Mahakama ya Afrika Yaibana Burkina Faso Kesi ya Mauaji ya Mwandishi

Jaji Niyungeko akisoma hukumu ya  Zongo.

Jaji Niyungeko akisoma hukumu ya Zongo.


Na Mtuwa Salira, EANA

NI karibuni miaka 16 sasa baada ya kuuawa kwa mwandishi wa habari za uchunguzi wa nchini Burkina Faso, Norbert Zongo, hatimaye haki imetendeka juu yake baada ya hukumu ya kihistoria iliyotolewa na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (ACHPR) yenye makao yake jijini Arusha.

Katika hukumu hiyo iliyotolewa mwishoni mwa wiki, ACHPR iliamuru Burkina Faso kuifungua na kuisikiliza upya kesi hiyo iliyohusisha pia mauaji ya watu wengine watatu.

Hukumu hiyo iliyosomwa karibu kwa muda wa saa moja mbele ya jopo la majaji 10 lilokuwa likiongozwa na Jaji Kiongozi, Gerard Niyungeko, ilimuru pia serikali ya Burkina Faso kuchukua jukumu la kuwasaka na kuwapata watuhumiwa wa mauaji hayo.

Mahakama hiyo iliielekeza serikali ya Burkina Faso kuhakikisha kufanya kila linalowezekana kuwafikisha watuhumiwa husika kwenye vyombo vya sheria ili nao wapate haki wanayostahili kisheria.

Serikali ya Burkina Faso ilifunga jalada la kesi hiyo mwaka 2006 kwa maelezo ya kukosa ushahidi.
Mahakama pia imeamuru serikali ya nchi hiyo kuzilipa fidia ya zaidi ya dola za Marekani milioni 1, familia za watu hao waliouawa.

Inadaiwa kwamba Zongo aliuawa akiwa na wenzake hao watatu alipokuwa anafanya harakati za kuandika habari za uchunguzi wa dereva wa kaka yake Rais aliyepinduliwa wa Burkina Faso, Blaise Compaore mwaka 1998.

Mwandishi huyo wa habari za uchunguzi na Mhariri wa gazeti la kila wiki la L’Independent na wenzake walipatikana wakiwa wamechomwa moto hadi kufa wakiwa katika gari yao karibu kilometa zipatazo 100 kutoka makao makuu ya nchi hiyo, Ouagadougou.