MAHAKAMA YAAMURU ASKOFU MOKIWA AKAMATWE

 
  

 

 Na Janeth Mushi, Thehabari, Arusha

 
 MAHAKAMA Kuu Kanda ya Arusha, chini ya Jaji Kakusulo Sambo
imeamuru kukamatwa kwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Dk. Valentino Mokiwa
na Stanley Hotay kwa kukiuka amri ya Mahakama na kumsimika Askofu, Stanley
Hotay.
Amri hiyo imetolewa ikiwa ni siku mbili tangu kusimikwa kwa askofu huyo, ambapo Ijumaa iliyopita mahakama
hiyo ilisitishwa kusimikwa kwa Askofu Hotay kutokana na kesi iliyofunguliwa
dhidi yake na waumini wa kanisa hilo, ambapo Askofu Hotay aliingia katika
mgogoro wa kikatiba kuhusiana na umri wake.
 
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa sherehe za kumsimika askofu
huyo zilifanyika Makao Makuu ya Dayosisi hiyo ya Mount Kilimanjaro na kuongozwa
na Askofu Mokiwa, ambapo alieleza kuwa sherehe zilizofanyika ni za kumsimika
Askofu wa Kanisa la Anglikana na si Askofu wa kanisa hilo Dayosisi hiyo, na kwamba kusimikwa rasmi
kungelifanywa baada ya mashauri yaliyoko mahakamani kumalizika. 
Katika
kesi hizo moja ya madai namba 18/2011 na Jinai namba 48/2011 zilifunguliwa
dhidi ya Wadhamini wa Kanisa hilo na Askofu Mteule wa Dayosisi hiyo, Hotay na Bw. Lothi Oilevo, Bw. Godfrey Mhone na Bw. Frank Jackob pamoja na mambo mengine waliiomba Mahakama kuzuia kusimikwa
kwa askofu huyo kwa madai ya kuchakachua umri.
 
Akinukuuvifungu mbalimbali vya sheria, Jaji Sambo alisema Askofu Mokiwa na Hotay
walichokifanya kwa yeyote ni ukiukaji wa amri ya mahakama “Nimeridhika kuwa
amri halali ya mahakama imekiukwa na ieleweke bayaha kuwa nchi hii inatawaliwa
na Utawala wa Sheria na hilo limekuwa likisisitizwa mara kwa mara na rais wetu
(Jakaya Kikwete) na viongozi wengine wajuu,”
alisema Jaji Sambo.
 
 Aliieleza mahakama kuwa ma-askofu hao wamefanya kitendo muhimu kilichosababisha amri ya
mahakama isiheshimiwe jambo ambalo ni hatari kwa utawala wa sheria; “kama anasema utanifanya na kuingilia hata kukiuka amri ya
Mahakama Kuu sembuse, mahakama zingine za chini itakuweje!..hivyo mahakama ni
wajibu wake kutumia vifungu kadha wa kadha kama kifungu cha 114 (i) C na K na
(iii) pamoja na kifungu namba 124 vinavyoipa mahakama hii kuwaadhibu wale
watakaokiuka amri ya mahakama…huwezi kuacha mahakama inachezewa na vifungu
vyote hivyo vipo…sasa naamuru…ni amri ya dola kuwa Askofu Dk. Mokiwa na Hotay
wakamatwe mara moja”.
Awali Jaji huyo alisema walalamikaji waliwasilisha mahsuri hayo mahakamani na kuomba
itolewa amri ya kuzuia sherehe hizo kimya kimya lakini kwa busara na mahakama
hiyo ikaamua kuuita upande mwingine ambao nao ulitoa pingamizi la awali
lililotaka ombi hilo liondolewa na sherehe za kumsimika Askofu huyo zifanyike
lakini baada ya mahakama kuona muda wa kutoa maamuzi ni mfupi iliamuru sherehe
hizo kusimama hadi uamuzi wa mahakama utakapotolewa jana (Jumatatu).
 
Alidai kuwa pamoja na jitihada zote hizo za kutumia busara wao waliendelea na
kumsimika mchungaji huyo kuwa Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, wakati
mahakama iliona si busara kuendelea na zoezi hili wakati wapo watu wengine
wakipiga kelele juu ya hilo, lakini kabla mahakama hiyo haijatoa maamuzi, wao
wamemwapisha, na sasa ni kuwa mwenendo mzima wa shauri hilo hauna maana yoyote
kwani ni kweli kabisa kuwa ni ngumu kumtoa Uaskofu maana yake ni kwamba
mwenendo mzima wa mashauri hayo umevamiwa.
Jaji huyo alisema wadai katika madai yao walieleza
 
 kuwa Katiba ya Kanisa hilo inaelekeza kuwa mgombea kiti hicho anayeweza kukalia kiti hicho lazima awe na
miaka kati ya 40 na 60 ndipo anapoweza kukabidhiwa dhamana ya kuwa kiongozi wa
ngazi hiyo, ambapo Askofu huyo alidaiwa kuwa mwaka jana alikuwa anayo miaka 38
tu.
Awali, wakili wa Upande wa Madai Meinrad D’souza aliileza mahakama hiyo kuwa amri
iliotolewa na Mahakamam hiyo haikutekelezwa hivyo sherehe za kumsimika Uaskofu
Hotay zilishafanyika Jumapili iliyopita jambo ambalo ni kukiuka amri halali ya
mahakama, hivyo kwa ukiukaji huo aliiomba mahakama hiyo kwa vya sheria
vilivyopo kuwakamata wahusika wakuu wa tukio hilo ambao ni Askofu Mokiwa na
Hatay.
 
“Mheshimiwa Jaji kabla ya kuendelea na lolote kuna jambo muhimu limetokea kutokana na amri
ya mahakama yako iliyotolewa Ijumaa iliyopita, amri hiyo imekiukwa na sherehe
za kumsimika Askofu Stanley Hotay zimefanyika Makao Makuu ya Dayosisi ya Mount
Kilimanjaro, upo ushahidi wa kutosha juu ya hilo na kwamba kwa mujibu wa katiba
ya Kanisa Askofu kupatikana kwa kuchaguliwa kutoka katika Dayosisi husika,
labda hiyo ni utaratibu mpya wa kuwapata maaskofu”aliongeza D’souza.
Akijibu
hoja hizo, Wakili Tadayo alisema kilichofanyika ni kumsimika Uaskofu wa Kanisa
hilo Tanzania na si Askofu wa Dayosisi hiyo na kwamba kitendo cha kumsimika
uaskofu hakina maana kuwa ndiyo Askofu wa Dayosisi hiyo, kitendo hicho na cha
awali na iwapo shauri litaisha mahakamani atasimikwa rasmi kuwa Askofu wa
Dayosisi hiyo, hivyo aliomba Mahakama hiyo kuendelea kusoma maamuzi wa mahakama
juu ya maombi ya walalamikaji.