau, alikamatwa mwaka 1952 na kuwekwa kizuizini kwa miaka tisa bila kufunguliwa mashtaka yoyote. Aidha, Nyingi alikuwa akipigwa mara kwa mara, likiwemo tukio ambalo wenzake 11 walipigwa hadi kufa na yeye kujeruhiwa vibaya huku akiwa ameacha kwenye rundo la maiti kwa siku tatu.
Mara ambaye wakati huo alikuwa msichana mwenye umri wa miaka 15, alinyanyaswa kingono, ikiwemo kubakwa kwa kuingiziwa chupa ya soda iliyokuwa na maji ya moto kwenye sehemu zake za siri.
Maelfu ya waasi waliuawa na majeshi ya kikoloni na inakadiriwa kuwa Wakenya 150,000, wengi wao wakiwa hawahusiki na harakati za Mau Mau, waliwekwa kizuizini katika kambi ambazo zinafananishwa na kambi za kazi zilizokuwa zikisimamiwa na shirika la Gulag wakati wa utawala wa Kisovieti.
-DW