‘Magonjwa ya Polio, Surua kubaki historia Tanzania’

Makamu wa Rais DK. Gharib Bilal akipata maelezo kutoka kwa mtoa huduma wa afya kabla ya kutoa matone ya Vitamin A wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Chanjo ya Kitaifa ya Surua,utoaji wa matone ya Polio, Vitamin A na dawa ya minyoo uliofanyika leo kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid Karume, Arusha Picha na MAGRETH KINABO – MAELEZ0

Na Magreth Kinabo- MAELEZO, Arusha

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imesema itahakikisha magonjwa ya polio na surua na mengineyo ambayo yanaweza kukingwa kwa chanjo yanatokomezwa ili yabaki kuwa historia.

Kauli hiyo imetolewa leo mjini hapa na Makamu wa Rais DK. Gharib Bilal wakati akizindua Kampeni ya Chanjo ya Kitaifa ya Surua na utoaji wa matone ya Polio, Vitamin A na dawa ya minyoo hafla iliyofanyika kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

“Ili kufanikisha azma hiyo, Serikali imehakikisha kwamba, viwango vya chanjo kwa watoto na wakina mama wajawazito vinaendelea kuongezeka na hata kupita malengo yaliyowekwa, kitaifa na kimataifa kwa kutumia kigezo cha chanjo ya ‘pentavalent’ inayozuia magonjwa ya kifaduro, donda koo, pepo punda na homa ya ini, homa ya uti wa mgongo na kichomi,” alisema Dk. Bilal.

Aliongeza kuwa kiwango cha chanjo hiyo kimeongezeka kutoka asilimia 85 mwaka 2005 hadi asilimia 91 mwaka 2010. Wakati huo huo mataifa mengine bado hajafikia hata lengo la asilimia 85. Dk . Bilal alisema kiwango cha chanjo ya suruakimefika asilimia 92 .kampeni hiyo inafanyikia kwa siku nne nchini kote na kauli mbiu yake ni ‘Chanjo ni Haki ya Kila Mtoto.’

“Kwali hiyo basi, wananchi wote mnasisitizwa kujitokeza kuwaleta watoto ili chanjo hii, iwafikie wote kwa asilimia 100,” alisisitiza.

Aidha Makamu huyo wa Rais alisema kukamilishwa kwa chanjo hizo, kutowasaidia watoto wote kutopata maradhi mbalimbali, ambayo yanazuilika kwa chanjo na hivyo kuwa na afya njema.

“Kukamilishwa kwa chanjo kutaiwezesha serikali kutumia fedha ambazo zingetumika kugharamia wagonjwa na matibatu ziweze kutumika katika miradi mingine muhimu ya maendeleo na kufanikisha kauli ya ‘maisha bora kwa kila Mtanzania’.

Naye Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda alisema wizara yake inatarajia kuanzisha chanjo nyingine kwa ajili ya kuzuia vichomi kwa watoto na magonjwa ya kuhara, kuanzia Januari Mosi, mwaka 2012.

Aliongeza kuwa uanzishaji huo unahitaji maandalizi ,ikiwemo ubadilishaji wa ratiba ya chanjo kutoka wiki nne, wiki nane na wiki 10 kwa chanjo ya Polio na Pentavalent na kuwa wiki sita, wiki 10 na wiki 14. Hivyo matumizi ya ratiba hiyo mpya yataanza rasmi Januari Mosi, mwaka 2012.

Dk . Mponda alisema wizara yake itaanzisha chanjo ya kuzuia saratani shingo ya kizazi, ambayo inatarajiwa kutolewa kwa wasichana wenye umri wa miaka tisa, ambapo itatolewa kwa awamu kwenye mikoa ya Dodoma, Dares Salaan na Kilimanjaro.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya la Dunia (WHO), Dk. Rufaro Chatora aliipongeza Tanzania kwa hatua iliyofikia ya utoaji chanjo, ambapo alisema juhidi ziendelee kufanyika kukabiliana na matatizo hayo ili kufikia kiwango cha asilimia 95.

Jumla ya watoto walio chini ya miaka mitano kuanzia miezi tisa milioni 6.7 wanatrajiwa kupatiwa chanjo ya surua, chini ya miaka mitano watoto milioni 7.9 chanjo ya polio, matone ya Vitamin A watoto milioni 7.1 walio na umri wa miezi sita hadi chini ya miaka mitano na milioni 6.2 wenye umri wa mwaka mmoja mpaka chini ya miaka mitano watapewa dawa za minyoo.