Serikali imesema uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi itakayoshughulikia migogoro na masuala mbalimbali ya usatawi wa Waislamu nchini umefikia katika hatua nzuri.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema jana wakati akijibu hoja za wabunge zilizojadili kwenye hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara na Taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
Alisema itaanzishwa wakati wowote baada ya maandalizi kukamilika na kwamba utekelezaji wake uko katika hatua nzuri baada ya kamati ndogo iliyoteuliwa na Waziri wa Katiba na Sheria yenye wawakilishi wa Waislamu na Serikali imetoa taarifa yake ya mwanzo ya namna ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi.
Waziri Mkuu alisema mambo yatakayoshughulikiwa na mahakama hiyo ni pamoja na ndoa na talaka, mirathi, wosia, hiba/zawadi na wakifu vilevile itahusika na mashauri ya jinai.