Mahakama EAC kuzindua ofisi ndogo kila nchi mwanachama

Nembo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)

Na Nicodemus Ikonko, EANA, Arusha

MAHAKAMA ya Afrika Mashariki (EACJ) mwezi ujao itazindua rasmi ofisi ndogo za mahakama hiyo katika kila nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ili kusogeza huduma hiyo muhimu karibu na wateja wake.

Msajili wa Mahakama hiyo Profesa John Ruhangisa aliliambia Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) katika mahojiano maalum hivi karibuni kuwa hatua hiyo inalenga raia katika kanda hiyo kuzifahamu vizuri kazi za mahakama hiyo pamoja na Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) ambazo zote kwa pamoja ni nguzo muhimu katika kuimarisha uhai na mtangamano unaoendelea hivi sasa.

“Mpango huo uliidhinishwa na Baraza la Mawaziri la EAC katika kikao chake cha Novemba mwaka jana,” alifafanua Prof. Ruhangisa katika mahojiano hayo yalifanywa kwa lugha ya Kiingereza na itapatikana kwenye vyombo vya habari hivi karibuni pia katika lugha za Kiswahili na Kifaransa. Nchi wanachama wa EAC ni pamoja na Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi.

Wakati huo huo Prof. Ruhangisa aliiambia EANA pia kwamba mamlaka ya EACJ yatapanuliwa katika siku za usoni kushughulikia pia kesi za makosa ya jinai zikiwemo za mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu. Alisema mabadiliko hayo ni kwa mujibu wa maelekezo ya kikao cha hivi karibuni cha wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.

“Ni kweli kwamba upanuzi wa mamlaka ya Mahakama hii yatahusisha pia mashitaka ya uhalifu dhidi ya binadamu na hii ni kwa mujibu wa maelekezo ya Kikao cha Wakuu wa Nchi wananchama. Inamaanisha kwamba Mahakama hii itakuwa na uwezo wa kushughulikia mashitaka kama vile ya mauaji ya kimbari na mengine kama vile ya watuhumiwa wa Kenya ambao kesi yao sasa ipo mbele ya ICC (Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai),” Profesa Ruhangisa alifafanua.

Alieleza kwamba vyote viwili, Mahakama na Jumuiya ya EAC vina majaji wenye uwezo wa kushughulikia kesi za aina hii.

Lakini alikiri pia kwamba kuna vikwazo. Alisema upatikanaji wa rasilimali watu na fedha za kugharimia upanuzi huo ni miongoni mwa changamnoto iliyopo. Mambo haya yanatakiwa kupatiwa ufumbuzi kwanza, aliongeza.

Alifafanua kwamba ili mahakama iweze kushughulikia kesi za jinai kunahitajika kuanzishwa kwa idara mbalimbali ikiwa ni pamoja na za mwendesha mashitaka, upelelezi, ulinzi wa mashahidi na magereza.

“Inawezekana kiufundi na kiutekelezaji lakini masuala mengi yanahitajika kufanyiwa kazi na kupatiwa ufumbuzi kabla ya kuelekea rasmi upande huo,” alishauri.

Iwapo EACJ itafanikiwa kufikia hatua hiyo ya upanuzi wa mamlaka yake kushughulikia kesi za jinai, itakuwa imelamba ‘bingo’ ya hatma yake ya kuweza kushughulikia matatizo yake yenyewe katika kanda ya EAC. Na pia kamwe kutoshuhudia tena mauaji yaliyotokea Rwanda mwaka 1994 na yale ya Kenya kufuatia ghasia zilizozuka baada ya uchaguzi mkuu. Hivi sasa EACJ inashughulikia mashauri yanayohusu zaidi madai.