Mahakama Arusha yawabwaga madiwani waliotimuliwa Chadema, kibao chaigeukia Serikali kuwalipa

 

Na Janeth Mushi, Arusha

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoani Arusha jana imetupilia mbali kesi ya madai namba 17/2011 iliyofunguliwa Agosti 10 mwaka huu na madiwani watano waliopinga kuvuliwa uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Hakimu wa Mkazi wa Mahakama hiyo, Hawa Mguruta akitupilia mbali kesi hiyo mahakamani alisema Mahakama haiwezi kuingilia uamuzi ya Kamati Kuu ya (CHADEMA) ambapo chama hicho kimesajiliwa kisheria kama chama cha siasa hivyo maamuzi waliyoyatoa kwenye chama hicho ni sahihi.

Mguruta alidai kuwa Mahakama hiyo haiwezi kukiuka katiba ya chama
hicho pamoja na maamuzi yote yaliyofikiwa huku akinukuu kesi
mbalimbali ziliwahi kuamuliwa na mahakama mbalimbali nchini.

Baada ya uamuzi huo kutolewa na Hakimu Mguruta, baadhi ya madiwani
waliovuliwa uanachama ambao walifika mahakamani hapo akiwemo aliyekuwa Naibu Meya wa Manispaa ya Arusha Estomih Mallah, John Bayo na Reuben Ngowi walisema kwa pamoja hawana la kusema juu ya uamuzi huo wa Mahakama.

Wakili wa upande wa utetezi Method Kimomogolo katika pingamizi zake
alizoziwasilisha mahakamani kwa njia ya maandishi alidai kuwa Mbowe
hawezi kushtakiwa binafsi, Chadema haiwezi kushtakiwa kwa jina lake,
maombi ya kufukuzwa uanachama yamepitwa na wakati kwani madiwani hao walishakata rufaa Baraza Kuu la Chama hicho na Mahakama haina uwezo wa kusikiliza ksi hiyo bali Mahakama Kuu ndio yenye uwezo.

Awali wakati Chadema wakilalamikia madiwani hao kufukuzwa uanachama wao Waziri Mkuchika alindika barua yenye kumbukumbu namba HA.23/235/01/06 iliyotolewa Agosti 23 na kumfikia Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Estomih Chang’ah ambapo ilidai Tamisemi bado inawatambua madiwani hao na watandelea kulipwa posho zao hadi hapo mahakama itakapotoa uamuzi kama madiwani hao watano ni wanachama halali wa Chadema au la.

Barua hiyo pia ilidai mahakama ndio muamuzi wa mwisho hivyo ni vyema suala hilo likasubiriwa kutolewa maamuzi lakini madiwani hao
wataendelea kuhudhuria vikao na kulipwa posho zao.

Mkurugenzi Chang’ah awali alipozungumza na waandishi wa habari
alisema alipokea barua hiyo kutoka kwa Mkuchika yenye maelezo hayo
hapo juu kutokana na barua ya awali ya aliyoindika MD/ US/101/ 1/107
Agosti 12 mwaka 2011.

Aliongeza kuwa suala la madiwani hao kuendelea kuwa madiwani ni
uamuzi utakaotolewa na mahakama kwani walishafungua kesi ya madai
hivyo mahakama ndio yenye kutoa maamuzi kisheria na barua hiyo
imetolewa na nakala kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isdore Shirima,
Katibu Mkuu, Wilbroad Slaa pamoja na Waziri Mkuu, Peter Pinda.

Alisema Sheria ya Serikali za Mitaa namba 8 ya mwaka 1982 kifungu cha 26 (1) (e) kinafafanua kuwa waziri mwenye dhamana na serikali za
mitaa atatamka kuwa nafasi ya diwani iko wazi baada ya kupokea
taarifa rasmi ya maandishi kutoka kwa Mwenyekiti au Meya wa Jiji la
Arusha.

Nje ya mahakama umati wa wananchi waliokuwa wamehudhuria kesi hiyo walikata miti na kuanza kuimba nyimbo mbalimbali za ushindi hadi Ofisi ya Mbunge wao, Godbless Lema huku polisi wakiwasindikiza bila kutumia nguvu ya aina yoyote.

Madiwani hao ni John Bayo, Ruben Ngowi, Charles Mpanda, Rehema
Mohamed na Estomii Mallah ambao walikuwa wamefungua kesi hiyo kupinga kuvuliwa uanachama na kupinga kusemwa vibaya kwenye mikutano ya hadhara itakayofanywa na chama hicho

Kwa upande wake Mbunge Lema akizungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake alisema hakuna mbunge anayefurahia kupoteza madiwani
wake watano aliowapata kwa gharama lakini ikiwa madiwani hao wanakiuka sheria na kanuni hakuna jinsi lazima watoke.

Kufuatia hali hiyo mbunge huyo alidai kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu Tawala za Serikali na Mitaa (TAMISEMI) na Mkurugenzi wa
Manispaa ya Arusha Estomih Chang’ah kuwa wajiandae kwani CHADEMA
itawafungulia kesi kutokana na Mkuchika kuamuru madiwani hao
waliofukuzwa uanachama kuendelea na vikao na kulipwa posho zao hadi
hapo mahakama itakapotoa uamuzi juu ya kufukuzwa kwao uanachama.

Alisema kutokana na ushindi walioupata wametoa televisheni tano, taulo
za kike, kompyuta 1 na pinta kwa mahabusu na wafungwa waliopo gereza Kuu la Arusha na kuongeza kuwa uchaguzi wa Meya urudiwe upya ingawa hawatashinda lakini ni bora urudiwe kwani Chadema hawamtambui Meya, Gaudence Lyimo, ili hata kama ni kushinda awe ameshinda kihalali.