Mahakama Kuu yasitisha Kafulila kuvuliwa ubunge

Mbunge Kafulila akizungumza bungeni

MBUNGE wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila amepata amri ya Mahakama Kuu ya kuzuia utekelezaji wa uamuzi wa chama chake kumvua uanachama.Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi, ilimvua uanachama Kafulila, Desemba 18, mwaka huu, siku 10 baada ya kumwengua kwenye nafasi ya Katibu Mwenezi wa chama hicho kwa tuhuma za kutoa siri za chama.

Amri hiyo ya Mahakama Kuu imetolewa siku chache baada ya Kafulila kufungua kesi namba 218/2011 akipinga uamuzi huo na kuomba zuio la utekelezaji wake hadi kesi yake ya msingi itakapomalizika.

Katika maombi yake, Kafulila aliitaka Mahakama itengue utekelezaji wa uamuzi huo wa chama chake ili aendelee kuwa mwanachama na mbunge wakati kesi ya msingi ikiendelea. Wakili wa Kafulila, Daniel Welwel alisema jana kuwa ombi la mbunge huyo wa Kigoma Kusini kuzuia utekelezaji wa uamuzi wa chama chake, limekubaliwa.

Alisema ombi hilo lilikubaliwa jana kwa zuio lililotolewa na Jaji Alice Chingwile wa Mahakama Kuu na utekelezaji wake umeanza mara moja na kwamba utaendelea hadi hapo kesi ya msingi itakapomalizika.

“Amepata ‘Injunction’ kuzuia utekelezaji wa uamuzi wa Halmashauri Kuu (ya NCCR-Mageuzi) kumvua uanachama mpaka kesi ya msingi itakaposikilizwa,” alisema Welwel.

Alipoulizwa kama tayari Kafulila ameshawasilisha hati ya zuio hilo kwa viongozi wa NCCR-Mageuzi, alisema hajafanya hivyo kwa kuwa ndiyo kwanza walikuwa wamepata amri hiyo ya mahakama.

Awali, Kafulila alisema kwa kutolewa amri hiyo, ataendelea na majukumu yake ya ubunge kama kawaida na kuwataka wananchi wake kutokuwa na wasiwasi…
“Kikubwa ni kwamba nitaendelea kuwatumikia wananchi wangu (Kigoma Kusini) hivyo wasiwe na wasiwasi,” alisema Kafulila.

Kafulila alifukuzwa uanachama pamoja na wenzake watatu, akiwamo aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho katika uchaguzi wa mwaka jana, Hashim Rungwe.

Mbunge huyo kijana kabla ya kuvuliwa uanachama, Halmashauri ya NCCR-Mageuzi ilipokaa, aliingia katika ukumbi wa mkutano huo akiwa na nguvu na matumaini ya kumsimamisha uongozi Mwenyekiti wa chama chake, James Mbatia lakini upepo ulivuma vibaya kuelekea upande wake na hatimaye akajikuta akisulubiwa kwa kuvuliwa uanachama.

Kafulila alitokea Chadema kujiunga na NCCR- Mageuzi, mwishoni mwa mwaka juzi. Mwaka jana alifanikiwa kuingia bungeni baada ya kumshinda mgombea wa CCM, Kifu Gullamhussein.

Mwanasiasa huyo alianza kung’ara katika medani za siasa nchini kutokana na kusimamia hoja zenye maslahi ya umma kama Katiba Mpya, kupinga nyongeza ya posho za wabunge na kutaka wale ambao walisababisha hadi Dowans kupata tuzo ya zaidi ya Sh100 wachukuliwe hatua.

Safari ya kumshughulikia Kafulila ilianzia Desemba 8, mwaka huu baada ya kuvuliwa wadhifa wa Katibu Mwenezi wa chama hicho na baadaye kuhitimishwa kwa kumfukuza uanachama.

Wajumbe 64 wa mkutano huo wa Halmashauri ya NCCR-Mageuzi walifika katika ukumbi wa mkutano wakionekana kuwa na shauku ya kutaka kujua hatima ya chama hicho baada ya kuibuka kwa mvutano baina ya Kafulila, Mbatia na Katibu Mkuu, Samwel Ruhuza.

Katika mkutano huo, Mbatia alikuwa mmoja wa watuhumiwa ambao alipaswa kujibu madai ya kukifanya chama kama CCM B huku Kafulila akituhumiwa kuvujisha siri za chama nje ya utaratibu wa vikao. Moja ya tuhuma za Kafulila ni kueleza vyombo vya habari kwamba ameondolewa katika nafasi ya uenezi.

Tuhuma dhidi ya Mbatia zilitolewa na Kamishna wa chama hicho Mkoa wa Tanga, Mbwana Hassan pamoja na wengine 26 waliosaini hati ya kutokuwa na imani naye.

Hata hivyo, akizijibu shutuma hizo mbele ya waandishi wa habari Ruhuza alisema kuwa mkutano huo ulitoa maazimio kwamba Mbatia yuko safi, hodari na shujaa wa chama.

“Wajumbe wote waliotoa malalamiko walijiondoa na Mbatia akawa safi hiyo ikiwa ni pamoja na hao waliokuwa wakimpinga awali,” alisema Ruhuza.

CHANZO: Mwananchi